MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf
Manji, amebariki kutemwa kwa mshambuliaji mpya wa Yanga,
Ogbu Brendan Chukwudi,raia wa Nigeria, lakini akawageukia nyota wanne katika kikosi hicho na
kuwakabidhi jukumu moja kubwa.
Ogbu
alitua nchini hivi karibuni kujaribiwa na Yanga, lakini nyota huyo alionyesha
uwezo mdogo sambamba na kuwa majeruhi kila wakati, matatizo ambayo yaliilazimu
klabu hiyo impe nauli ya kurudi kwao haraka.
Akizungumza
na Championi Jumatano, Manji amesema kwa sasa
hawatahangaika kumtafuta straika yeyote kutoka nje, badala yake washambuliaji
waliopo sasa katika kikosi hicho wanatakiwa kuonyesha uwezo mkubwa kwa kufunga
mabao msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kikosi
hicho mpaka sasa kimesaliwa na washambuliaji wanne ambao ni Jerry Tegete, Said
Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Shaban Kondo na Hussein Javu, aliyesajiliwa hivi
karibuni akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Manji
alisema endapo nyota hao wanahitaji kubaki katika kikosi hicho mzunguko wa pili
wa ligi, wanatakiwa wafanye kazi yao ipasavyo ya ufungaji. Alisema endapo hilo
litashindikana, Yanga itatumia kiasi chochote cha fedha kusajili nyota wapya
katika dirisha dogo la usajili, Januari, mwakani.
“Tumewasajili
ili waweze kuhakikisha Yanga inapata mabao mengi katika mechi zake, ndiyo maana
tunawalipa fedha za kutosha, kwa sasa hatutasajili mshambuliaji yeyote,
tunataka hawa tulionao sasa wafanye kazi yao ipasavyo, ndiyo maana tukamuongeza
na Ngassa ili aongeze nguvu katika timu,” alisema Manji na kuongeza:
“Tunaamini
bado wana uwezo mkubwa, ndiyo maana tumeamua kuwapa muda zaidi, wakishindwa
kutupa kile tunachohitaji, tunaweza kuwaondoa na kutafuta wachezaji wengine
katika dirisha la usajili lijalo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment