November 9, 2020



DAR Dabi imepita na kwa sasa maisha yanaendelea kama kawaida hivyo masuala ya kufikiria nyuma ni kujilisha upepo kwa wakati uliopo.


Kwenye soka kila timu ina haki ya kupata ushindi ikiwa itafanya maandalizi mazuri na kutumia makosa ya wapinzani wake ndani ya uwanja.


Tunaona kwamba sare ya bao 1-1 kwa Yanga na Simba kila mmoja amepokea kwa namna ambavyo alikuwa anatarajia na wengine waliamini kwamba timu moja ingepoteza ila mwisho wa siku dakika 90 ni mwamuzi wa haki kwa timu zote.


Makosa ambayo yamejitokeza ni muhimu kuyafanyia kazi ili kuweza kuwa bora kwa ajili ya mechi zijazo pia mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) upo umuhimu wa kuongeza nguvu kwenye mechi zote za ligi.


Imekuwa kawaida licha ya kwamba ni dabi nguvu kubwa imekuwa ikiwekezwa kwa Yanga na Simba kwa kuwa ni klabu kongwe. Hili naona halipo sawa, timu zote iwe Ihefu, Mbeya City hata Azam FC pia uwanjani wanasaka pointi tatu, muhimu kuzijali zote.

Kwa kufanya hivyo itaongeza umakini na ushindani kwenye ligi yetu ambayo kwa sasa inazidi kukua ndani na nje ya Tanzania hasa kutokana na ubora wake.


Shukrani kwa Azam TV ambao wamekuwa wakirusha mechi nyingi moja kwa moja hili pia linachangia kukuza soka letu na kuwatangaza wachezaji kitaifa na kimataifa.


Kazi ni kwao kuonyesha uwezo ndani ya uwanja na kupambana kwa hali na mali kufikia malengo ambayo wamejiwekea kwenye soka.

Tukiachana na masuala ya dabi hebu tuongeze pia nguvu kwenye timu yetu ya Taifa ya Tanzania. Taifa Stars ina kibarua kigumu mbele cha kukutana na Tunisia katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazotarajiwa kufanyika mwaka 2021 nchini Cameroon.

 

Stars inakutana na Tunisia baada ya kufanikiwa kuingia katika hatua ya makundi kwa kuwaondoa Burundi mapema mwaka jana hivyo kuipata nafasi hiyo adhimu ambayo kila mpenda soka angependa kuona timu yake inafanikiwa kusonga mbele.

 

Stars tayari imeshacheza mechi mbili hadi sasa za kundi J na kupelekea iwe nafasi ya tatu katika kundi hilo ikiwa imeshinda mchezo mmoja na kutoa sare mmoja kabla ya mchezo wa Novemba 13 mbele ya Tunisia.

Mchezo huu ambao utakuwa ni wa tatu kucheza tangu waingie katika hatua ya makundi, ni muhimu kuweza kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo  wa kundi lao.

 

Kikosi cha Stars tayari kimeshatangwazwa na kocha Etienne Ndayiragije ambaye amewaita wachezaji ambao ameona watamfaa katika mchezo huo watakaocheza Novemba 13 nchini Tunisia.

 

Mechi hizi ni muhimu kwa timu yetu kuweza kufanikiwa kushinda ili kufikia malengo ya kushiriki kwa mara nyingine Afcon baada ya ile tuliyoshiriki mwaka jana ikiwa imepita miaka 39 mara ya kwanza.

 

Michuano hii ni muhimu hivyo ni lazima tupate nafasi hiyo kwa mara nyingine tena. Kama nilivyosema mchezo huu ni muhimu, hivyo unahitaji kuungwa mkono na kila Mtanzania ili timu iweze kufanikiwa kuvuka hatua hii ambayo ni ngumu kutokana na kila timu kuhitaji kusonga mbele.

 

Hasa ukizingatia timu tunazokutana nazo pia zina uchu wa kushiriki michuano hii. Wadau mbalimbali wanatakiwa kujitokeza kutoa sapoti kuelekea mechi hii na ile ya marudiano itakayochezwa Novemba 17 Uwanja wa Mkapa.

 

Kwa sababu moja tu, mwisho wa siku tuweze kuibuka na ushindi ambao utatuletea faida huko mbele kwani iwapo timu yetu ya taifa ikifanikiwa kushiriki fainali hizo itasaidia kutangazika kwa nchi yetu na kutuletea manufaa.

 

Aidha kwa upande wa wachezaji waliopewa nafasi hiyo, wanatakiwa kuichukulia mechi hii kwa uzito wa hali ya juu kwa kujitoa  ipasavyo  ili kupata ushindi ili kusonga mbele zaidi katika michuano hii.


 

Baada ya kazi ya kwanza kuwa nchini Tunisia mwisho wa kazi  huku nyumbani itapendeza ikiwa mtapata matokeo chanya mbele ya wapinzani wenu ijapokuwa na huku hamtocheza na mashabiki lakini naamini hakuna kitakachoshindikana.

 

Wachezaji mnatakiwa kuuona mchezo huu kama fainali pia ni sehemu sahihi ya kuonyesha uwezo wenu kwani mechi hizi mnaweza kujiuza katika timu nyingine nje kwa kuwa michezo hiyo huwa inafuatiliwa na baadhi ya mawakala.


Jambo la msingi ni maandalizi mazuri hivyo hatahuko ambapo kambi imewekwa nchini Uturuki ni muhimu kuzidi kuongeza juhudi ili kuwa bora zaidi.


2 COMMENTS:

  1. Nadhani tulishinda moja na kupoteza moja ugenini dhidi ya Libya 2-1

    ReplyDelete
  2. Sioni wapi Taifa stars atapona, TUNISIA oyeeeeee

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic