TUNACHOTAKIWA kwa sasa kukifanya ni kumuombea Rais John Magufuli apumzike salama kwa kuwa mwendo ameumaliza.
Uwepo wake duniani na kuondoka kwake ni
somo kwetu pia tunapaswa kujua kwamba ni lazima nasi tufanye matendo mema ili
kuacha alama.
Kazi ambayo imebaki kwetu ni kuendeleza
yale maono ambayo alikuwa anayafikiria na kuyatendea kazi. Hakuna wa kumlaumu
kwa sasa kwa kuwa kazi ya Mola haina makosa.
Wengi wanaumia kutokana na kuondoka kwake.
Hilo ni kweli kwa kuwa alikuwa ni mtu wa watu na anapenda kufanya kazi kwa
wakati na kwa umakini.
Haivumiliki kwa namna ambavyo Watanzania
wamekuwa wakimlilia kwa huzuni ila imetokea jambo ni moja kwa sasa kumuombea
apumzike salama mwendo ameumaliza.
Kwa timu ambazo bado hazijawa na mwendo
mzuri ni muhimu kwa sasa kufanya kazi ya kurekebisha makosa ambayo wameyafanya.
Miongoni mwa vitu ambavyo alikuwa anapenda
Magufuli ni kuona matokoe mazuri kwa timu zetu zote zikiwa uwanjani kwenye
mechi zake za ushindani.
Alipokuwa akipata nafasi ya kwenda uwanjani
alikuwa anaheshimu wito ambao anapewa na kuhudhuria uwanjani na kuacha majukumu
yake kwa muda.
Utendaji kazi wake unaonekana na hauhitaji
kuanza kuuzungumzia kwa sasa kwa kuwa mengi aliyofanya yameonekana na
yataendelea kukumbukwa.
Kazi kwa timu zote pamoja na wamiliki ni
kuangalia namna ya kuenzi aliyoyaacha Magufuli kwa vitendo. Hakuna kingine cha
kufanya ambacho kitakuwa ni heshima kwake zaidi ya kufanya yote kwa umakini na
juhudi.
Ikumbukwe kuwa alikuwa anapenda kuona timu
za Tanzania zinaweza kutwaa kombe la Afrika. Ni deni kwa timu zote kuweza
kutimiza agizo hili.
Namna ambavyo Watanzania wanavyopenda
michezo ilikuwa hivyo kwake pia. Hakuishia kufuatilia Bongo pekee bali hata nje
ya nchi alikuwa anafuatilia.
Magufuli alikuwa anajua kuhusu Barcelona
ile ya Lionel Messi alikuwa anajua maumivu ya timu ya taifa ya Tanzania
kupoteza, alikuwa anajua ngumi alikuwa anajua riadha na michezo yote alikuwa
anafuatilia.
Kwa maana hiyo ni kazi kwa kila mwanafamilia ya michezo kufanya kazi yake kwa vitendo huku akijua kwamba shujaa Magufuli alikuwa anatambua na kufuatilia michezo yote.
Alikuwa anapenda muziki iwe ni Bongo Fleva,
Singeli mpaka nyimbo za dini alikuwa anafuatilia na anajua kazi za sanaa ambazo
zilikuwa zinafanywa na watu wake.
Ni deni ametuachia Watanzania kuyafanya
yote kwa vitendo ili kuweza kuendeleza maono yake ambayo alikuwa akiyafikiria
enzi za uhai wake.
Wakati huu pia ni muda wa kuangalia hesabu
kwa timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja kwa msimu huu wa 2020/21.
Kazi kubwa ambayo inabidi ifanyike ni
kuongeza juhudi na kufanya kazi kusaka pointi tatu. Mzunguko wa pili
ushindani ni mkubwa.
Zipo timu ambazo tayari zimeonyesha nia ya
kushuka daraja kwa kuwa wachezaji wameonekana kukata tamaa. Hili kwa sasa
halipaswi kupewa nafasi bali kutulia na kuanza upya kupiga hesabu.
Ushindi upo kwa timu ambayo itajiandaa na
kwa namna ligi ilivyo hakuna ambaye anamiliki ushindi hata akiwa nyumbani
anaweza kupoteza.
Tumeona wazi kwa baadhi ya mechi ambazo
zimechezwa ugenini, timu zinapata matokeo tofauti na ilivyokuwa zamani. Pia
zamani kulikuwa na ubabe mwingi kwa mechi za nyumbani.
Wakati huu imekuwa tofauti ule ujanjaujanja
hauna nafasi na kila timu inapata ushindi kutokana na maandalizi ambayo
yamefanywa kabla ya mchezo.
Inamaanisha kwamba kila timu ambayo
itafanya maandalizi mazuri kabla ya mchezo husika ina nafasi ya kushinda kwa
namna yoyote.
Basi hicho kinahitajika muda wote na
itafanya wachezaji kuanza kupata ushindi ndani ya dakika 90 ambazo watakuwa
uwanjani kuwakilisha timu zao.
Ni mzunguko ambao kila timu inapambania
malengo yake kuweza kupata ushindi. Inawezekana kwa kuwa kila mmoja anapambania
ndoto zake.
Jambo la msingi ni kuona kwamba mzunguko
huu wa pili yale makosa ambayo yalikuwa yanafanyika yanapunguzwa ama kuachwa
kabisa.
Waamuzi nao pia wana kazi ya kutimiza
majukumu yao kwa umakini. Sheria 17 za mpira zitumike katika kusimamia ushindi.
0 COMMENTS:
Post a Comment