TAYARI ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara
imewekwa wazi na mzunguko wa 19 unatarajiwa kurejea ndani ya ardhi ya Bongo.
Tayari zipo mechi za viporo ambavyo vilitokana na timu
mbili kuwa kwenye mashindano ya mechi za kimataifa ambazo ni Namungo FC pamoja
na Simba.
Kwa jana kila mmoja ameweza
kushuhudia namna timu hizo zilivyojuwa zikisaka ushindi ndani ya uwanja na
mwisho wa siku kila mmoja akapata kile ambacho alikuwa anahitaji.
Kwa upande wa Namungo FC wao wapo
kwenye hatua ya 32 bora Kombe la Shirikisho huku Simba wakiwa hatua ya makundi
Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupenya kwenye hatua za mwanzo walizoanza
nazo.
Kwa hatua ambayo wameweza kufika
kwa sasa wanastahili pongezi kwani sio kazi rahisi kuwa hapo. Yote kwa yote na
wadau pia ikiwa ni pamoja na mashabiki nao pia wanastahili pongezi kwa kutoa
sapoti kwenye mechi ambazo zilikuwa zinachezwa uwanjani.
Pia iwe somo kwa wakati ujao kwa
wale ambao wanapanga ratiba kupiga hesabu kwamba timu zetu kwa sasa zimeweza
kufikia hatua ya mashindano makubwa hivyo wawe wanawapigia hesabu mpaka kwenye
hatua ya makundi na sio kwenye hatua za awali.
Licha ya kwamba viporo haviwezi kuepukika
ila inaonekana ratiba mara nyingi inaishia kwenye mechi za kimataifa za awali
na kusahau kwamba kuna uwezekano timu ikaweza kusonga hatua ya mbele na kuweza
kuendelea kuperusha bendera ya Tanzania.
Wakati ujao itapendeza ikiwa ratiba
itakuwa rafiki ili kupunguza hivi viporo kwa kuwa vinatibua mipango ya kwenye
ligi.
Itakuwa vema ikiwa kila timu ikaaza
maandalizi kwa sasa kabla ya ligi kurejea kwa kuwa huu ni mzunguko wa pili
ambao unatoa maamuzi nani atakuwa nani ndani ya ligi.
Kwa wale ambao walikuwa kwenye
mwendo mbovu kwenye mzunguko wa kwanza kwa sasa ni wakati wao kuweza kujipanga
upya ili waweze kufanya vizuri.
Inawezekana ikiwa kila mmoja
akaamua kwamba kwa sasa ni wakati wa kuendelea kupambana kwa ajili ya taifa
pamoja na timu kiujumla.
Ukiweka kando maandalizi ya Ligi
Kuu Bara pia ni muhimu kwa timu yetu ya Taifa ya Tanzania kuanza mipango upya
kwa ajili ya wakati ujao.
Tumepoteza nafasi ya kutinga hatua
ya robo fainali kwenye michuano ya Chan ambayo imemalizika nchini Cameroon.Hili
ni mbaya kwetu kwa kuwa wachezaji walituahidi kwamba wanakwenda kupambana.
Kutolewa na pointi nne ni mbaya ila
kwenye mchezo hakuna cha kubadilisha kwa sasa. Karata yetu tuliichanga vibaya
kwenye mchezo wa kwanza. Kufungwa na Zambia tena mabao 2-0 mchezo wa ufunguzi
ilikuwa ni hatua mbaya.
Dakika 90 za mwisho ambazo zilikuwa
zimeshika funguo ya ushindi nazo zilimeguka huku timu ikishindwa kupata
matokeo. Ilikuwa ni huzuni kwa Watanzania kiujumla ila kwa kuwa imetokea hakuna
namna.
Wakati ujao ni muhimu kujipanga ili
kufanya vizuri kwenye mechi za mwanzo ili kuongeza hali ya kujiamini. Kila
mmoja ni muhimu kuwa na mipango makini pamoja na utayari wa kufanya makubwa.
Mambo mengi tumeyakosa kwa sasa ila
yanapaswa kuwa funzo kwetu kiujumla na kila mmoja ambaye atakuja kuitwa ndani
ya Stars ili kupata matokeo wakati ujao.
Mashabiki furaha yao ipo kwenye
kupata ushindi ila kwa kuwa hakukuwa na ushindi basi ni ganzi ndani ya mioyo ya
mashabiki na taifa la Tanzania kiujumla.
Kushindwa kutinga hatua ya fainali
kumezima ndoto za wachezaji wengi kuweza kusonga mbele kwenye mashindano ya
kirafki na yale ya ushindani.
Ile nafasi ya wachezaji kuweza
kuingia sokoni imeyeyuka hivyo kwa sasa ni muda wa kuendelea kupambana kwa kuwa
ligi inarudi.
Muda mwingine ukifika iwe kazi ni
moja kujitoa kuanzia mchezo wa kwanza ambao huwa unakuwa umeshika furaha ya
ushindi kwenye mechi zetu.
Kupoteza mbele ya Zambia iwe funzo
kwa kuwa mechi mbili tulionekana kuzinduka ila tulikuwa tumechelewa na
wachezaji walishindwa kulinda ulinzi kutokana na tatizo la kukosa uzoefu.
Kikosi cha ushindi kianze
kuandaliwa wakati huu kwa kuwa ni muhimu kila mchezaji kujipanga na kujiweka
vema kwa ajili ya mechi zote za ushindani.
Benchi la ufundi pia linapaswa
lianze kutafuta mechi za kirafiki na kikosi chenye ushirikiano zaidi kuliko
kwenda na kikosi kipya ambacho kinakuwa na wachezaji wale ambao hawana uzoefu.
Haina maana kwamba wachezaji wapya
wasipewe nafasi hapana hapa ninamaanisha kuwa na wachezaji ambao wana uzoefu na
mechi za ushindani itaongeza nguvu kwenye ushindani.
Taifa stars sasa inachaguliwa kwa matakwa ya mawakala na sio masuala ya kiufundi.Inasemekana mawakala hao wamemteka kocha pia wa timu ya taifa . Mpango ni kuteua wachezaji wenye umri mdogo ili wauzike nje kutokana na faida ya umri wao kuwa mdogo?Ligi yetu inawachezaji wengi wazuri wazoefu kama kutakuwa na utulivu kwenye suala la uteuzi wa wachezaji na Taifa stars kamwe haiwezi kuwa nyonge.Huwezi kumchamgua mchezaji kwa kufanya vizuri ndani ya nusu msimu wa ligi. Mfano mzuri kabisa ni saido wa Yanga ndani ya timu ya taifa Burundi. Burundi walimjumuisha Saido hata kama alikuwa hana timu.
ReplyDeleteKundi la wachezaji kama akina kichuya,salum kimenya,Paul ngalema,mudathiri yahaya,Akina muzamiru,akina kabunda,Andrew vicent,keny Ally na vijana wengi wengineo. Katika kundi la wachezaji hawa utagundua si wachezaji wanaoimbwa sana na vyombo vya habari ila ni wachezaji vijana na wana uzoefu tayari na rahisi kuwanganisha pamoja kuunda timu imara. Lakini timu iliokwenda chan ilikuwa ni utani zaidi na kamwe taifa stars kwa usimamizi huu haiwezi kutoboa.