March 13, 2013



Na Saleh Ally
HAKUNA ubishi hata iwe vipi, kiungo mshambuliaji mwenye kasi wa Simba, Mrisho Ngassa, hawezi kubaki katika kikosi hicho msimu ujao.
Mkataba wake na Simba umekwisha, taarifa za kuwepo mwingine zimeshakanushwa, lakini hata mabosi waliohakikisha anajiunga na klabu hiyo, Zacharia Hans Pope na Geofrey Nyange Kaburu wameshaachia ngazi.

Ingewezekana hata baada ya kuondoka mabosi hao, huenda angetamani kuendelea kubaki na kuitumikia Simba, lakini mazingira kwake yanaonekana kuwa magumu sana.
Swali la kwanza la kujiuliza ni kuhusiana na hisia za wadau wengi wa Simba, kwamba Ngassa hachezi vizuri, lakini amekuwa akijitahidi kufunga.

Tayari kuna hisia kuwa ana mapenzi na Yanga, basi hawezi kucheza vizuri, lakini wengi wanaosema hayo hakuna anayekuwa wazi na kueleza mambo kwa takwimu kwamba kiasi gani alishindwa kuisaidia timu.
Ninaamini lazima msimu ujao Ngassa atakwenda Yanga, maana hana ujanja hata kama alikuwa hataki kucheza huko. Timu kubwa tatu Tanzania, mbili tayari hawezi kucheza.
Azam FC ana matatizo nao, Simba alikoamua kwenda wanaamini anawahujumu. Atakwenda wapi? Jibu ni lahisi kabisa.
Kukaa benchi:
Kuna mechi muhimu, Ngassa amekuwa akiwekwa benchi bila ya maelezo ya kutosha. Simba wameshindwa kuwa wazi kwamba ni sababu zipi zinafanya Ngassa awekwe benchi na badala yake vijana ndiyo wanaocheza.

Vijana ni suala zuri, lakini kwa kuwa Ngassa alisajiliwa na Simba basi ni lazima aitumikie kwa kuwa uwezo wake ni msaada mkubwa. Kama kungekuwa na tatizo, basi hapana shaka lilikuwa linawezekana kumalizwa kwa mazungumzo naye akacheza soka na kutoa mchango wake.

Mfano, Simba iliondoka nchini kwenda Angola ikiwa imefungwa bao 1-0 na Libolo, lazima ilihitaji mchezaji mwenye kasi na presha kubwa kwa wapinzani wao waliokuwa ugenini. Lakini akawekwa benchi na kuingizwa dakika 18 za mwisho!


Kurudishwa benchi:
Mwanzoni kabisa mwa mzunguko wa pili, ilikuwa ni mechi dhidi ya Ruvu JKT. Simba ilikuwa imetawala mchezo huku Ngassa akiwa tishio kwa mabeki wa timu hiyo ya jeshi.
Simba ikaenda mapumziko ikiwa na bao moja, waliporejea kipindi cha pili, Ngassa aliwekwa benchi, pia Kocha Mkuu, Patrick Liewig, hakuwa na maelezo ya kutosha baada ya mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Maana JKT walibadilika na kuanza kushambulia mfululizo kwa kuwa hawakuwa na presha tena ya Ngassa, hivyo wakacheza kwa utulivu na kuwa tatizo kwa Simba.

Watu wa karibu:
Kuna wadau walio karibu na timu hiyo wamekuwa msaada sana, lakini inawezekana hisia zao kupata nafasi kubwa kuliko zile za kitaalamu kunaweza kukawa tatizo pia. Wako wanaoamini Ngassa anaihujumu, lakini bado hawana uthibitisho wa kutosha kwani mambo mengi yanakwenda kwa hisia.

Mapenzi na Yanga:
Ngassa ameonyesha wazi ana mapenzi na Yanga, siku chache baada ya kuvaa jezi ya timu hiyo ya njano na kijani na kusababisha mgogoro mkubwa na Azam FC, viongozi wa Simba wakaingia katika mchakato wa kumsajili.

Nini ambacho kilikuwa hakijulikani kuhusiana na mapenzi yake hayo?  Vipi walikubali kumchukua ajiunge na timu yao? Hata walipoulizwa na waandishi, walisema wanaamini kazi ni kitu muhimu kuliko mapenzi, na Ngassa angejali zaidi kazi.

Cristiano Ronaldo anaipenda Manchester United, hiyo si siri hata kidogo. Lakini Madrid hawajawahi kuacha kumuamini kwa kuwa wanajua tofauti ya kazi na mapenzi. Usiseme hapa ni Tanzania na huko ni Ulaya, kuamini hakuna nchi wala bara. Hata Ngassa angeaminiwa, bado angeweza kufanya kazi yake vizuri kuliko hisia za mapenzi yake na Yanga kuwa fimbo ya kumuua. Angeweza kuachwa aipende Yanga halafu afanye kazi yake Simba.

Sasa kipi tena kiliwafanya waanze kutomuamini na kumuona ni tatizo?  Kama wangemuamini na kumueleza wazi hakika angefanya kazi yake katika kipindi ambacho ana mkataba nao.

Ugonjwa:
Ngassa si mchezaji wa kwanza kucheza Simba akaonekana ana mapenzi na Yanga. Kumbuka Edibly Lunyamila, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, lakini wako kama akina Hamis Gaga, Method Mogella ‘Fundi’, Said Mwamba ‘Kizota’na wengine wengi walitoka huku, kwenda upande wa pili na wakacheza vizuri kwa kuwa waliaminiwa.

Ugonjwa ulioanza Simba wa kutaka mapenzi kuliko uwezo au utumishi bora, unaweza kuendelea kuitafuna. Maana baada ya Ngassa, mwingine tena atashikwa ‘uchawi’ wa Uyanga na mwisho watamnyima raha, naye ataondoka zake.



3 COMMENTS:

  1. Mkuu..
    Nimekuwa msomaji wa blog yako kwa muda sasa...

    lakini kwanza,nadeclare interest,mimi ni shabiki mkubwa wa Simba SC kwa tanzania,Liverpool FC na FC Barcelona....

    kimsingi sifurahishwi hata kidogo na uandishi wako uliojaa unazi(ushabiki wa waziwazi)na mapenzi kwa timu fulani...

    Hata kama simba ina matatizo,unapaswa kuyaandika kwa kufuata ethics za kazi yako ya uandishi(sina taaluma hii,lakini kwa jinsi unvyoandika,haihitaji hata elimu ya darasa la saba kujua umeegemea upande gani,unless uweke wazi tu,kwamba blog yako sio kwa ajili ya habari za michezo ,bt kwa ajili ya timu uipendayo...

    Vilevile nikukumbushe tu kwamba,waandishi wengi sana wa habari wana mapenzi yao kwa timu flani,ila kwa kuwa wanaielewa taaluma yao vizuri,wanajaribu kuheshimu taaluma zao...

    Sikulazimishi kuandika ninavyotaka mimi,nakukumbusha tu kuandika bila unazi ili kujijengea heshima kama wenzio,mfano Shaffihdauda,binzubeiry(huyu ana mapenzi na timu yake flani,lakini anaandika kama taaluma yake inavyotaka)na wengineo...

    Nilitamani sana kukuandikia maelezo haya kwa e mail yako,bahati mbaya nimeikosa lakini naamini ujumbe utakufikia mkuu....

    Mr.Mnanka D.Joseph
    Ardhi University
    Dar es salaam,TANZANIA.

    mnanka88@gmail.com

    ReplyDelete
  2. nashukuru sana kwa maoni ndugu mnanka, nafurahi kuona wewe msomi wa chuo kikuu kama ulivyojitambulisha, ila umenisikitisha sana na kunilazimu niingie hofu kidogo na wewe.

    ingawa si wasomi tu, lakini wewe ulipaswa kuchambua mambo kwa hoja na si kuyapeleka kama wauza kahawa wa kariakoo, naamini kabisa kusomea masuala ya ardhi hata ungekuwa na phd, bado utakuwa mgeni kwenye ethics za media, inawezekana bado uko kwenye kundi la wanaoamini kuwa na elimu ya chuo kikuu hata kama taaluma yako ni ujenzi, basi utakuwa unajua kila kitu (jiondoe huko).
    nikirudi kwenye suala la msingi, nafikiri vizuri ukaeleza mambo kwa details, kwamba wewe ni mnazi, sababu ni hii na ile.
    naona hii makala inaelezea kuhusu simba, sasa ulitaka lazima tuchanganye na kitu kingine au jina la timu nyingine? au pointi yako msingi nini mheshimiwa.
    wala huna haja ya kuficha, hata kama utakuwa umeagizwa kutoa maoni, kama ni yako, mimi sijali, usiweke kwenye email yangu...ntakupa siku nyingine, mwagika tu hapa tuende hoja kwa hoja, siku ya mwisho mambo yatakaa sawa.

    ReplyDelete
  3. Salehe binafsi sijaona hoja ya ndugu Mnanka D.Joseph....yeye alitakiwa kuja na hoja kuku challenge wewe badala yake anakuja na ushabiki wa Simba, Binafsi namuona bwana Mnanka D.Joseph ni mshabiki na sio mpenzi wa soka...Good job Saleh..

    Timothy

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic