Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji Emmanuel
Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa).
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo (Januari 22 mwaka huu)
kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi
aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.
Okwi
ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa
na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi
sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel
likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Katika
FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi
ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki
mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa
kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.
Hivyo,
TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi
nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho
hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment