December 23, 2020

 


DESEMBA 16 dirisha la usajili lilifunguliwa rasmi ikiwa ni ruksa kwa timu za Bongo kufanya usajili wa ajili ya wachezaji.Hii ni fursa kwa benchi la ufundi kutoa ripoti na kuchagua aina ya wachezaji ambao wanawahitaji.

Muda pekee wa kufanya maboresho pale ambapo kuna makosa ni sasa. Hakutakuwa na wakati mwingine kwa timu kuweza kufanya usajili kwa ajili ya msimu wa 2020/21.

Benchi la ufundi kwa mechi ambazo zimechezwa limeona wapi pana tatizo. Nina amini kwamba kila kitu kimeweza kuonekana kwa wakati huu ambapo ligi inaendelea.

Kuanzia kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara zote usajili huu unawahusu kwa wakati huu.

Ni wazi kwamba kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu zinazoruhusiwa kufanya usajili kwa sasa ni zile ambazo hazijakamilisha idadi ya wachezaji wanaotakiwa.

Neno langu ni kwamba mabenchi ya ufundi ni muhimu kuangalia mapema mahitaji yao yapo kwenye nini kwa wakati huu ndani ya timu zao.

Kabla sijaenda mbali ninapenda kuwaomba Watanzania kuendelea kuziombea dua timu ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.

Simba itakuwa na kazi nchini Zimbabwe na itacheza na FC Platinum, leo Namungo itakuwa na kazi mbele ya El Hilal Obeid ya Sudani.

Mashabiki ni jukumu letu kuungana kuwaombea wawakilishi wetu ili wafanye vizuri na wachezaji pia ni jukumu lenu kupambana kupata matokeo.

Nikirudi kwenye mada ambayo nipo nayo leo ninaamini kwamba mabenchi ya ufundi yana jukumu kubwa la kuwasilisha majina ya wachezaji inaowahitaji, kisha uongozi kufanyia kazi katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Kwa wachezaji ambao watapata bahati ya kupata changamoto mpya wana jukumu la kuendeleza juhudi kwenye maisha yao mapya ambayo wanakwenda kuishi.

Imani yangu ni kwamba benchi la ufundi litasimamia masuala ya usajili na kupata wachezaji ambao wanahitaji kwa kufuata taratibu ambazo zimewekwa.

Ikiwa itakuwa hivyo kila mmoja atakuwa na kazi moja ya kutimiza majukumu yake kwa wakati pale ambapo atapewa kazi ya kufanya.

Imani yangu kwa zile timu ambazo zilikuwa zinashindwa kupata matokeo kutokana na kuwa na wachezaji ambao hawana uzoefu muda ni huu.

 

Pia ikumbukwe kwamba usajili wa wakati huu ni mdogo haina maana kwamba kikosi kizima kinasajiliwa hapana ni usajili kwa nafasi ambazo zipo wazi.

Mapendekezo ambayo yatafanyika na benchi la ufundi yatajibu ndani ya ligi kwa kuwa suala la mpira ni mchezo wa wazi.

 

Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa wachezaji watakaopata nafasi kwenye timu mpya ni kuendeleza juhudi kwenye kusaka matokeo ndani ya uwanja.

Lengo la timu kwenye usajili wa mchezaji ni kuona kwamba anapata nafasi ya kuwa ndani ya timu na kufanya yale ambayo yanaleta matokeo chanya ndani ya uwanja.

 

Ikiwa mchezaji atashindwa kuishi kwenye msingi ya mpira itakuwa rahisi kwake kuanguka.Jambo la msingi ni kuona kwamba kila mchezaji habweteki pale anapopata nafasi.


Kujifunza kwa yale ambayo yaliweza kukuweka sokoni ni muhimu kupambana na kuendelea kuyafanya muda wote. Hii ni njia bora ambayo itawafanya wachezaji kuzidi kuwa kwenye ubora wao.

 

Kuwa na kipaji ni muhimu na kuendeleza kipaji ni muhimu pia kwa kuwa kisipoendelezwa ni rahisi kupotea.

 

Benchi la ufundi pia ikiwa litafanya usajili mzuri basi yale malalamiko kwamba wanashindwa kupata matokeo kwa kuwa hawana wachezaji wenye uzoefu nina amini litakwisha.

 

Ipo wazi kwamba kuna timu ambazo mwendo wake ni wa kusuasua ndani ya ligi kwenye kusaka matokeo. Nyingine mwendo wao ni kupwa na kujaa.

Leo inafanya vizuri kesho inakwama kuendelea pale ilipoishia hivyo inakuwa inakwenda mbele na kurudi nyuma. 

Ushindani ndani ya ligi ni mkubwa hakuna ambaye hajui lakini ni muhimu na timu kuwa na mwendelezo mzuri kwenye kusaka matokeo ndani ya uwanja.

Kwa wakati huu mfupi ambao hautadumu kwa muda mrefu ni mrefu pia kwa wale ambao watautumia kwa umakini.

Kwa timu ambazo zina kazi kimataifa leo nina amini zitapambana kusaka matokeo kwa kuwa matokeo mazuri ni furaha kwa Tanzania. 

 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic