Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa
Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye
vizuri katika mechi yake ya leo dhidi ya Morocco mjini Marrakesh.
Stars, ambayo inashika nafasi ya pili
kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory
Coast kwa tofauti ya pointi moja, leo inacheza na Morocco katika mechi ya nne
itakayofanyika Marrakesh baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi
ya kwanza iliyofanyika Dar es salaam mwezi Machi.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF
haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo
imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya USD
milioni 10.
“Katika kipindi chote hiki hatujawahi
kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema
Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.
“Lakini katika mwaka mmoja uliopita
(tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa
kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu
sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki
na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi.
“Posho za wachezaji zimepanda kwa
karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni
kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”
Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio
sasa umeanza kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na
maandalizi ya muda mrefu.
“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee
timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia timu kwa kuwa
vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema
Tenga.
Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo
cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji,
akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro,
George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na
kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.
Katika mkutano huo, Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii Tanzania (NSSF) ulikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao
wamekwenda Morocco kuishangilia timu. Afisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma
Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na
nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana.
0 COMMENTS:
Post a Comment