April 4, 2021


MAJIRA ya saa 10 kamili za jioni kwa saa za Afrika Mashariki ndani ya Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam siku ya Machi 28, mwaka huu kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilikuwa na kibarua cha mwisho cha mchezo wa kufuzu michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya kikosi cha timu ya Taifa ya Libya.

Mchezo huo haukuwa na maana kubwa sana kwa Watanzania zaidi ya kusaka heshima ya kutoruhusu kupoteza mchezo katika ardhi ya nyumbani, lakini tayari hesabu zilikuwa zimekwisha tuondoa katika michuano hiyo.

 

Matumaini ya Watanzania walio wengi kuona timu yao ya taifa, ikikata tiketi kwa mara ya pili mfululizo kushiriki michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya timu za taifa yaliyeyushwa mapema tu siku ya Alhamisi ya iliyopita, Machi 25, baada ya Stars kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Equatorial Guinea.

 

Katika mchezo huo, Stars si tu walipoteza mchezo, lakini walionekana kucheza katika kiwango kisichoridhisha kwa dakika zote tisini, kiasi cha kushindwa kupiga hata shuti moja lililolenga lango kwa muda wote wa mchezo.

 

Kilichobaki kwa sasa ni kujiandaa kisaikolojia kuwatazama wachezaji wa mataifa ya wenzetu kwenye luninga, pale watakapokuwa wanauwasha moto nchini Cameroon mapema mwakani.

 

Ikumbukwe kuwa Tanzania ilisubiri kwa miaka 39, mpaka pale ulipokuja utawala wa Hayati Rais, Dk John Pombe Magufuli ili kuweza kukata tiketi ya kushiriki michuano ya AFCON ya mwaka 2019 iliyofanyika kule nchini Misri.

 

Wengi wetu tulidhani funzo hilo la kusota kwa miaka mingi kuisaka tiketi ya AFCON lilitosha kutufanya tujipange vizuri ili kuweza kupata tiketi nyingine ya AFCON lakini haijawa hivyo, na kwa mara nyingine tunaanza mahesabu upya ya kuisaka AFCON nyingine wakati ambapo nchi yetu kwa sasa ikiwa chini ya Rais Samia Suluhu.

 

Hatuna haja ya kuanza kunyoosheana vidole juu ya nani wa kulaumiwa kutokana na kile ambacho kimetokea, lakini tunapaswa kujifunza ili kuweza kuanza maandalizi na kujipanga mapema ili isije ikatokea tukapoteana kwa miaka 39 mingine.

 

Nadhani tuna vitu vingi vya kujifunza kutoka kwa wenzetu wa Taifa la Uganda, ambao kutokana na mifumo yao mizuri ya kukuza soka la vijana wameonekana kuwa tishio katika medani ya soka hasa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Mimi naamini katika maneno ya makocha wengi ambao wamewahi kupata nafasi ya kufundisha vikosi vyetu vya timu za Taifa ya kwamba, Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa vijana wenye vipaji vya soka, lakini changamoto yetu kubwa imekuwa katika mifumo ya kukuza na kulea vipaji hivi.

 

Ni wakati sasa wa Taasisi zinazosimamia soka hapa nchini, kujitafakari na kuchukua hatua.


Uchambuzi wa Edibily Lunyamila, unaupata ndani ya gazeti la michezo la Championi kila Jumatatu.

1 COMMENTS:

  1. Hakuna kitu hapo, baadhi ya vingozi wanajipigia hela tuu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic