MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na ile ya Kombe la
Shirikisho Afrika imezidi kushika kasi katika viwanja mbalimbali barani humu,
ambapo kwa Ligi ya Mabingwa michuano hiyo ipo katika hatua ya makundi huku ile
ya Shirikisho ikiwa katika hatua ya mtoano.
Hongera kwa Simba ambao wameanza vyema kibarua chao kwa
ushindi wa ugenini dhidi ya AS Vita katika mchezo wao wa kwanza wa kundi A,
ushindi huo unatoa mwanga mzuri kwa Simba katika kuhakikisha wanafikia malengo
yao ya angalau kufika nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu
barani Afrika.
Simba wanastahili pongezi kutokana na uimara mkubwa
waliouonyesha kwenye mchezo huo kwa kulinganisha na mchezo wa mwisho dhidi ya
AS Vita, katika hatua kama hiyo msimu wa 2018/19 ambapo katika msimu huo Simba
walikubali kipigo cha mabao 5-0.
Jukumu lililosalia kwa Simba hivi sasa ni kuhakikisha moto
walioanza nao hauzimiki, bali wanaendelea kushikilia hapo hapo na ikiwezekana
kuongeza ufanisi zaidi katika michezo yao mitano iliyosaliwa nayo, ili kufuzu
hatua ya robo fainali na ikiwezekana nusu fainali kama yalivyo malengo yao.
Kama Watanzania wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaendelea
kuwaombea kheri Simba kwani mafanikio yao ni mafanikio ya soka la Tanzania kwa
ujumla, kama tujuavyo kama Simba watafika mbali kwenye michuano hii basi
Tanzania itazidi kuvuna pointi nyingi kiasi cha kuongeza namba za timu shiriki
kutoka mbili za sasa hadi nne.
Lakini pia pongezi kwa wawakilishi wa Tanzania katika
michuano ya kombe la Shirikisho Afrika Namungo, ambao wao wamefanikiwa kupenya
hadi katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo na kwa sasa wanaikimbizia tiketi
ya hatua ya makundi.
Namungo inayoonekana kupitia kwenye kipindi kigumu ndani ya Ligi Kuu
Bara, imeonyesha uhai mkubwa katika michuano ya kimataifa kwa kuziondosha timu
mbili kutoka nchi za Sudani na Sudani ya kusini.
Licha ya mafanikio ya michuano hiyo ya kimataifa, lakini kuna
mdudu ameingia ambaye anafanya kuanze kuwepo mashaka juu ya ufanisi na
mafanikio ya michuano hiyo, changamoto hiyo ni ile ya baadhi ya klabu kuanza
kutumia faida ya kuwepo maambukizi ya Corona kwenye baadhi ya nchi kama sehemu
ya kudhoofisha wapinzani.
Ishu hii ilianza kuibuka wakati wa michuano ya kombe la
mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani CHAN iliyofanyika nchini
Cameroon kuanzia Januari 16 hadi Februari 7, mwaka huu.
Kupitia michuano hiyo kocha wa DR Congo, Florent Ibenge
aliweka wazi kwamba baadhi ya nyota wa kikosi chake pamoja na yeye mwenyewe
walipakaziwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona ili kuidhoofisha timu yao.
Baada ya kuwa kama stori kwa wenzetu tukio hilo pia limetokea
kwetu Watanzania kupitia Klabu ya Namungo ambayo ilipata wakati mgumu nchini
Angola kufuatia kudaiwa baadhi ya nyota wake wameambukizwa virusi vya Corona.
Hali hiyo ilileta sintofahamu kubwa kiasi cha Shirikisho la
soka Tanzania (TFF), kuingilia kati na kuwasiliana na Shirikisho la soka Afrika
(CAF), na kupelekea mchezo huo kufutwa kupisha uchunguzi.
Kwa hili nadhani TFF wanastahili pongezi kubwa kwa kusimamia
maslahi ya Taifa katika mchezo wa soka.
Uchambuzi wa Lunyamila kupitia gazeti la Championi Jumatatu
TFF iendelee kupambana kuhakilisha timu zetu hazionewi ovyo na hao wahuni. Hili suala ni la kulishikia bango iliwezekana hiyo klabu ya angola inatolewa kabisa ktk mashindano ili haya mambo ya kunyanyasana yaishe. Kama angola hakuna corona na hawataki maambukizi basi wajitoe kwenye mashindano wabaki wagumu.
ReplyDelete