IMEELEZWA kuwa maisha ya Kocha Mkuu wa Barcelona, Ronald Koeman kwa sasa yanakaribia kufika ukingoni kwa kuwa ni suala la muda tu kwake kutimuliwa ndani ya kikosi hicho kinachoshiriki La Liga.
Mwendo wa Barcelona katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ni wa vichapo tu kwa kuwa wamepoteza mechi zote mbili ambapo wanashika mkia kwenye kundi E wakiwa bila pointi na vinara ni Bayern Munich wenye pointi sita.
Kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Benfica iliyo nafasi ya pili kwenye kundi katika mchezo uliochezwa Septemba 29 huku mabao yakipachikwa na Darwin Nunez dakika ya 3 na 79 kwa penalti na lile la tatu lilipachikwa na Rafa Silva dakika ya 69 huku nyota wa Barcelona Eric Garcia akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 87 kimetibua mambo ndani ya Barcelona.
Mpaka sasa hata Koeman mwenyewe hajui hatma yake na anaamini kwamba atatimuliwa muda wowote kuanzia sasa na kesho ana mtihani mwingine mbele ya Atletico Madrid katika mchezo wa La Liga unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Wanda Metropolitan.
Licha ya kuwa kwenye La Liga hajapoteza mchezo bado yupo nafasi ya sita na Barcelona ina pointi 12 huku vinara wakiwa ni Real Madrid wenye pointi 17.
0 COMMENTS:
Post a Comment