IMEELEZWA kuwa ikiwa usajili wa nyota wa kikosi cha Ruvu Shooting Edward Manyama ukikamilika basi itakuwa ni vita mpya ya namba ndani ya kikosi hicho.
Imekuwa ikielezwa kuwa Manyama ambaye ni beki wa kushoto wa Ruvu Shooting ambaye pia aliwahi kucheza timu ya Namungo FC yupo kwenye rada za Simba.
Tetesi hizo zimekwenda mbali na kubainisha kwamba tayari nyota huyo amesaini dili la miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo.
Kwa sasa nafasi hiyo ndani ya Simba yupo nahodha msaidizi Mohamed Hussein ambaye yupo pia kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, mshindani wake ni Gadiel Michael na wakati mwingine Erasto Nyoni naye amekuwa akipewa jukumu hilo.
Gadiel ambaye yeye alijiunga na Simba akitokea Yanga naye amekuwa akipata changamoto kubwa kutoka kwa Mohamed ambaye ameongeza dili la miaka miwili hivi karibuni.
Ikiwa Manyama atajiunga na Simba basi kazi kubwa itakuwa kwenye utatu huo unaonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes kuweza kupambania namba kikosi cha kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ruvu Shooting zimeeleza kuwa beki huyo mkataba wake upo ukingoni hivyo anaweza kujiunga na timu yoyote ambayo itaweka dau nono.
Manyama alikuwa kwenye rada za Yanga msimu uliopita ambapo dili lake baada ya kubuma akaibukia ndani ya Ruvu Shooting akitokea ndani ya Namungo FC.
0 COMMENTS:
Post a Comment