November 25, 2013





Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwenyekiti wa klabu ya Simba Ismail Rage amewapanga mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa ajili ya kumshangilia.

Utafikiri kocha wa timu fulani aliyekuwa anapanga fomesheni ya 4-4-2 au 4-3-3 katika ushambuliaji, naye akaamua kuwaelekeza mashabiki namna watakavyomshangilia wakati anatoka kwenye chumba baada ya mkutano na waandishi kwenye makao makuu ya klabu hiyo.


Tukio hilo la aina yake lilifanyika kwenye Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyopo Msimbazi jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari.

Mwenyekiti huyo, akisubiliwa na kundi kubwa la mashabiki hao nje ya ofisi hiyo ya Simba, alionekana na kusikika akiwapanga kwa ajili kumshangilia.

Rage alimuita pembeni mmoja wa komandoo na kumtaka ashuke kutoka ghorofani haraka na kwenda kuwaambia mashabiki wajiandae kwa ajili ya kumshangilia akiwa anatoka mjengoni hapo.

Mwenyekiti huyo alisikika akiwaambia waandishi wa habari kuwa “Mnataka mnione nikiwa nashangilia na mashabiki basi subilini muone ntakavyoshangiliwa.

“Anzeni nyie waandishi wa habari kuanza kushuka chini mkiwa na kamera zenu muone nitakavyoshangaliwa, ndiyo muamini kuwa napendwa,” alisema Rage.

Waandishi bila kujali, haraka wakashuka chini na kukuta kundi la mashabiki waliokuwa wanamsubili mwenyekiti kwa shauku kubwa kwa ajili ya kumshangilia.

Mara baada ya kushuka chini alipokewa na mashabiki hao kwa shangwe kwa kumpa mikono na wengine kumnyooshea wakimpongeza wakimtaka kuendelea madarakani.

Aliposhuka chini alisimama kama dakika tano kwa ajili ya kuzungumza na mashabiki hao na baadaye kuelekea kwenye gari aina ya Toyota V6 Granvia lenye namba T 300 CPR.

Baada ya kuingia kwenye gari alifungua dirisha la juu la gari hilo na kusimama na kuwapungia mikono mashabiki hao waliosikika wakiimba Simba! Simba! Simba! Simbaaa! Kwa sauti kali hadi gari hilo linaoondoka likisukumwa na kundi hilo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic