April 8, 2013



 
Ni zaidi ya joto la kawaida leo katika jiji la Manchester nchini England kutokana na hali ilivyo.

Sio joto kutoka angani, kila kitu ni moto kwa kuwa kuna mechi ambayo inaweza kusimamisha kila kitu bila ya kujali kina ukubwa gani. Kazi inaanza saa 4 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
 
Vikosi vitakavyokuwa...

Wenye mji, Manchester United na Manchester City wanapambana katika mechi muhimu ya Ligi Kuu England, mechi ambayo pamoja na upinzani mkubwa kati yao lakini inatakiwa kutoa majibu mengi.


Kwamba nani ni mbabe zaidi ya mwenzake, lakini kama City wakipoteza huenda ndiyo wameihakikishia United ubingwa. Na kama wasipopoteza, je, wanaweza kuizuia United. Maana City inashuka dimbani Old Trafford leo ikiwa nyuma kwa tofauti ya pointi 15!


Lakini bado kuna suala la heshima, kwa City itakuwa bora kushinda bila ya kujali kwamba ushindi kwao ni kuizua Man United kuwa bingwa au la.

Tayari Kocha Mkuu wa City, Roberto Mancini amesema anaamini kuifunga United ni kitu kinachowezekana lakini tiu nyingi zinayokutana nayo zimekuwa zikiihofia.

“Ni timu inayofungika, ila wengi wanalegea na kuamini kama haiwezekani kucheza na United na kuifunga. Mimi na wachezaji wangu tunaamini wanafungika na tutacheza kwa ajili ya kufunga na kushinda,” anasema Mancini.

Mchezaji Wayne Rooney wa United ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi katika mechi hiyo ya watani, amepachika mabao 10 ambayo ni idadi ya juu zaidi na analingana na wakongwe wengi ambao wamestaafu, kama akifunga leo basi atakuwa anashikilia usukani wa waliofunga mabao mengi katika mechi kati ya City na United, tokea kuanza kwake.

Kocha Alex Ferguson anaamini ana kikosi bora zaidi ambacho kina kila sababu ya kushinda nyumbani, ingawa amesisitiza ugeni wa City hauwezi kuwa mkubwa sana kwa kuwa ni jirani zao wanaotokea hapo jijini Manchester na tofauti ya timu hizo ni mitaa tu.

Wawili:
Katika kipindi kifupi kilichopita, wachezaji Rooney na nahodha wa City, Vincent Kompany ndiyo walioonekana kuwa viongozi wa timu zao hasa zinapocheza mechi hiyo muhimu ya watani.

Kompany amekuwa na mchango mkubwa katika ulinzi na wakati mwingine amefunga mabao ya ushindi lakini Rooney amekuwa akiongoza vilivyo mashambulizi kwa United.

Hata hivyo, Robon van Persie ni mtu wa kuchungwa sana kama ilivyo kwa Kun Aguero na Carlos Tevez upande wa City.

Atakumbukwa:
Hakuna anayeweza kukataa, kwamba Mario Balotelli ataendelea kuwa mmoja wa wachezaji watakaokumbukwa katika mechi ya leo.
Alikuwa akifanya vituko karibu kila mechi lakini alionyesha uwezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao muhimu. Hatakuwepo na huenda atakuwa katika ‘kideo’ nchini Italia akipiga chabo mechi hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic