February 7, 2021

 


NAPATA wakati mgumu kuelewa namna gani timu zetu za Bongo zinakwama hasa baada ya kupanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza na kuanza kushiriki Ligi Kuu Bara, sijui wapi huwa zinakwama kwa kweli maana ni vurugu tupu.

Zama zile naikumbuka ile Mbeya City iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ambaye kwa sasa amejiweka kando kwenye masuala ya soka kutokana na matatizo ya kiafya.

Hawa walikuja kwa kasi na kuutikisa ule ufalme wa zile timu mbili pale Kariakoo Yanga na Simba. Unaambiwa ilipokuwa na mchezo wa ligi Bongo kulikuwa na ndiga nne zinatoka Mbeya zinashuka Dar.

Zote zimebeba mashabiki na ndani ya uwanja wanashangilia mwanzo mwisho ila ghafla mambo yamebadilika. Mbeya City leo haitishi tena uwanjani inanyooshwa na Biashara United ambayo imepanda hivi karibuni.

Unaweza kusema labda nataka hizi timu zitakazopanda daraja zisifungwe hapana. Kila timu lazima ionje joto ya ushindi,sare na kufungwa ni mpira ndani ya dakika 90 ila hapa nazungumzia ule mwendo wao.

Iweke kando Mbeya City itazame Singida United namna ilivyokuja kwa kasi ndani ya ligi. Yanga ilikuwa inapata tabu kushinda kwa Singida United. Ilitinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho mbele ya Yanga.

Ikiwa inafikiria kukwea pipa ndoto zao zilizimwa na Mtibwa Sugar. Haikukata tamaa ilifanya vizuri ndani ya ligi kwenye msimu wake wa kwanza. Ngoma ikawa msimu wake wa pili inarukaruka tu na ilibaki kidogo ishuke daraja.

Fungu la kukosa ikawa msimu wake 2019/20 ilikwama kuonyesha ushindani na ilishuka daraja. Ule ushindani wake wa mwanzo ile kasi yake imesahaulika na sasa huko Ligi Daraja la Kwanza haipo tena.

Imeshushwa kwa madaraja mawili na matokeo yake yote yalifutwa kwa kosa la kushindwa kutokea uwanjani kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Alliance.

Kinachonifurahisha ni kwamba Singida United ilikuwa nyumbani na mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Yanga wachezaji walicheza kwa furaha zote licha ya kufungwa mabao 3-0.

Weka kando Singida United itazame Ihefu FC ambayo imepanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza mwendo wake unaonyesha kwamba inahitaji kurudi kule ilikotoka.

Ila ngumu kuweka wazi kwamba kwa sasa inashuka kwani ni mwanzo wa mzunguko wa pili ina muda wa kujiuliza ikikwama tutakuja kuzungumza habari nyingine.

Ukiachana na Ihefu na Mbeya City ipo Namungo FC ambayo inawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Inaonekana wazi kwamba kuna timu mbili kwenye himaya moja.

Ipo ile ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho ikiwa huko inaonekana inacheza soka la maana na kupata matokeo ila ikirudi kwenye ligi inakwama kupata matokeo.

Hapo unaweza kujiuliza hivi kuna timu mbili ndani ya Namungo ama kuna mechi ambazo lazima Namungo yenyewe icheze na kuna nyingine kwao wanazichukulia kawaida?

Imepanda daraja msimu uliopita na ilikuwa moja ya timu bora ila kwa sasa inapotea taratibu, hivyo bado nafikiria nini kinazikumba timu zikipanda daraja, misingi ama uwekezaji?

Itazame ile KMC iliyoshiriki ndani ya ligi kwa msimu wa kwanza kisha itazame ya leo, inaonekana kuna jambo linawakwamisha ni lazima mipango iwe makini.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic