March 20, 2013


 Mlezi wa Simba, Rahma Al Kharusi maarufu kama Malkia wa nyuki amesema hajatua katika klabu hiyo kwa lengo la kutaka madaraka.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mtandao huu, Malkia wa nyuki alisema, hakubaliani na yeye kuteuliwa nafasi ya makamu mwenyekiti katika mkutano wa wanachama uliofanyika wiki iliyopita.

“Nafikiri ingekuwa vizuri kama wangenitaarifu mapema, tukajadiliana na nikajua sababu hasa ya wao kufanya hivyo ni kitu kipi. Siwezi kuchukua nafasi hiyo, vizuri mambo yakafuata taratibu.

“Kuhusiana na suala la nini nataka Simba, nasisitiza sina shida na kiti wala mkeka, nataka maendeleo ya klabu kama mwanachama mwenye uchungu. Bado nina imani Simba inaweza kujirekebisha na kufanya vizuri zaidi ya hapa.

“Nataka kwenda Bukoba kusaidiana na vijana katika mechi dhidi ya Kagera, lakini ikiwezekana niungane nao Mwanza ili tuisaidie timu. Nafikiri hilo ndiyo jambo la msingi kwa wakati huu na si suala la nafasi au cheo kipi.


“Watu wote waangalie bado kuna mambo mengi ya kupambana, sitaki kukataza watu wasifanye jambo fulani, au kuzuia kitu fulani lakini nawashauri tuungane huku kwanza kuisaidia Simba.

“Nguvu yangu kubwa itaonekana msimu ujao, lakini naona si vizuri kuiacha timu ikaendelea kuyumba, ndiyo maana naendelea kupambana hadi mwisho wa msimu. Halafu shughuli itaonekana msimu ujao,” alisema Malkia wa nyuki.

Mwanamama huyo maarufu zaidi kwa kipindi hiki katika medani ya mchezo wa soka, amekuwa ndiye jembe na mkombozi wa Simba ambayo imekuwa katika matatizo lukuki kila kukicha kutokana na uongozi wake kutokuwa makini.

 Malkia wa nyuki amekuwa wa pili kukataa nafasi hiyo aliyoteuliwa baada ya Zacharia Hans Pope ambaye alipewa nafasi ya mwenyekiti wa Simba kwa muda baada ya wanachama hao kukutana.
Hata hivyo, tayari Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ameshasema kwamba walichofanya wanachama hao ni sawa na kikao cha harusi na akirejea nchini atawashughulikia.

Rage yuko nchini India anakopatiwa matibabu ya mgongo na ilielezwa, huenda angefanyiwa upasuaji.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic