Mchezo wa soka ni kati ya michezo
inayotoa ajira kiwango kikubwa sana, hii si Tanzania tu, badala yake sehemu
kubwa duniani.
Wanasoka ni kati ya waajiriwa wanaolipwa
vizuri zaidi kuliko maprofesa au marais wa nchi mbalimbali duniani na wengi ni
matajiri.
Utajiri wa ukanda wa soka unatokana na
umakini unaofanywa na watu wanaoongoza mchezo huo hasa katika nchi
zilizoendelea kisoka.
Mfano mzuri utakuwa ni Ulaya, timu za
huko ni tajiri na ndizo zinaongoza kulipa mishahara ya kufuru kwa wachezaji na
makocha wake. Malipo hayo gumzo hayapatikani kutoka hewani.
Timu hizo zinafanya mambo kadhaa ambayo
yanazisaidia kuwa bora kifedha na moja ya nguzo ya kutafuta fedha kwa uhakika
ni viingilio vya uwanjani.
Hivyo mashirikisho yanapotumia wataalamu
wake kupanga ratiba zinahakikisha suala la biashara linaangaliwa. Hakuna
ubishi, soka ni biashara na si burudani pekee.
Timu zinahitaji kujiendesha na kila kitu
ni fedha. Mfano kambi, usafiri na mambo mengine muhimu, yote ni mamilioni ya
fedha. Hivyo lazima kuwe na akili ya biashara ili kufanya mambo yaende vizuri.
Kwa hapa nyumbani, Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), linategemea kujiendesha kwa fedha zinazopatikana katika ligi
hiyo pamoja na fedha za msaada kutoka katika Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa).
Ndiyo maana nataka kusisitiza kwamba
wataalamu wa TFF wanapokuwa wanapanga ratiba ya Ligi Kuu Bara, basi wana kila
sababu ya kuangalia suala la biashara, kwamba siku gani ni nzuri kwa timu
husika kupata fedha nyingi.
Mfano mzuri ni mechi kati ya Yanga dhidi
ya Coastal Union ambayo ilichezwa Jumatano, siku ya kazi, yenye foleni
zinazokera. Lakini wapangaji ratiba wa TFF walionyesha wazi hawakuwa na wazo la
biashara badala yake wanaangalia nani acheze na nani.
Achana na ukubwa wake kihistoria, lakini
Coastal Union sasa ni kati ya timu tano za juu na zenye umaarufu mkubwa, hivyo
kila inapokutana na Yanga au Simba, basi inakuwa ni “big match”, hilo halina
ubishi.
Sasa tatizo ni lipi kama mechi hiyo
ikipangwa Jumamosi au Jumapili, siku ambayo mashabiki wanaweza kujitokeza kwa
wingi zaidi kwa kuwa siku hizo wanakuwa na nafasi zaidi ukilinganisha na
Jumatano.
Kuangalia suala la foleni hasa kwa siku
za katikati ya wiki ni muhimu, inawezekana mapato ya Yanga dhidi ya Coastal
ambayo yametangazwa kwamba ni Sh milioni 152, yangeweza kuwa zaidi ya hapo kwa
asilimia 50 nyingine kama mechi hiyo ingechezwa Jumamosi au Jumapili.
Wakati wa upangaji ratiba lazima
kuangalia mazingira halisi ya miji pia, mfano foleni kubwa za Dar es Salaam,
maana wako wanaotaka kwenda uwanjani lakini wakakwazwa na foleni, au muda
waliochelewa kutoka kazini.
Mechi za Septemba 14 ligi itakapoanza
tena nyingi zimezingatia hilo, mfano angalia Simba dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar au Coastal na Prisons mjini Tanga na Mbeya City na Yanga
jijini Mbeya.
Inawezekana mechi nyingine zisiwe kubwa
sana, lakini zikapata watu wengi kwa kuwa siku zitakazochezwa inakuwa inatoa
nafasi kwa mashabiki.
Lakinikatika ratiba hiyo hiyo,
ukiangalia mechi za Septemba 21 utagundua Simba itakuwa Uwanja wa Taifa ikiivaa
Mbeya City, lakini ajabu kabisa siku inayofuata kutakuwa na mechi mbili. Moja,
Uwanja wa Taifa na nyingine Azam Complex.
Maana yake ni hizi, ndani ya siku mbili
katika jiji la Dar es Salaam kutakuwa na mechi tatu. Mashabiki watakwenda
Uwanja wa Taifa kwa siku mbili mfululizo, sawa si tatizo. Lakini ile mechi ya
JKT Ruvu dhidi ya JKT Oljoro itakayochezwa siku moja na ile ya Yanga na Azam
FC.
Hii inaonyesha kiasi gani TFF haijali
timu kama JKT Ruvu kama zinahitaji pia kupata mapato, hapa limeangaliwa suala
la kukamilisha ratiba na uzuri wa uwanja wa kuchezea. Lakini haki angalau
wangecheza kwenye uwanja wao wa Mabatini mkoani Pwani ambako mashabiki
wangeweza kujitokeza.
Inawezekana kabisa kwa ratiba ya timu 14
kukaangaliwa suala la mapato, nasisitiza soka ni biashara na si ilimradi kila
timu icheze tu basi. Ondoeni hisia za kwamba timu fulani kawaida haina
mashabiki, katika maisha mabadiliko yanatokea kwa kuwa kuna mipango.
0 COMMENTS:
Post a Comment