“KWANGU kumbukumbu mbaya zaidi ni
ile ya mwaka 2003 ambapo nilikosa mkwaju wa penalti dhidi ya klabu ya Santos ya
Afrika Kusini, katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya
kwamba tulifanikiwa kuendelea mbele.
“Tulisonga mbele kwa kuwa Santos
nao walikosa penalti, lakini tukio hilo liliniacha katika hali ngumu sana kwa
kuwa nilihisi nimeifelisha timu yangu.” Anaanza kufunguka mshambuliaji wa
zamani wa kikosi cha klabu ya Simba na Taifa Stars, Madaraka Selemani ‘Mzee wa
Kiminyio’
Nyota huyo ambaye alipata
mafanikio makubwa katika soka la ndani na nje ya Tanzania kwa miaka ya kuanzia
1984 hadi 2005 kupitia Championi Ijumaa, amefunguka mambo mengi kuhusu maisha
yake ya soka kama ifuatavyo;
Historia yako kwa ufupi?
“Mimi ni mzaliwa wa mkoani Morogoro,
lakini nimekaa sana Dar es Salaam kwa kuwa wazazi wangu ambao kwa sasa ni
Marehemu walihamia miaka mingi iliyopita, hivyo makuzi yangu yalikuwa hapa Dar
es Salaam.
“Kuhusu kucheza soka, nilianza
kucheza mpira wa mtaani ambapo nilifanikiwa kucheza timu kama Sifa United,
Rupia, Tambaza ya magomeni na nyinginezo nyingi, lakini katika soka la
ushindani hasa kwa Ligi Kuu, nilianza na CDA ya Dodoma mwaka 1984 ambapo
nilikutana na nyota kama Jamhuri Kihwelo.
“Mwaka 1985 nikajiunga na kikosi
cha Majimaji ya Songea ambayo kwa wakati huo ilikuwa na wachezaji kama Justin
Simfukwe, ambapo baada ya hapo mwaka 1989 nikajiunga na klabu ya Fanja kutoka
Uarabuni.
“Mwaka 1994 nilirejea Simba
ambapo niliwakuta nyota kama Mohammed Mwameja, Malota Soma. Kutoka Simba
nilijiunga na timu inaitwa Kajimuro mwaka 2000 ambayo ni timu ya Sigara ambayo
ilibadilishwa jina, nikarejea Simba mwaka 2002 na kucheza mpaka nilipostaafu
mwaka 2005.
Kwa sasa unajishughulisha na
nini?
“Baada ya kuachana na soka kwa
sasa najishughulisha na majukumu yangu binafsi ambayo nisingependa kuyaweka
wazi, lakini nashukuru Mungu ndiyo yananiendeshea maisha.
Vipi kuhusiana na familia yako?
“Mimi ni baba wa familia ya mke
mmoja na watoto wawili ambao ni Mwanahenzi wa kike na Selemani Madaraka wa
kiume, kwa upande wa mke yeye si shabiki wa soka na hana timu.
Kusafiri kwako kama mchezaji
kuliiathiri vipi familia?
“Kwa kuwa masuala ya kusafiri ni
jambo la kawaida kwa mchezaji, nashukuru familia yangu ilikuwa inaelewa.
Utofauti wa maisha kwa sasa,
kulinganisha na wakati unacheza soka ni upi?
“Utofauti wa kuendesha maisha
unatokana na namna ambavyo mtu amejipanga wakati akiwa bado mchezaji, hilo
ndilo linaweka tofauti ya ugumu na urahisi wa maisha, lakini kwangu naona
maisha yako vilevile tu.
Kikosi gani kwako kilikuwa bora
zaidi wakati unacheza soka?
“Kikosi bora zaidi kwangu ni cha
klabu ya Simba cha mwaka 1994, na kuthibitisha hili ukiangalia kikosi cha timu
ya taifa cha mwaka 1994 ambacho kilishinda kombe la Chalenji pale Uganda,
kilikuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao walikuwa wakitoka Simba.
“Baadhi ya wachezaji wa Simba
waliokuwa kwenye kikosi hicho ni; Steven Nemes, Mwamedi Mwameja, Deo Mkuki,
George Masatu.
Ni upi utofauti wa ushindani wa
Simba na Yanga, wa zamani na sasa?
“Ushindani ulikuwepo tangu zamani
na kilichozidisha upinzani huo ni ile hali ya Simba na Yanga kutocheza mara kwa
mara kama ilivyo sasa, unaweza kukuta kwa mwaka zinacheza mara mbili pekee
tofauti na sasa ambapo hukutana mara kwa mara na kupunguza ladha.
Mafanikio gani umeyapata katika
mchezo wa soka?
“Mafanikio ni mengi kwa maana ya
mataji mbalimbali ambayo kwa kweli siwezi kukumbuka idadi yake, lakini hata
kuhusiana na mabao, unajua kwa kipindi chetu hatukuwa na utaratibu maalum ya
kukusanya na kutunza rekodi, hivyo ni vigumu kukumbuka kwa usahihi.
Ni yupi mchezaji wako bora wa
muda wote
“Binafsi nimefanikiwa kucheza na
wachezaji wengi bora katika vikosi vya timu zote ambazo nimecheza, hivyo
inakuwa vigumu kutaja mchezaji mmoja.
Umefanikiwa kucheza michezo
mingapi ya dabi ya Kariakoo?
“Kwa kipindi nilichokuwa ndani ya
kikosi cha Simba, nilifanikiwa kucheza michezo mingi dhidi ya Yanga, kwa hesabu
za haraka ni kama michezo 15.
Mchezo upi unaukumbuka zaidi
kwenye maisha yako ya soka?
“Nakumbuka michezo mingi lakini
miongoni mwa michezo bora zaidi ambao naukumbuka ni ule dhidi ya Yanga ambapo
nikiwa na kikosi cha Majimaji niliwahi kufunga hat-trick mwaka 1989.
“Nakumbuka baada ya mchezo huo
mashabiki wengi wa Simba walikuja na kunibeba katika hali ya kushangilia.
Ishu ya ushirikina kwenye michezo
ya Simba na Yanga ina ukweli?
“Ishu ya ushirikina siyo tu kwa
Simba na Yanga, mimi naweza kisema klabu nyingi zinaamini katika ushirikina,
kuanzia wakati wetu na hata sasa.
“Kwa upande wangu ni ndani ya
kikosi cha CDA ya Dodoma na Kajimuro, ndizo timu pekee ambazo sikuwahi kuona
mambo hayo.
Unadhani hizo imani husaidia?
“Kwa kuwa ile ni imani,
inategemea na yule ambaye anaamini lakini mimi licha ya kuhusishwa katika
mazingira ya kitimu, lakini huwa siziamini na imewahi kutokea mara nyingi mnaahidiwa
ushindi na hao wataalamu lakini mnaingia uwanjani na kupoteza mchezo, japo
nisingependa kuweka wazi michezo husika.
Unadhani TFF inakutumia ipasavyo
kuendeleza soka?
“Wachezaji wa zamani tuko hivyo
hatuwezi wote kutumiwa na Shirikisho, wapo wenzetu wanaotuwakilisha.
Umewahi kufikiria kujihusisha na
ukocha?
“Unajua si wachezaji wote wa soka
wanalazika kuwa makocha, wengine wanaweza kujihusisha na shughuli nyingine za
kujenga taifa.
Unaendelea na ratiba ya mazoezi
kwa sasa?
“Ndiyo huwa nimekuwa na kawaida
ya kufanya mazoezi kila wikiendi, na mara chache siku za wiki ambako huko huwa
tunacheza michezo mbalimbali ya Maveterani ambapo kwa upande wangu huzichezea
timu za Mbweni Veterani na ile ya Simba Veterani.
Siri ya mafanikio ya Simba ya
mwaka 2003 iliyowavua ubingwa Zamalek ni ipi?
“Siri kubwa ilikuwa ni umoja wa
wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa ujumla, nakumbuka kuelekea mchezo
huo tuliweka kambi nchini Oman, huku pia iliongezwa nguvu ya Talib Hillary
ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba ambaye alilisaidia benchi la ufundi
kwenye mbinu za kupata matokeo na kwa kufuata mashauri yake tulifanikiwa.
Mchezaji gani wa kimataifa
anakuvutia kwa sasa?
“Wapo wengi kama vile; Clatous
Chama, Prince Dube, Chris Mugalu, Mukoko Tonombe na wengine ambao ni vigumu
kuwataja wote.
Kuna kitu unajilaumu ambacho
hukukifanya wakati unacheza soka?
“Hapana, mimi naamini kila kitu
kina wakati wake sisi tulikuwa na wakati wetu na huwezi kusema kuna kitu cha
ziada unachoweza kukifanya tena.
Una ushauri gani kwa wachezaji wa
sasa?
“Jambo la muhimu ni kuwa,
wanapaswa kujifunza kutokana na mapungufu ya wale waliowatangulia na
kuhakikisha hawarudii makosa.
Umewahi kuhusika katika matukio
ya kuuza mechi za Simba na Yanga?
“Niliwahi kushawishiwa kutoka
Simba kwenda Yanga wakati wa mfadhili wa Yanga Marehemu, Abbas Gulamali, ambapo
nilifikia hatua ya kukutana na Abbas mwenyewe na kumalizana kila kitu.
“Lakini kabla hatujakamilisha
usajili nilibadilisha maamuzi kutokana na ishu ya masilahi na Simba kupanda
dau.
Unalizungumziaje suala la
mabadiliko kwenye klabu za Simba na Yanga?
“Jambo la muhimu ni kwamba
mabadiliko ya mfumo ni jambo la lazima kwa kuwa mpira wa sasa ni biashara na
unahitaji fedha nyingi kwa ajili ya uwekezaji ambazo ni ngumu kuzitoa kwa
wanachama.
“Hivyo wanahitaji watu wenye nia
ya uwekezaji kwa ajili ya kuweka fedha, zitakazosaidia kupata wachezaji wazuri
na kuweza kuwahudumia.
Tukio gani huwezi kulisahau
kwenye maisha yako?
“Miongoni mwa matukio ambayo
siwezi kuyasahau kwenye maisha yangu ni lile la kupinduka na gali mwaka 1986,
nikiwa na kikosi cha Majimaji wakati tunatoka Songea na kurejea Dar es Salaam.
“Nashukuru Mungu kwa kuwa licha
ya ubaya wa tukio lenyewe, lakini hakuna aliyepata majeraha.
Unadhani ni sababu gani
inapelekea washambuliaji wa kigeni kuwatawala wazawa?
“Unajua hapo sababu kubwa ni ishu
ya muunganiko wa kitimu, na kwa kuwa mara nyingi klabu za Simba na Yanga ambazo
huwa na muunganiko mzuri wa kitimu huleta nyota wa kigeni ambao ni bora, hali
hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa.
“Lakini naamini Bocco akipewa
nafasi katika michezo iliyosalia, na kwa kasi yake ya sasa anaweza kuibuka
mfungaji bora kutokana na ubora wa kikosi chao, licha ya kwamba Dube anaongoza.
0 COMMENTS:
Post a Comment