Kamati ya Ligi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi
sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria
imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza
(FDL).
Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa
kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha
daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo
kwenye mechi mbili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT
na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika
mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka
huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa
faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi
milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu
hiyo waingie bure uwanjani.
Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza,
Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya
kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya
Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.
Nao wachezaji Joseph Mapalala,
Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara
wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya
vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya
Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa
kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.
Klabu ya Villa Squad imepigwa faini
ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United
wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake
kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.
Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa
Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye
mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa
ajili ya hatua za kinidhamu.
Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga
unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia
marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.
BONIFACE WAMBURA
MSEMAJI TFF
0 COMMENTS:
Post a Comment