Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic,
juzi alimpanga kwa mara ya kwanza kipa wake mpya, Yaw Berko ambaye aliibuka
kivutio kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM.
Katika mchezo huo ambao mashabiki
walikuwa wakimshangilia kipa huyo kwa nguvu kubwa dakika zote alizokuwa
uwanjani, Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutinga robo
fainali.
Kipa huyo aliweza kuchukua nafasi ya Ivo
Mapunda ambaye amekuwa akicheza kwenye michezo mingi ya timu hiyo, lakini
aliweza kuonyesha kiwango cha juu kwa kuokoa michomo mikali.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa
Amani mjini Unguja, ulihudhuriwa na mashabiki wengi ambao walikuwa
wakishangilia muda wote.
Simba iliweza kuutawala mchezo huo na
kujipatia bao la mapema lililofungwa na Amri Kiemba katika dakika ya nne ya
mchezo.
Hata hivyo, Loga alifanya jambo ambalo
lilishangiliwa, ni baada ya kuwaanzisha wachezaji watatu Wazanzibar katika
mchezo huo, jambo ambalo alisema ni kwa kuwa wana uzoefu na timu za huko.
Aliwaanzisha Abdulhalim Humud, Ali Badru
na Adeyum Saleh ambao wote ni wazaliwa wa Zanzibar.
Kwa matokeo hayo Simba sasa inatarajiwa
kuingia uwanjani leo kuvaana na Chuoni ya Zanzibar katika mchezo wa robo
fainali.
0 COMMENTS:
Post a Comment