Na Saleh Ally
WACHEZAJI wengi wa Tanzania wameamua kujivika uzee na kubaki
mitaani wakicheza mechi za ‘maharage’, maarufu kama ndondo lakini uwezo wao ni
mkubwa sana.
Inawezekana kabisa kama utafanyika mchujo katika mechi za
mchangani au mashindano maarufu kama bonanza, basi utapata wachezaji wengi tu
ambao umri wao ni kuanzia miaka 25 lakini wanaweza kuwa msaada mkubwa katika
timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
Wapo wachezaji ambao wameamua kustaafu soka mapema na
wamerudi kucheza mchangani ambako wanapata malipo kupitia katika timu za
mchangani ambazo zinakuwa na wadhamini wanaosikia ufahari kuwa na wachezaji
waliong’ara zamani.
Hali inaonyesha kwamba, wachezaji wengi ambao wamestaafu soka
mapema, bado maisha yao si mazuri na wamekuwa wakihangaika kwa kuishi kwa fedha
kidogo za kuchangisha.
Inawezekana wamekata tamaa mapema kutokana na mazingira
waliyopitia, tatizo kidogo linaweza kuwa kwao kwa kushindwa kuwa makini au
kujitafutia angalau miradi midogo ili wajiendeleze watakapostaafu.
Lakini viongozi wanaokuwa katika timu wanazochezea, ndiyo
wanakuwa tatizo kubwa sana kwa kuwa huwajali wachezaji hao kwa muda tu na baada
ya hapo wanasahau kila kitu kuhusiana nao.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Godfrey Bonny, maarufu kama Ndanje,
ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiitwa “Babu” na ikaonekana hawezi kucheza
Yanga kwa madai kwamba ni mzee sana.
Ilikuwa ni rahisi kwa Ndanje naye kurudi katika mkumbo huo wa
kucheza ‘mabonanza’, lakini alifanya mambo mawili makubwa ambayo
yanamtofautisha na wachezaji wengi wenye uwezo kama wake au zaidi ambao sasa
wanasumbuka na kuishi maisha ya kubahatisha katika timu za mchangani.
Ndanje, askari magereza wa zamani, alikubali kurudi Mbeya,
kitu ambacho ni kigumu kwa wachezaji wengi ambao wanaamini maisha yanapatikana
jijini Dar es Salaam pekee.
Baada ya kutua huko, alijiunga na timu ya Mbeya City na
kujifua vilivyo. Alirejea na kupata namba na kuonyesha kwa nini alikuwa tegemeo
alipokuwa Prisons, Yanga na hata timu ya taifa.
Wakati akiwa fiti, pamoja na kuonekana ni mzee, Ndanje
hakujali, aliendelea kuangalia nafasi ya kucheza soka nje ya Tanzania, baadaye rafiki
yake, Yona Ndabila ambaye ni mshambuliaji tegemeo wa timu ya Ligi Kuu ya
Swaraswot Youth Club ya nchini Nepal, akamtafutia timu.
Ikaonekana kama haiwezekani, lakini Ndanje alitua Nepal na
baada ya siku chache alipata namba katika kikosi cha kwanza cha Swaraswot Youth
Club na amekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kwenye kikosi hicho.
Mafanikio hayo ya Ndanje yanaweza kuonekana ni madogo lakini
yanafaa kuwafungua macho wachezaji wengi wenye uwezo, kwamba wanaweza kupata
nafasi katika nchi kama Nepal na nyingine ambazo kiwango chao si cha ushindani,
kama ulivyo wa Ulaya na wakacheza.
Lakini pia wanaweza kuendelea kucheza katika timu nyingine
kama Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na nyingine ambazo hazina presha za wanachama
na wakaendelea kupata ajira badala ya kutegemea misaada au huruma ya watu
fulani.
Ndanje bado anaishi kwa ajira yake, lakini pia ameweka rekodi
ya kuwa mmoja wa Watanzania waliocheza soka la kulipwa bila ya kujali ni nchi
gani, kuliko angebaki mchangani na kusubiri huruma.
Wapo wengi wanaweza kufikia hapo, leo wanasumbuka kucheza
timu za mchangani, yote hiyo inatokana na ugumu wa wao kuamini uwezo wao, pia
kukata tamaa mapema.
SOURCE: GAZETI LA CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment