Na Boniface Wambura, Banjul
Kikosi
cha Taifa Stars kimewasili salama hapa Banjul, Gambia tayari kwa mechi ya
mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji itakayochezwa kesho (Septemba 7 mwaka
huu).
Lakini
kivutio zaidi ni uamuzi wa Kocha Mkuu, Kim Poulsen kumpanga winga mwenye kasi wa
Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas kama beki wa kulia na Henry Joseph amemrudisha
katika namba yake, atakipiga namba nne.
Kikosi
kamili cha Poulsen; Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto Nyoni, Nadir Haroub,
Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa, Simon
Msuva na Khamis Mcha.
Stars imewasili hapa jana (Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni
ikitokea Dakar, Senegal ambapo ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua
kutumia usafiri wa barabara kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko
kuingia Banjul badala ya kulala na kuchukua ndege nyingine siku inayofuata.
Wachezaji wako katika hali nzuri na leo jioni wanatarajia kufanya
mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Independence ulioko Bakau ambao utatumika
kwa mechi ya kesho. Timu imefikia hoteli ya Seaview iliyoko kandokando ya
Bahari ya Atlantic.
Mechi hiyo itaanza saa 10.30 jioni kwa saa za hapa ambapo nyumbani
Tanzania itakuwa saa 1.30 usiku, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda
Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene Ndagijimana, Honore Simba na Issa
Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka Liberia.
Washabiki na vyombo vya habari vya hapa wanaizungumzia mechi hiyo
ambayo ina umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia ikiwa imeita wachezaji
tisa wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo imepata uongozi mpya wa
Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania kuhakikisha haimalizi mechi za
mchujo ikiwa na pointi moja tu.
Kwa upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema nia ni kuona
Stars yenye pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast
ambayo tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho kutoka kundi
hili la C.
“Mechi hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka matokeo mazuri
ugenini. Lakini kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka katika nafasi
ya kuwa wa pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi kwenye viwango
vya ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi ya sisi
kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim.
0 COMMENTS:
Post a Comment