June 10, 2021


Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limefanya mawasiliano na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusiana na uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Agosti 7 mjini Tanga.

Imeelezwa, TFF imeishitakia Fifa kuhusiana na baadhi ya wabunge kuishawishi Serikali kuingilia uchaguzi huo ambao uko katika hatua za awali kabisa.

Taarifa za ndani kutoka katika shirikisho hilo, zimeeleza kumekuwa na mawasiliano kati ya TFF na Fifa kuhusiana na uchaguzi huo, hata hivyo haikuelezwa awali TFF wameieleza nini Fifa.

Mara nyingi, Fifa wamekuwa wakitoa adhabu ya kuzifungia nchi ambazo Serikali zake zimekuwa zikiingilia uchaguzi wa mashirikisho, hali ambayo baadhi ya wadau wameieleza kuwa kama ni tatizo kama wabunge wataendelea kuitaka Serikali iingilie uchaguzi huo.

Juhudi za kuwapata viongozi wa TFF jana zilishindikana kutaka kujua nini hasa ambacho TFF wamekuwa wakiwasiliana na Fifa kuhusiana na uchaguzi huo ambao umepamba moto.

Juzi na jana, baadhi ya waliotaka kugombea akiwemo Mbunge wa Mwelra, Zahoro Mohamed Haji walilalamika kushindwa kupata ruhusa ya kugombea kutoka kwa wanachama wa shirikisho hilo.

 Kila mgombea hutakiwa kupata kura angalau tano kutoka kwa wanachama zaidi ya 40 wa shirkisho hilo.

Imeonekana Rais wa TFF, Wallace Karia na mgombea mwingine aitwaye, Evance Mguesa ndio waliofanikiwa kupata kuaminiwa na wanachama hao, jambo ambalo limelalamikiwa na wagombea hao huku wengine wakilalamika kuitaka Serikali iingilie uchaguzi huo wa TFF.


Leo asubuhi juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao zilifanikiwa na akasema wamekuwa na mawasiliano na Fifa si kwa ajili ya kushitaki na badala yake ni utaratibu wa kawaida.

“Ni utaratibu wa kawaida kabisa kuwasiliana na Fifa kwa ajili ya kuwaeleza mchakato wa uchaguzi unakwenda vipi. Tunawaeleza mambo yote, kwamba kuna malalamiko, jambo ni hili na kadhalika,” alisema Kidao.

Kidao alisema wao hawana sababu ya kuichongea Serikali kwa kuwa wanaporipoti Fifa lazima wafanye hivyo kwa Serikali pia kwa kuwa inapaswa kujua mchakato wa uchaguzi unaendeleaje pia.


“Serikalini pia tunaripoti kama tunavyofanya kwa Fifa, lazima Serikali ijue nini kinaendelea na uchaguzi umefikia wapi. Huu ni wajibu wetu kufanya hivi kwa Serikali na Fifa.”


1 COMMENTS:

  1. Kama ni kweli TFF wamefikisha taarifa hizo FIFA basi watakuwa ni majuha,wabunge walikuwa wanachangia maoni yao kwenye mjadala wa kupitisha makadirio ya bajeti ya wizara inayohusika na michezo na wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu mwenendo wa soka la nchi yao wakiwa kama wapenzi wa soka,pia kulikuwa na utani na vijembe kati ya wabunge mashabiki wa Simba na wale wa Yanga sasa sijui kama huko ni kuiambia serikali iingilie mchakato wa uchaguzi.
    Wameshasahau jinsi serikali ilivyoingilia mchakato wa uchaguzi uliopita ambao uliwaweka madarakani hao wanaotuma hizo taarifa(kama ni kweli...) hadi kutumika mbinu chafu za kuwabambikia kesi akina Jamal na Wambura ili mradi wasigombee ili akina fulani wapite kiurahisi japokuwa walikuwa hawatakiwi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic