January 28, 2021


 KAZI kubwa kwa wawakilishi wetu kimataifa ni kuweza kupeperusha bendera ya taifa la Tanzania kwa mafanikio makubwa hasa kwenye mechi za kimataifa.

Ipo Namungo FC inaiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho ambapo imetinga hatua ya 32 bora kwa hatua ambayo wamefikia wanastahili pongezi.

Wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi wamefanya kazi kubwa kupambana kutoka mwanzo mpaka kufika hapa ambapo wameweza kufika.

Hakuna ambaye anaweza kusema kwamba ilikuwa kazi rahisi kufika hapo ambapo ipo kwa sasa kwenye michuano ya kimataifa.

Kazi ya kwanza inayofuata ni kupata matokeo ugenini kwani mechi zile za mwanzo ambazo iliweza kucheza ilianzia nyumbani hivyo ina kazi nyingine ya kufanya ugenini.

Kwa Afrika soka letu sera yake ni moja kwamba kila mmoja anashinda mechi zake za nyumbani huku ugenini akiwa hana uhakika wa kushinda asilimia kubwa.

Imani yangu ni kwamba kwa namna ambavyo ulimwengu wa soka umebadilika kwa namna yoyote inawezekana kupata matokeo ugenini pia ikiwa wachezaji watajituma.

Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wanapeperusha bendera ya Tanzania na kazi yao ni moja kusaka ushindi kwenye mechi zake zote.

Imetinga hatua ya makundi kwa faida ya ushindi wa nyumbani na ilitinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa ugenini.

Hapo inaleta picha kwamba tayari inajua uzuri wa kushinda ugenini na uzuri wa kutumia uwanja wa nyumbani kwenye kusaka ushindi.

Kwa hatua ambayo wametinga ya makundi wana kazi ya kusaka ushindi ili kuweza kuibuka kwenye hatua ya robo fainali na mwisho wa siku nusu fainali kabla ya kumaliza na fainali.

Haya yote hayatawezekana ikiwa hakutakuwa na maandalizi mazuri kwa wakati huu ambao umebaki kwani muda ni mchache na mashindano yapo karibu.

Februari inakuja kama ambavyo Januari ilikuja na kwa sasa inaelekea kukatika taratibu kwa kasi ambayo hakuna ambaye anatarajia.

Jambo la msingi ni maandalizi hakuna mafanikio ambayo yanaweza kufikiwa kirahisi kwenye ulimwengu wa mpira kwa wakati huu kama hakutakuwa na maandalizi mazuri.

Ikiwa Simba itawekeza nguvu kubwa kwenye mechi za nyumbani kisha ikasahau kwamba kuna mechi za ugenini zile tanotano ilizopokea zama zile za Patrick Aussems kwenye mechi za ugenini zitajirudia.

Uzuri ni kwamba ina historia nzuri na Uwanja wa Mkapa ila rekodi hazichezi na zimewekwa ili zivunjwe kwa namna yoyote kazi ni nzito.

Watanzania wana matumaini makubwa na wawakilishi wetu ambao ni Namungo na Simba kimataifa na kufikia mafanikio ambayo kila mmoja anafikiria ni muhimu kuanza mipango wakati huu.

Kupambana kufika hatua ya nusu fainali haitakuwa rahisi hata kutinga hatua ya robo fainali pia kwa kuwa kila timu inahitaji ushindi ndani ya uwanja.

Wapo wale ambao wanafikiria kwamba itakuwa ngumu kwa Namungo kusonga mbele na itakuwa ngumu kwa Simba kusonga mbele.

Kweli kabisa ugumu upo hilo lipo wazi kwani kila timu inahitaji ushindi ndani ya uwanja sasa kinachotakiwa kwa wawakilishi wetu ni kuweka mipango kazi makini wakati huu kabla ya mashindano hayajaanza.

Kupata ushindi ni faida kwa taifa na timu kiujumla kuzidi kufungua milango ya mafanikio. Pia wachezaji nao wanapandisha thamani zao hasa kwa kufungua ukurasa mpya kwenye soko la biashara.

Kila la kheri wawakilishi wetu na muda wa kuanza kufanya maandalizi ni sasa na imani yetu ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic