Siku chache baada ya kutoroka na taarifa kueleza amekimbilia kwao Zambia, Felix Mumba Sunzu amerejea mazoezini, lakini kocha wake, Patrick Liewig akamzuia kufanya mazoezi.
Liewig raia wa Ufaransa, amemkataza Sunzu kufanya mazoezi na wenzake leo asubuhi na kutaka apewe maelezo alipokuwa amekimbilia bila ya kumpa taarifa.
Kocha huyo anayejulikana kwa umakini katika suala la nidhamu, amemtaka Sunzu kutoa maelezo ya kutosha ndiyo apime kama atamruhusu kuendelea naye.
Sunzu alipoulizwa kama alikimbilia Zambia alikataa katakata, ingawa taarifa zinaeleza hakuwa nchini.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala aliafiki kwamba Sunzu alipotea katika kikosi hicho kabla ya mechi ya Coastal Union na haikujulikana alipo.
Kilichotokea, siku moja kabla ya kuivaa Coastal Union, Sunzu hakuonekana na simu yake ilikuwa haipatikani.
“Kweli hayo yametokea, lakini Sunzu amesema alikuwa hapa nchini ila alikuwa kwake tu amezima simu,” alisema.
Sunzu naye alieleza suala hilo kuwa ni kutokea kwa upepo mbaya baada ya yeye kutoelewana na kocha.
“Ni kweli sikwenda mazoezini kwa siku kadhaa, niliamua kuzima
simu tu. Unajua ilitokea kutoelewana kati yangu na kocha, lakini nimeamua
kurudi kazini,” alisema.
Kuna taarifa kwamba kuna kundi la wachezaji ndani ya Simba
liko katika mgogoro wa chinichini na uongozi, ingawa zimekuwa zikifanyika
juhudi za dhati kufunika mambo hayo yasiende katika vyombo vya habari.
Lakini inaonekana hali bado haijatulia ndani ya Simba na kuna
madudu kibao ambao yanaendelea chini kwa chini, hali ambayo inaweza kusababisha
mambo makubwa zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment