Kiungo wa Simba SC, Henry Joseph,
amewasihi mashabiki wa timu hiyo kuwa wavumilivu licha ya matokeo mabaya
waliyoyapata katika mechi zao za hivi karibuni kwenye Ligi Kuu Bara.
Simba iliyopo nafasi ya nne kwenye
mzunguko wa lala-salama wa ligi kuu msimu huu, imepata matokeo mabaya katika
mechi zake tatu mfululizo kwa kutoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, kisha
kufungwa na Mgambo JKT 1-0, kabla ya kutoka sare nyingine ya 1-1 na Mbeya City.
Henry
alisema kuwa anajua wazi kuwa mashabiki wanaumia kutokana na matokeo hayo
lakini amewataka kuwa wavumilivu kwani wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha
wanapata matokeo mazuri lakini mwisho mambo huwa mabaya.
Alisema kuwa Simba bado ina nafasi ya
kumaliza katika nafasi nzuri za juu na kwamba kwa sasa wamejipanga vya kutosha
kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizobaki ili kuwapa mashabiki kile
wanachokitaka.
“Matokeo tunayopata ni sehemu ya mchezo,
huwa tunapambana ili kupata matokeo mazuri kwani tunajua kuna mashabiki kibao
nyuma yetu huwa wanataka kuona tunashinda, lakini bahati mbaya hutokea kinyume
na matarajio yetu,” alisema Joseph.
0 COMMENTS:
Post a Comment