NKONGO (KATIKATI) WAKATI ALIPOCHEZESHA MECHI KATI YA RWANDA DHIDI YA RWANDA, HAPA AKIZUNGUMZA NA KIUNGO WA AMAVUBI, HARUNA NIYONZIMA. |
Watanzania wanane wameteuliwa kuchezesha mechi mbili za
marudiano za raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho zitakazochezwa
wikiendi ya Februari 14 na 16 mwaka huu.
Waamuzi hao walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(Caf) ni Israel Mujuni atakayechezesha mechi ya CL kati ya Rayon Sport ya
Rwanda na AC Leopards de Dolisie ya Congo itakayofanyika jijini Kigali.
Mujuni atasaidiwa na Josephat Bulali, Samwel Mpenzu na Ramadhan
Ibada, wakati Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Jean Marie Hicuburundi wa Burundi.
Naye Waziri Sheha ataongoza jopo lingine kwenye mechi ya CC kati
ya FC MK ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na El Ahly Atbara ya Sudan.
Mechi hiyo itachezwa jijini Kinshasa.
Sheha atasaidiwa na Ferdinand Chacha, John Kanyenye na Israel
Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo ni Chayu Kabalamula kutoka Zambia.
SEMINA YA KUPANDISHA MADARAJA WAAMUZI
JAN 21
Semina kwa ajili ya kupandisha madaraja waamuzi itafanyika
Januari 21 na 22 mwaka huu katika vituo vitatu vya Dodoma, Mwanza na Songea.
Waamuzi watakaoshiriki katika semina hizo ambazo pia zitahusisha
mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) watajigharamia wenyewe na
wanatakiwa kufika vituoni siku moja kabla. Waamuzi hao ni wa daraja la pili na
tatu.
Kituo cha Dodoma kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar
es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Pwani, Singida na Tanga.
Wakufunzi katika kituo hicho ni Paschal Chiganga, Said Nassoro na Soud Abdi.
Wakufunzi wa kituo cha Mwanza kwa ajili ya waamuzi wa mikoa ya
Geita, Kagera, Katavi, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora ni Alfred
Kishongole, Kanali Issarow Chacha, Saloum Chama na Zahra Mohamed.
Kituo cha Songea ni kwa ajili ya waamuzi kutoka Iringa, Lindi,
Mbeya, Mtwara, Njombe, Rukwa na Ruvuma. Wakufunzi katika kituo hicho ni Charles
Ndagala, Joseph Mapunda, Riziki Majala na Victor Mwandike.
Waamuzi wote wanatakiwa kwenda katika kituo walichapangiwa.
Vilevile wanatakiwa kuwa na barua kutoka kwa makatibu wa Vyama vya Waamuzi wa
Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) wa mikoa yao ikiwatambulisha pamoja na kuonesha
madaraja yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment