LICHA ya kwamba Simba wanacheza soka la pasi nyingi ambalo wengi wanapenda kuliita pira biriani ila bado wana deni kwa Rais John Pombe Magufuli la kuleta kombe la Afrika kwenye ardhi ya Tanzania.
Magufuli ametangulia mbele za haki akiwa ameacha alama ya
kusimamia ukweli pamoja na kuona yale ambayo anahitaji yakitokea ila bado
ameacha deni kwa timu zote za Tanzania.
Agizo lake la kuona kwamba Simba ama timu nyingine inaleta Kombe
la Afrika kwenye ardhi ya Tanzania haitafutika kwa kuwa maneno yanaishi.
Ukiweka kando agizo la kuitaka Simba na timu nyingine ambazo ni
Yanga, Azam FC, Kagera Sugar, Azam FC kuleta kombe la Afrika bado alikuwa
anasisitiza kuhusu umoja.
Ile Kasumba kwa timu kutengana hasa kwenye mashindano ya
kimataifa alikuwa anachukia na hakuwahi kupenda suala hilo kabisa zama za uhai
wake.
Aliweka wazi kwamba inahitajika umoja na mshikamano katika
mashindano ya kimataifa kwa timu zote na mashabiki wote.
Magufuli alisema kuwa ikitokea Yanga itakuwa inacheza mashindano ya kimataifa ama ikitokea Simba itakuwa inacheza mashindano ya kimataifa basi ni lazima mashabiki waungane washangile timu ambayo itakuwa uwanjani.
Bado kwenye mpira ameacha alama na neno lake kwa wizara ya
michezo alikuwa anahitaji kuona timu ya Taifa ya Tanzania inapata matokeo
chanya kila wakati.
Ni aina ya maisha ambayo yalikuwa kwenye kasi kubwa lakini kila
kitu kilikuwa kinaonekana na leo inabaki kuwa historia.
Msema ukweli, mchapakazi, mpenda michezo na burudani leo
amemaliza mwendo ila ameacha maagizo ambayo yanapaswa yatimizwe kwa vitendo na
kila mmoja.
Ikiwa utahitaji kuandika ama kusema yale ambayo ameyafanya
Magufuli itakuwa ngumu kuyamaliza yote kwani kila sekta alikuwa anafanya na
kuacha alama.
Mpenda michezo, mpenda maendeleo mpenda kazi na mzalendo wa
kweli katika awamu ya tano ni alama ambayo inaishi muda wote.
Katika kipindi hiki ni muhimu kwa kila timu kujipanga na
kutimiza majukumu ambayo yanawahusu ili kuweza kufikia mafanikio ambayo ni
ndoto ya kila mmoja.
Matabaka ambayo yamekuwa yakijengwa kila siku yanaturudisha
nyuma na kutufanya tubaki pale ambapo Magufuli pamoja na viongozi wengi wapenda
maendeleo walikuwa wanayakataa.
Kwa sasa ni muda wa kufanya kwa vitendo na kuendelea kupambana
ili kuweza kuona kila kitu kinatokea. Kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia sahihi
ya kumuenzi Magufuli kwa vitendo.
Muda ambao umebaki kwa sasa ni kuendelea kutimiza kazi zetu kwa
vitendo. Hakuna ambaye anapenda kufeli hivyo ili kufaulu ni lazima kufanya kazi
kwa juhudi na kuwa na mipango makini.
Tumekuwa tukiona kwamba wapo ambao wanajitokeza kuwapa sapoti
wapinzani wa timu moja inapocheza kimataifa, tuliona wakati ule kulikuwa na
mashabiki ambao ni Watanzania walikuwa wanakwenda kuwapokea wapinzani wa Simba.
Ni zama za kuungana na kuenzi yale ambayo Magufuli alikuwa
anahitaji kuona yakitokea. Wakati wa kuwa wamoja ni sasa na zile tofauti zote
ziwekwe kando.
0 COMMENTS:
Post a Comment