Mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester
United, Andy Cole anatarajia kutua jijini Dar es Salaam Ijumaa hii, imethibishwa.
Ziara ya Cole nchini inalenga kuwapatia
uzoefu washindi wa tiketi za promosheni ya Airtel ya 'Mimi ni Bingwa' ambao
watasafiri kwenda kuangalia mechi za klabu ya Manchester United moja kwa moja
(live) katika uwanja wa Old Trafford pamoja na kukabidhi vifaa vya mazoezi
kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ya chini ya umri wa miaka 17.
Hii ni ziara ya pili Tanzania kwa
mchezaji Cole baada ya kutembelea Tanzania mwaka 2011 alipozindua mpango wa
kutafuta vipaji wa Airtel Rising Star.
Akizungumza na waandishi wa habari juu
ya ziara hiyo, Meneja Uhusiano wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania, Bw
Jackson Mmbando alisema kuwa mchezaji huyo mkubwa wa zamani wa Man U atakuwa na
wakati wa kuzungumza na kushiriki mazoezi na wachezaji wa timu ya Tanzania
chini ya miaka 17, timu ambayo wengi wao ni matunda ya mpango wa kuvumbua
vipaji wa Airtel Rising Star.
"Andy Cole ataongea na nyota hao
wanaochipukia, na kuwashawishi kuongeza jitihada zaidi katika michezo pamoja na
kuwapatia mbinu za jinsi gani ya kufikia mafanikio katika fani yao ya michezo.
"Mbali na kuwaonyesha wachezaji
hao njia ya mafanikio, mchezaji huyo mkubwa wa zamani wa Manchester United pia
atakabidhi vifaa vya mazoezi kwa timu hiyo," alisema Mmbando.
Alisema kuwa Cole pia atahudhuria droo
ya moja kwa moja (live) ya kuwatafuta na kuwatangaza washindi wa tiketi tatu za
kwenda Old Trafford, kabla ya kuungana na washabiki wa Man U kuangalia mechi
moja kwa moja (live) itakayoonyeshwa Coco beach kati ya Manchester United na
Aston Villa itakayochezwa jumapili.
Rashid Jacob Kagomola na Dickson Lyatuu
ni washindi wa kwanza wawili wa promosheni ya Mimi ni Bingwa waliojishindia
tiketi za kwenda Old Trafford, ambapo zawadi zaidi ya shilingi milioni 40
tayari imetolewa kwa ajili ya washindi wa kila siku na kila wiki.
Mmbando alisema kuwa bado kuna zawadi
nyingi zaidi kushindaniwa katika promosheni, na kuongeza kuwa ili mteja
kushiriki anatakiwa kutuma ujumbe mfupi (SMS) wa neno "BINGWA" kwenda
namba 15656.
Aidha, alisema Airtel imeweka vituo
mbali mbali ambavyo washabiki wa Man U wataweza kuangalia mechi za Manchester
United moja kwa moja (live) kupitia luninga kubwa, na kutaja vituo hivyo kuwa
ni Mbeya - Shaba Pub, Mwanza - Shooters Pub, Dodoma - Four ways, Dar es Salaam
- Coco Beach, Morogoro - Nyumbani Lounge na Arusha - Empire Sports Bar.
Mwaka 2011 kampuni ya mawasiliano ya
Airtel Tanzania ilizindua mpango wa kuvumbua vipaji katika soka kwa ushirikiano
na klabu ya Manchester United, uliolenga kuvumbua vipaji na kuviendeleza katika
mpira wa miguu Tanzania.
Cole amekuwa na dhamira ya kuonyesha
uzoefu wake kwa wachezaji nyota wanaochipukia ikiwa ni kama njia ya kuunga
mkono maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu duniani.








0 COMMENTS:
Post a Comment