TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wana habari,
KUMEKUWAPO na taarifa za
kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba uliopangwa kufanyika Kesho
(Machi 17, 2013) jijini Dar es Salaam kujadili mustakabali wa klabu.
Ikumbukwe kwamba Mkutano Mkuu wa
Wanachama ndiyo chombo cha juu kabisa cha maamuzi kwa klabu yetu. Katiba ya
Simba SC imeupa Mkutano Mkuu hadhi ya juu mno na ndiyo maana imeweka utaratibu
wa kufanyika kwake.
Miongoni mwa utaratibu ni kwamba
ni lazima uitishwe na Mwenyekiti aliye madarakani wa klabu. Kwa kushirikiana na
Kamati ya Utendaji, ndiye atakayepanga ajenda, mahali na wakati wa kufanyika
kwa mkutano wenyewe.
Katika miaka ya nyuma, zilikuwepo
nyakati ambapo klabu ilikaa hadi miaka mitatu pasipo kuitishwa kwa Mkutano Mkuu
wowote wa wanachama. Hakuna mwanachama au kikundi chochote kilichojitokeza kudai
mkutano wa dharura wakati huo ingawa ilikuwa ikifahamika kwamba huo ulikuwa ni
ukiukwaji mkubwa wa katiba ya klabu.
Tangu uongozi huu uingie
madarakani takribani miaka mitatu iliyopita, mikutano mikuu miwili ya wanachama
imefanyika kwa mujibu wa KATIBA. Mungu akijaalia, uongozi huu utafanya mkutano
mwingine wa kawaida wa wanachama baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kwa kuzingatia hali
halisi ya klabu, Mwenyekiti wa Simba, Alhaji Ismail Aden Rage (Mb), mwezi
uliopita alitangaza dhamira yake ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wakati
wowote kuanzia sasa.
Rage alisema mkutano huo ungekuwa
na ajenda moja tu; Kujadili Mwenendo wa Klabu kwenye mashindano inayoshiriki
msimu huu.
Kwa bahati mbaya, Mwenyekiti
alishikwa na maradhi na akapelekwa India kwa matibabu na yuko huko hadi Mola
atakapomjalia afya njema na kurejea. Kuna uwezekano mkubwa, Inshallah, akarejea
mwishoni mwa wiki ijayo.
Hii maana yake ni kwamba uongozi
umeridhia kufanyika kwa Mkutano wa wanachama. Kimsingi, kama uongozi umeridhia,
hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano mkuu mwingine.
Mwenyekiti ameruhusiwa kuitisha
Mkutano Mkuu kwa sababu alichaguliwa na wanachama na hivyo ana nguvu ya
kisheria (locus standi) kufanya hivyo. Hawa wengine wanaoitisha mkutano
wana nguvu gani ya kisheria kufanya hivyo?
Walichaguliwa na nani kuwakilisha
wanachama? Lini na wapi?
Uongozi pia unaweza kuitisha
mkutano kwa vile wenyewe ndiyo wenye leja ya wanachama. Klabu sasa ina database
yake ya kompyuta inayotambua wanachama walio hai na wasio hai.
Kwa kutumia database hiyo,
uongozi huu unatambua wanachama walio hai na wasio hai. Hakuna mtu mwingine
yeyote, aliye nje ya uongozi huu anayefahamu wanachama walio hai na wasio hai.
Hao wanachama wanaoitana kufanya mkutano, wamehakikiwa na nani kubaini uhalali
wao huo?
Uongozi wa Simba SC unaona kwamba
wale wanaolazimisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wana ajenda binafsi na si za
maslahi ya klabu. Kama kweli wangekuwa na nia njema na klabu wangesubiri
mkutano ambao utaitishwa punde.
Kwani, kuna uharaka gani wa
kufanyika mkutano kesho? Kwanini hawataki Mwenyekiti, ambaye wanachama walimpa
mamlaka ya kuongoza klabu kwa kipindi cha miaka minne, awepo kwenye mkutano
huo?
Kwanini hawataki kuungana na wana
Simba wengine kumwombea Mwenyekiti kwa Mungu ili amwepushe na ugonjwa na
kumrejesha salama hapa nyumbani? Kwanini mikutano hii iitishwe katika kipindi
ambacho uongozi umefungua mikono yake na kukaribisha kila mmoja mwenye mapenzi
mema na klabu kuja kuchangia?
Kwenye macho ya Katiba ya Simba
na sheria za Tanzania, huu mkutano wa kesho ni batili na una lengo la kuleta
vurugu na mifarakano kwenye jamii na michezo kwa ujumla wake. Michezo ni amani
na furaha na michezo si vurugu.
Tayari uongozi wa Simba umetoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
kuhusiana na ubatili wa mkutano huo. Tunapenda kuwaomba wanachama wetu
wasiopenda fujo na vurugu kwenye michezo kukaa mbali na mkutano huo kwa vile
vyombo vya dola vitaufuatilia.
Uongozi hautajiingiza katika
kutoa dhamana au msaada wa namna yoyote kwa yeyote ambaye atachukuliwa hatua na
vyombo vya dola kutokana na kujihusisha na mkutano huo.
Pia, Simba SC inatoa wito kwa
vyombo vya habari kuwa makini wakati vinaporipoti matukio ya vurugu kwenye
michezo. Kabla mtu hajahojiwa kujieleza kama mwanachama wa Simba, ni vema
kwanza akaonyesha kadi yake ya uanachama na risiti za malipo yake.
Wakati mwingine, waandishi huwa
tunawapa nafasi kwenye vyombo vyetu vya habari watu ambao hawana mchango wowote
kwenye kukuza michezo bali kuleta vurugu. Kwanini, tungejiuliza, ni watu wale
wale ambao kila mwaka huonekana wakati wa vurugu na wakati wa amani huwa
hawaonekani?
Kwanini, vyombo vyetu vinatoa
nafasi kwa watu ambao lengo lao ni kuhakikisha vilabu vyetu vinazidi kubaki
nyuma, vinakuwa na vurugu kila wakati na michezo inaonekana kama ni sehemu ya
wahuni na watu wasio na utaratibu?
Mpira bado haujaleta tija kubwa
kwenye uchumi wa Tanzania na kunufaisha wachezaji kwa sababu baadhi ya watu
makini na makampuni makubwa yanaogopa kujiingiza kwenye michezo kwa sababu ya
tabia kama hizi.
Ni vema vyombo vya habari
vikafanya jitihada kubwa katika kuwatambua waleta vurugu, si katika klabu ya
Simba pekee, bali kwenye sekta ya michezo kwa ujumla, ili visiwape nafasi ya
kuharibu na badala yake vitoe nafasi kwa wale wenye lengo la kujenga.
Tunasisitiza, uongozi huu
utaitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama Wote mara baada ya kurejea kwa Mwenyekiti.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
0 COMMENTS:
Post a Comment