Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema
ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika
kwenye Miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea
tamko la serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga amesema serikali zimeshafanya
mazungumzo na kwamba serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa
ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na
mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya
kutoa tamko.
“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo
wa CECAFA. Kwa hiyo, kama serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri,
hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama
vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano
na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa
usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji
usalama kwa kuwa ni wajibu wa serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga alisema kuwa mashindano hayo
yalikuwa yafanyika Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba
isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa
mashindano hayo.
Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius,
CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya
mashindano hayo kutoka uongozi wa chama cha mpira wa miguu cha Sudan na
wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA
zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri
wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya
kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri
tamko la serikali,” alisema Tenga.
“Lakini napenda kuishukuru serikali
ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo.
Tayari Katibu Mkuu wa CRCAFA (Nicholaus Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo
hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika
nazo,” alisema.
Alisema watu wasipotoshe tamko la
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa
Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe. Membe alisema serikali itafanya
uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema serikali
haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,”
alisema Tenga.
“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF
kuipa serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa
mashindano, sasa tunasubiri tamko la serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa
kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa
usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA
kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho
kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa
majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama
chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na serikali ya Sudan
ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.
“Sasa ikitokea serikali yetu ikasema
hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama
yako nje ya CECAFA.”
0 COMMENTS:
Post a Comment