SOKA ina nguvu kuliko hata taasisi kubwa duniani, ndicho
kinachoonekana kuendelea hapa nyumbani. Wakati uchaguzi wa Shirikisho la soka
Tanzania (TFF) ulipoanza kupitia michakato yake, mambo yakawa hovyo tokea
wakati huo.
Nasema hovyo kwa kuwa nimewahi kuelezea namna ambavyo ukabila
na udini ulivyoingia katika uchaguzi huo, kwamba kuna watu wamekuwa wakifanya
kampeni zao kwa kutumia mambo hayo mawili.
Kwa wanaokumbuka nilikemea na kuelezea athari zake, lakini
nilieleza uchaguzi uliomungiza Tenga madarakani nilivyoufuatilia kwa karibu
namna udini na ukabila ulivyokuwa tatizo na athari zake.
Wiki iliyopita, nikachambua namna waandishi
tunavyojidhalilisha kupita kiasi kuhusiana na suala la kuchambua mambo
yaliyojitokeza kisheria. Hata kama hatujui lakini tumekuwa tukilazimisha tu kwa
kuwa tunaamini ukiwa mwandishi basi unajua kila kitu.
Nikashauri ni lazima tujifunze, tukubali kuuliza na kupata
mambo ambayo ni muhimu ili kujaziliza uchambuzi weyu. Pia niliwaasa watangazaji
wa redio ambao hawana taaluma ya uandishi lakini wanajiita waandishi na
kuchambua ili mradi tu kwenye vituo vya redio ili kuwaridhisha watu fulani.
Lakini leo kuna kitu kingine kimekuwa kinaendelea kujitokeza
kwa kasi, kitu hiki sidhani pia kama kipo sahihi na ninaona ni sehemu kubwa ya
vyombo sasa imeingia uko.
Mwandishi wa michezo unapokutana na wadau mbalimbali wa
vyombo vya habari wanataka kujua wewe uko upande gani, eti wewe ni wa Malinzi
au Nyamlani. Au inawezekana mtu ukakutana naye na moja kwa moja akaeleza kuwa
wewe uko upande fulani.
Juzi nilikutana na rafiki yangu, mdau mkubwa tu wa mchezo wa
soka na anashiriki vizuri kwa ukaribu kabisa na mchezo huo nchini.
Alichonieleza eti mimi ni wa Nyamlani, tena akasisitiza watu wote wanasema
hivyo.
Sikuona sana kama nina sababu ya kujitetea, huenda ningeweza
kuwa na chaguo lakini sina sababu ya kufanya hivyo kutokana na mambo mawili
makubwa.
Kwanza hata nikimtaka mtu sina uwezo wa kumpigia kura
ashinde, lakini pili na muhimu zaidi nataka kuendelea kuwa mwandishi makini
ikiwezekana zaidi ya hapa, najua sijafikia kuwa makini kuliko wengine wote
duniani.
Hivyo siwezi kuwa na makundi, sitaki kuendekeza ushabiki na
ndiyo maana siwezi kuwa mpambe wa Malinzi au Nyamlani. Nashukuru Mungu, pamoja
na kufahamiana na kuheshimiana na watu hao hao wawili, hakuna hata mmoja
amewahi kunifuata tokea kuanza kwa uchaguzi na kuniomba niwe mpambe wake kama
ilivyo kwa wengine.
Labda nimewasaliti? Kwa kuwa ni watu tunaoheshimiana sana,
nawaheshimu kama kaka zangu. Hawajawahi kunivunjia heshima hata siku moja na
wala sioni shida mmoja wao kama atakuwa Rais we TFF kwa mujibu wa sheria.
Lakini kamwe siwezi kuwa mpambe wao, wako ambao wamekuwa
wakieneza majungu wakiwemo waandishi ili kujijengea mazingira mazuri ya kuwa
wapambe bora karibu ya Nyamlani au Malinzi. Sina nafasi na muda hauniruhusu
kufanya hivyo.
Naweza kumsaidia Nyamlani au Malinzi, yoyote atakayekuwa
tayari atapata msaada wangu, kama watataka kueleza kitu kupitia gazeti
ninalolitumikia, basi mara moja nitafanya hivyo kwa kuwa ninajua Watanzania
wanataka kuwasikia na ndiyo kazi yangu.
Nafanya kazi kwa ajili ya wasomaji wa Championi na si nafsi
na mapenzi yangu, sijifurahishi, nafanya kitu ambacho nataka kitazamike na
kukubalika miongozi mwa wasomaji ambao ndiyo wenye gazeti hili.
Salamu kwa Nyamlani na Malinzi, huo ndiyo msimamo wangu.
Lakini pia salamu kwa wapambe wenu wanaoneza maneno yasiyokuwa na uhakika ili
kupata ‘kitu kidogo’ kwa ajili ya kuendesha maisha yao, hakuna nafasi kwa Saleh
Ally kuwa mpambe.
Nafanya kazi, hii ndiyo kazi yangu. Kwenye uandishi wa habari
sipiti, ndiyo kazi yangu na sijaingia kuifanya kwa kuwa nilikwama sehemu.
Nilikuwa nina ndoto nayo, naifanya kwa moyo mkunjufu na kama mafanikio
yatapatikana tu.
Wapambe fanyeni kazi zenu, acheni kugeuka makalani na
kuendeleza vita ya kudidimiza soka ya Tanzania. Tumbo huwa halilidhiki, njaa
huwa haishi hadi mwisho wa maisha, angalieni isiwapeleke kubaya. Natumia neno
njaa kwa kuwa siamini kama mtakuwa na mapenzi kupindukia na Malinzi na Nyamlani
bila ya kujali nafsi zenu. Tuupende kwanza mpira wa Tanzania na kusaidia
maendeleo yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment