MSHAMBULIAJI Ditram Nchimbi ‘Duma’ wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, amefikisha mwaka mmoja bila kufunga bao ikiwa inaamanisha kwamba siku 365 na zaidi zimekatika mazima.
Yote yamekuja kwa sababu Nchimbi ni
mshambuliaji wa kati na imezoeleka kazi ya mshambuliaji ni kufunga mabao bila
ya kujali kafungaje. Kitendo cha kukaa mwaka mzima kama mshambuliaji bila
kufunga kimeshtua wengi nikiwemo mimi mwenyewe.
Japokuwa kuna muda hubadilishiwa
majukumu na kuchezeshwa pembeni, lakini hilo haliondoi jukumu lake mama kwamba
yeye ni mshambuliaji asilia na kitu pekee cha kufurahisha watu ni kufunga mabao
ndiyo maana baada ya muda huo bila kufunga watu wameibuka huku wengine
wakicheka na kubeza juu ya uwezo wa mshambuliaji huyu.
Vyovyote vile ambavyo straika huyo
atachukulia kitu muhimu zaidi ambacho anatakiwa kutambua kwamba ana mzigo wa
kufanya kwa ajili ya kuwaziba midomo hawa ambao wameibuka na kumnyooshea vidole
kwa sasa kwa kufanya kazi nzuri ikiwemo ya kufunga.
Lakini kwangu nina mtazamo tofauti
na wengi ambao wanamkejeli au kumcheka straika huyo badala yake nataka tutazame
suala hilo kama taifa kwa ujumla.
Kwa nini nasemea taifa ni kwamba
wakati ambao tunamcheka Nchimbi kutokana na rekodi hizo kutokuwa nzuri kwake je
ni nani ambaye mshambuliaji mzawa ambaye tunamtegemea hasa kwa wakati huu?
Nasema hivyo kwa sababu kila
nikitazama mastraika wetu wa hapa nyumbani simuoni hata mmoja ambaye unaweza
kusema huyu ni mkali na ambaye ana muendelezo wa kufanya vizuri kwa miaka na
miaka.
Kama utazama na kuibuka na straika
ambaye ni mkali kwa hapa nyumbani basi ni John Bocco pekee na nje ya hapo
hakuna ambaye anaweza kusimama kidete na kupambana na mastraika wengine wa nje
ambao wanasajiliwa.
Namtaja Bocco kwa sababu ndiye
mshambuliaji pekee wa hapa nchini ambaye amekaa kwenye mstari kwa zaidi ya
misimu 10 na anaifanya kazi yake japokuwa amekuwa akiandamwa na majeraha ya
mara kwa mara.
Tazama kwa misimu ya kati waliibuka
mastraika waliofanya vizuri akina Salim Aiyee na Ramadhan Kapera lakini baada
ya muda wamepotea na hawasikiki kabisa kwenye soka la hapa nyumbani.
Tunachotakiwa kutambua kwamba
tatizo siyo kumcheka Nchimbi kutofunga ila kuelewa kama taifa tumeshindwa kuwa
wazuri katika kuzalisha na kuwatunza washambuliaji wetu wazawa.
Hili tatizo ndilo ambalo linatakiwa
kushughulikiwa kwa sasa na klabu, wadau pamoja na wote ambao wanasimamia soka
letu la hapa nyumbani kuona wanaibua vipaji vipya vya washambuliaji ambao
watakuja kufanya mapinduzi katika ligi yetu.
Bila ya kukaa chini na kutafuta
majibu ya hiki ambacho kinatusumbua kama taifa tutaendelea kuwa wahesabu wa
siku kwa washambuliaji yupi kafikisha siku ngapi bila ya kufunga, kitu ambacho
siyo kizuri hata kidogo.
Wakati huu ambao tunacheka na
kumnyooshea vidole Nchimbi inatakiwa tuanze kutafuta mwarobaini wa kuwapata
washambuliaji wapya ambao watakuja kufanya kazi kwa klabu na taifa kwa siku za
mbele.








Sisi watanzania wajinga sana,wapo wengi duniani hawajafunga lakini sisi na waandishi wa habari HOPLESS iv hatujifunzi au???
ReplyDelete