VIVIER Bahati, Kocha Msaidizi wa kikosi cha Azam FC amebainisha kwamba jambo lao ambalo walitarajia kulifanya kwa msimu wa 2020/21 halijatimia hata kidogo.
Mwanzo wa msimu huu Azam FC ilibainisha kwamba ina jambo lake ambalo inahitaji kutimiza na iliweka wazi kwamba ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho.
Jambo hilo limekuwa gumu kwa sababu ubingwa wa Kombe la Shirikisho uliyeyukia mikononi mwa Simba baada ya kupoteza kwa kufungwa hatua ya nusu fainali bao 1-0 Uwanja wa Majimaji, Songea.
Jambo la pili la kusepa na ubingwa limebuma kwa kuwa ni Simba walifanikiwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa 2020/21 huku Azam FC ikiambulia nafasi ya tatu kwenye ligi.
Akizungumza na Saleh Jembe, Bahati amesema kuwa hakuna jambo ambalo limeweza kutimia kwa sasa katika yale ambayo waliyapanga hivyo watatumia makosa kuyafanyia kazi.
“Huwezi kusema kwamba jambo letu limekamilika hapana, tunaona kwamba tumekosa ubingwa wa ligi pamoja na Kombe la Shirikisho haya yalikuwa ni malengo yetu katika kutimiza jambo letu.
“Licha ya kwamba imeshindikana haina maana kwamba hatujaonyesha juhudi hapana kila kitu tumefanya kwa juhudi ila mwisho wa siku ni matokeo ambayo yametokea uwanjani, imani yetu ni kuona kwamba wakati ujao tunafanya vizuri,” amesema Bahati.
0 COMMENTS:
Post a Comment