April 3, 2013



 
Na Saleh Ally
WATU kadhaa wameishasema bila ya woga kwamba Kelvin Patrick Yondani ndiye beki bora wa kati nchini kwa kipindi hiki.
Yondani maarufu kama Cotton ndiye beki kisiki wa Yanga na uchezaji wake umekuwa ukionekana kuimarika katika mechi za timu yake.

Uchezaji wa Yondani umesababisha mashabiki wa Yanga wajenge imani kwake kupitiliza, kwani pamoja na kuwa na mabeki kibao imara, lakini anapokosekana wengi wamekuwa wana hofu.

Hata kama Yondani atakuwa nje, beki ya Yanga haipaswi kuwa na hofu kwa kuwa wana wachezaji wa kati mahiri kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite.

Hilo kwa mashabiki haliingii ‘akilini’ mwao kwa kuwa uimara wa Yondani, unasababisha waamini bila yeye katika safu ya ulinzi, basi mambo yatakuwa yanakwenda kwa kubahatisha.


Achana na mashabiki, makocha wote kutoka barani Ulaya ambao wamemfundisha ndani ya miezi 12 wameonyesha kuwa na imani naye ikiwezekana kuliko mchezaji mwingine yoyote.

Brandts:
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts huenda anaweza kuwa na nafasi nzuri sana ya kuzungumzia ubora wa Yondani kwa maana ya namna anavyocheza kwa kuwa yeye amekuwa beki hadi timu ya taifa ya Uholanzi iliyocheza Kombe la Dunia.


Kuhusiana na Yondani, Brandts anasema: “Kama ingekuwa Ulaya, ningeweza kusema Yondani alihitaji urefu kiasi zaidi ya hapo, lakini hapa Afrika ana kila kitu.

“Urefu wake unatosha, kitu kizuri alichonacho, ana uwezo mkubwa sana wa kupiga vichwa. Hii inafuta kabisa hisia za kocha kutaka aongezeke urefu zaidi ya hapo.

”Lakini ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, pia kasi yake ni bora. Ninasema hivyo kwa kuwa mara nyingi beki wa kati anatakiwa kuwa mfuta makosa.

“Kawaida mchezaji anapokwenda kufuta makosa hutakiwa kuwa na vitu viwili, kasi na utulivu wa akili anapokuwa amefikia eneo la tukio. Karibu kila mchezo, Kelvin amekuwa akirekebisha zaidi ya makosa matatu kwa ufasaha.”

Poulsen:
Ukiachana na Yanga, Yondani ni tegemeo katika safu ya ulinzi ya timu ya taifa, Taifa Stars. Kocha wake Kim Poulsen anasema ana imani kubwa:


“Kwangu Kelvin ni msikivu sana, anacheza ambavyo unamuelekeza. Kuna mambo kadhaa nilitaka ayapunguze, pia alifanya hivyo. Uchezaji wake ni wa uhakika na unapokuwa naye, hautegemei makosa mengi ambayo yanakuwa ni tatizo kwa timu.”

Milovan:
Kocha wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic ni mmoja wa makocha waliomfundisha Yondani kwa kipindi kirefu. Yeye aliwahi kuwaambia Simba wafanye juu chini kuhakikisha Yondani haondoki na kujiunga Yanga, aliporudi akakuta mambo tofauti.

 “Nilipoambiwa ameondoka, nikahisi kutakuwa na tatizo kwa kuwa msimu mzima sikuwa nimekutana na timu iliyokuwa na beki kama Kelvin. Ndiyo maana tulipata shida sana katika mabeki wa kati waliokuja kucheza Simba.


“Lakini wakati naanza naye, pia wako viongozi waliamini hafai. Nikawaambia waniachie, kuna baadhi ya vitu nilitaka aache kama vile kuvuta mpira muda mrefu, badala yake awe anauacha kwa viungo au kupiga mbele.

“Hadi nimeondoka naweza kusema kwa Watanzania, kipa bora ni Kaseja, beki bora ni Yondani na kiungo bora zaidi ni Boban (Haruna Moshi),” anasema Milovan raia wa Serbia.

Rekodi:
Pamoja na imani kubwa kutoka kwa makocha hao wageni, Yondani analindwa na rekodi, Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara lakini safu ngumu ya ulinzi ni ya Yanga kwa kuwa katika mechi 21, imeruhusu mabao 12 tu ukiwa ni wastani bora zaidi.

Azam FC katika mechi 21 imeruhusu mabao 16, Kagera katika mechi 22 imefungwa mabao 17 wakati Simba iliyo katika nafasi ya nne, imefungwa 19 kati ya 21 ilizocheza.

SOURCE: GAZETI LA CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic