June 25, 2021


 MIONGONI mwa washambuliaji wanaotajwa kuwaniwa na vigogo wa soka Bongo ni Kibu Denis ambaye anakipiga katika kikosi cha Mbeya City.

 

Kibu ana mabao matano msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara akiwafunga Ihefu FC, Polisi Tanzania, Gwambina na JKT Tanzania akifunga mawili.Pia ana asisti mbili ambazo zote alizitoa dhidi ya JKT Tanzania, mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.


Kumbuka hivi karibuni aliitwa kwa mara ya kwanza kuitumikia Taifa Stars inayonolewa na Kim Poulsen, ambapo alicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi, iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Katika mchezo huo uliochezwa Juni 13, mwaka huu, Kibu alianzia benchi, lakini kuingia kwake kipindi cha pili, akahusika kwenye mabao yote mawili kwenye ushindi wa 2-0.


Kibu alitoa asisti kwa John Bocco aliyefunga bao la kwanza, kabla ya kufanyiwa faulo nje kidogo ya eneo la hatari, ambapo Israel Mwenda akaenda kupiga mkwaju wa moja kwa moja na kuandika bao la pili.


Jina lake linatajwa kuibukia ndani ya Yanga kuelekea usajili wa msimu ujao jambo ambalo limekuwa gumzo ambapo hapa Spoti Xtra limefanya naye mahojiano.

 

HISTORIA YAKO KWENYE SOKA IPOJE?

“Nimeanzia Ngara mkoani Kagera, ambapo nilikuwa naitumikia Kumuyange FC.


“Hii timu nilianza nayo kuichezea Ligi ya Kata na nilikuwa miongoni mwa wale walioipandisha mpaka Ligi Daraja la Pili.


Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2018, timu ya Geita Gold wakaniona na kupendezwa na kiwango changu.


“2019 nilikuwa ndani ya Geita Gold kwa mkataba wa miaka miwili ambapo tulikuwa Ligi Daraja la Kwanza. Katika msimu huo tuliweza kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza, tukapata nafasi ya kucheza Play Off ya kupanda Ligi Kuu Bara.

 

“Mchezo wetu wa Play Off tulikutana na Mbeya City, hapo ndipo wagonga nyundo hao wa Mbeya waliponiona.


“Kwa sababu nilikuwa na mkataba na Geita Gold, wakakubali kuvunja, nikajiunga nao na sasa nipo ndani ya Mbeya City.


KUCHEZA TAIFA STARS KWA MARA YA KWANZA KWAKO ILIKUWAJE?

“Ninamshukuru sana Mungu kwa kupata nafasi ile, kwangu ilikuwa ni furaha sana. Nilitamani sana japo nipate hata dakika tano niweze kuwathibitishia Watanzania uwezo wangu.


“Kweli nafasi niliipata na nilicheza kwa maelekezo kutoka kwa mwalimu Kim Poulsen, nikajiamini. Mungu mkubwa, tukaibuka na ushindi.

 

MALENGO YAKO YAPOJE?

“Malengo yangu msimu ujao ni kuzidi kupiga hatua mbele ya safari yangu maana ndiyo kwanza kumekucha.

 

KIPI KINAKUBEBA?

“Nidhamu katika kazi na ushirikiano ambao tunaufanya, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kufikia malengo yetu.

 

NAFASI YA MBEYA CITY KUBAKI LIGI KUU IPOJE?

“Tuna nafasi ya kubaki kwenye ligi kwa asilimia 65, bado tupo sehemu salama, lakini lazima tushinde mechi zote zilizobaki au mbili kati ya hizo.

 

UNATAJWA KUIBUKIA YANGA, DILI LIMEFIKIA WAPI?


 Hilo kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kuwa wao wanalizungumzia ila mimi sijui lipoje,” anamalizia Kibu ambaye kichwani ana rasta za kimtindo.

2 COMMENTS:

  1. Yanga Kama kweli wanataka sign ya huyo jamaa hawajitambui usajiri ghani was kukurupuka wakifanya hivyo wasishangae Simba kuchukua kombe back to back 10 times

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic