LIGI Kuu Bara kwa msimu wa 2021/22 inazidi kushika kasi, ambapo Jumamosi michezo mitatu ya mzunguko wa pili ilichezwa kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini, hii ni baada ya michezo miwili ambayo ilipigwa Ijumaa.
Pazia la ligi kuu lilifunguliwa rasmi Septemba 25, mwaka huu ambapo ‘majayanti’ wa soka Tanzania, Simba na Yanga walikutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao uliisha kwa Simba kufungwa bao 1-0 huku baadhi ya nyota hususani wa Yanga wakionekana kuanza kwa kasi akiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alisababisha kadi nyekundu ya Taddeo Lwanga.
Championi Jumamosi, linakuletea baadhi ya dondoo muhimu za kiungo huyo fundi wa Yanga kama ifuatavyo;
UBORA WA KUPIGA PASI
Fei Toto katika michezo mitatu mfululizo iliyopita aliyoichezea Yanga katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam amefanikiwa kuonyesha uwezo mzuri wa kupiga pasi akiwa na wastani wa zaidi ya asilimia 80 wa pasi zake kufika kwa walengwa.
Kwenye mchezo dhidi ya Zanaco alipiga pasi 36 na kupoteza pasi tano pekee, kwenye mchezo dhidi ya Rivers United alipiga pasi 32 na kupoteza sita huku dhidi ya Simba akipiga pasi 47 na kupoteza pasi tano tu.
KUPIGA MASHUTI YA MBALI
Miongoni mwa sifa kubwa za Feisal akiwa uwanjani ni uwezo mkubwa wa kupiga mashuti hatari ya mbali ambayo wakati mwingine huishia kuwa mabao.
Kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba alipiga mashuti mawili ambapo moja lililenga lango, na kuokolewa na Aishi Manula huku moja likitoka nje.
UTATU WA AUCHO, BANGALA NA MFUMO
Mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba uliochezwa Septemba 25, mwaka huu ni miongoni mwa michezo iliyoleta taswira mpya kabisa ya ubora wa Fei Toto, hususani baada ya faida ya kupunguziwa majukumu ya kukaba ambayo yanafanywa na mapacha wake Khalid Aucho na Yannick Bangala.
Lakini pia hata mifumo ya 4-1-4-1 na 4-4-2 ambayo imekuwa ikitumiwa na kocha Nabi, umekuwa na matokeo mazuri kwake kutokana na idadi kubwa ya watu wanaocheza eneo la kati na kumruhusu kupiga pasi nyingi.
Katika mchezo dhidi ya Simba, Fei Toto alikuwa bora kwenye kutengeneza nafasi za kufunga na kutawala eneo la kiungo, ambapo alipiga pasi 47 na kupoteza pasi tano tu.
TAKWIMU ZAKE
Msimu uliopita akiwa na Yanga, Feisal alifanikiwa kuifungia timu hiyo mabao manne katika mashindano ya Ligi Kuu Bara pekee, na takwimu hizi kwa kiasi kikubwa alizipata baada ya kuwasili kwa kocha Nasreddine Nabi ambaye alianza kumpanga Feisal kama namba 10 kutoka kucheza kama kiungo wa chini.
Kwa msimu huu, Fei Toto amefunga bao moja mbele ya Kagera Sugar na ametoa asisti moja katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zanaco uliochezwa Siku ya Mwananchi Agosti 29, mwaka huu.
MAKOCHA WANASEMAJE KUMUHUSU?
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike akimzungumzia Fei Toto aliwahi kusema: “Feisal anapambana sana, ni mchezaji anayejituma na anajua nini anapaswa kufanya akiwa uwanjani, kama ingekuwa Ulaya basi naamini angeweza kucheza Barcelona.
“Hii ndiyo sababu kubwa ambayo imekuwa ikinifanya nimuite kila wakati kwenye kikosi changu licha ya baadhi ya watu kuhoji, naamini kama ataendelea hivi atakuwa mchezaji wa kutumainiwa na taifa.”
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United alisema: “Saido anacheza nafasi moja na Feisal, kwangu kama kocha kumuanzisha Feisal ni bora zaidi hususani linapokuja suala la uvumilivu wa dakika nyingi uwanjani, licha ya ukubwa na uzoefu wa Saido.”
Bila ushabiki Fei anazidi kua mtamu Kama akizingatia maelekezo ya walimu atafika mbali
ReplyDelete