April 16, 2013




Na Saleh Ally
HAKUNA anayeza kuyakataa mafanikio makubwa ambayo ameyapata mfanyabiashara maarufu wa jimbo la Katanga, Moise Katumbi Chapwe katika nyanja za madini.

Katumbi aliyelizaliwa mwaka 1964 akiwa ni ‘shombe’ wa Kikongo na Kiyahudi, baba yake mzazi raia wa Israel aliitwa Nissim Soriano.


Pamoja na mafanikio makubwa yaliyompatia mamilioni ya fedha na kuwa mmoja wa watu wenye nguvu ya kifedha barani Afrika, bado hakuwa maarufu sana hadi alipokuwa mmiliki wa timu ya soka ya TP Mazembe.


TP Mazembe ni moja ya timu vigogo barani Afrika kutokana na mafanikio makubwa iliyopata ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Afrika mara mbili chini yake, mwaka 2009 na 2010. Lakini kabla ya hapo, timu hiyo iliwahi kuwa bingwa Afrika mara mbili, 1967 na 1968.


TP Mazembe ilikuwa klabu kubwa, lakini ilishapoteza mwelekeo hadi Katumbi alipoingia na kuhusika na umiliki wakati akiwa ni Gavana wa jimbo la Katanga.

Uongozi wake una mafunzo mengi kwa timu za Tanzania, hasa Yanga na Simba ambazo zinaongozwa na wanachama ambao wanakuwa na sauti ya mwisho.

Kabla ya kurudi kwa wanachama, ubunifu na ujasiri wa Katumbi ndiyo umesababisha mabadiliko makubwa kwa timu hiyo ambayo sasa inamiliki uwanja mzuri wa kisasa pamoja na ndege mbili.

Lahisi kwa Watanzania kuifuatilia TP Mazembe kwa kuwa ina wachezaji Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu. Pia ni lahisi kujua inafanya kipi na inapita wapi.


Mfanyabiashara:
Katumbi hakuibuka kama mshumaa, Gavana huyo alianza kufanya biashara ya kuuza samaki ambayo ilikuwa inamuingizia faida ya dola 40 (Sh 64,000 tu kwa siku).

Lakini baadaye biashara yake ilienda inakua na akaendelea kujitanua hadi kuwa mfanyabiashara anayejulikana.

Hapa kinachoonekana kwa wafanyabiashara ambao wenye malengo, muhu ya mafanikio kama Katumbi ndiyo wanaweza kuleta mabadiliko katika soka ya Tanzania kupitia Yanga na Simba.


Ni timu kubwa, zenye mtaji mkubwa wa mashabiki na wanachama. Lakini hazipigi hatua na inawezekana zinaweka vigingi nyingine zisikue pia.

Kuimiliki:
Nguvu ya wanachama katika klabu za nyumbani bado imekuwa ni tatizo kubwa, kuna maamuzi yanaishia njiani kwa kuwa wanachama wamekuwa na hogu ya klabu zao kuuzwa na wao wakawa hawana sauti. Kila mwanachana na shabiki anataka kuwa na sauti ndani ya Yanga au Simba, hata kama hasaidii.


Uamuzi kama wa Katumbi kuamua kuimiliki TP Mazembe umesaidia, ndiye ana maamuzi ya mwisho na inakuwa lahisi kwake kufanya ubunifu au uamuzi wa mwisho wa kile anachokiamini.

Ujasiri:
Katumbi anaweza kuonekana ni ‘laini’ ndiyo na fedha zake zinaendesha kila kitu, si sahihi. Ingawa aliweza hadi kuuza samaki kuonyesha si mtu aliyeanza na raha, lakini baada tu ya kuchukua nafasi ya gavana wa Katanga, akamtimua nchini humo mfanyabiashara na milionea wa migodi, Billy Rautenbach.


Rautenbach alikabiriwa na tuhuma za masuala ya rushwa na wizi wa madini, lakini serikali ya Afrika Kusini ilikuwa ikimsaka pia. Baada ya kumtimua, Katumbi alibadili mfumo na fedha nyingi za machimbo ya madini ya Katanga zikawa zinatumika kwa faida ya eneo hilo.

Fedha hizo zimesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa katika eneo hilo na watu wakaanza kugundua kwamba faida nyingi ilikuwa ikipotea kutokana na madini kuibiwa na kusafirishwa nchi za nyingine nje ya DR Congo.

Wanachama:
Katumbi ni mchapakazi, asiye na hofu kuchukua maamuzi magumu ingawa angeweza kuwa na wakati mgumu kama angekuwa Yanga au Simba kwa kuwa wanachama ndiyo wamiliki na baadhi yao ndiyo wanaovuruga mambo.

Si lazima Yanga na Simba zibadili mfumo ili ziendelee lakini zinahitaji viongozi wafanyabiashara wenye mipango ya kujiendeleza kibiashara kama ilivyokuwa kwa Katumbi.

Lakini ikitokea akapatikana mtu kama huyo, bado atahitaji nafasi ya mabadiliko na anapaswa apewe nafasi ili awe kubadili mambo.

Anachokifanya Katumbi wala si miujiza, Tanzania kuna matajiri wengi, wanapenda mpira na wanaweza kuongoza, lakini mfumo unawakwaza na Simba na Yanga zinakufa tajiri pamoja na mtaji mkubwa wa watu wanaoziunga mkono ambao kuna timu lukuki zinalilia kuwapata.

Azam FC, ingawa inajichanganya na Usimba na Uyanga hasa kwa wafanyakazi wake wengine, lakini wamiliki wa timu hiyo wanaonyesha wamepania kuleta mabadiliko.

Katumbi si malaika, hata kama kisingizio kitakuwa kwa kuwa anamiliki migodi, lakini angekuwa hana mipango, ujasiri wa kuitekeleza na nafasi ya kutoa maamuzi magumu katika wakati sahihi, bado asingefanyikiwa.

Viongozi, mashabiki na wanachama wa Yanga na Simba wasifurahie mafanikio na rangi za Mazembe pekee, waangalie timu hiyo ya ‘porini’ inavyozidi kupata mafanikio wakati timu za kutoka mjini katika jiji la Dar es Salaam, zinapiga hatua nne mbele na kurudi hizohizo nne, mwisho wake, hadithi inakuwa ni ile ya “Wahapahapa”.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic