MAKOCHA wa
Yanga na Simba, wamekuwa wakizungumza sana kuhusiana na kutoridhishwa na
viwango vya wachezaji walio katika vikosi vya timu zao.
Si mara
moja, Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic alikuwa akizungumzia suala la
kutofurahishwa na viwango vya wachezaji wake kuanzia mazoezini hadi kwenye
mechi.
Awali kwa
kuwa alizungumza kocha huyo raia wa Croatia na ana sifa ya ukorofi, wengi
waliamini ni maneno ya kikorofi. Lakini Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm naye
alisema hilo kwamba kuna wachezaji ambao viwango vyao havimridhishi.
Kauli ya
Pluijm ilikuwa ni kusisitiza kuhusiana na namna ambavyo wachezaji wake
wanavyoweza kufanya anachotaka kifanyike. Hiyo ndiyo sifa ya uwezo wa mchezaji,
kwamba anaweza kubeba alichopewa, halafu akiingia uwanjani anafanya kile pamoja
na ziada.
Kiwango cha
wachezaji ni kitu kinachobeba mambo mengi sana, si uwezo wa mchezaji kukimbia
na kutoa pasi tu kwa mbwembwe anapokuwa uwanjani.
Kwa
mashabiki wengi wa soka, wanavutiwa zaidi na wachezaji wenye kasi kwa kuwa watakimbia
kwa kasi na ndiyo maana hushangilia kwa nguvu sana. Lakini kama hiyo haitoshi
mashabiki huvutiwa na wachezaji wenye uwezo wa kupiga chenga za maudhi.
Sawa yote
yanahitajika katika soka, lakini kadiri siku zinavyosonga mambo yanabadilika
sana na wachezaji wanatakiwa kuwa na vitu vingi vya ziada ambavyo vitawasaidia
kufanya mambo mengi wanayoagizwa na kocha.
Mfano,
mchezaji anajua namna ya kumiliki mpira. Adui anapokuwa kulia yeye atauhifadhi
kushoto. Wakati anakimbia na mpira afanye nini na sahihi mpira uwe umbali gani
anapokuwa kwenye kasi.
Lakini pasi
ipi ni bora kwa mwenzake katika kipindi gani. Lakini hiyo haitoshi, wakati
wanashambuliwa kutokana na namba yake, akae wapi. Au kama ni beki anapokuwa
amebaki pekee na mshambuliaji, ili kuwa na uhakika miguu yake inatakiwa kuwa
vipi.
Kuna mbinu
nyingi sana lakini si rahisi Logarusic au Pluijm kuzifundisha leo akiwa Simba
au Yanga. Hawa wachezaji walitakiwa kufundishwa wakiwa katika shule za soka
maarufu kama academy. Viwango vitakuwa bora pale tu wakiwa wamepata mafunzo
hayo ya awali.
Kweli
inawezekana tukakubali kuwa tumekosea na wachezaji wengi tulionao viwango vyao
vinategemea zaidi vipaji binafsi na si mafunzo ya utotoni. Je, sasa tunafanya
nini ili kubadilisha? Yanga, Simba na klabu nyingine zina shule bora kwa ajili
ya vijana.
Hakuna
ubishi Azam FC katika hili la kukuza vijana wanajitahidi, achana na Yanga na
Simba ambao ‘wanaokoteza’ vijana au kuwakusanya kila wanapoona michuano fulani
imekaribia na wengi wao wanalalamika hawana matunzo na hasa linapofikia suala
la malipo.
Kuna namna
ya kufanya, kama hadi sasa 2014 tumechelewa, kweli ni kosa. Lakini si sahihi
kuendelea kukubali kufanya kosa zaidi kwa kuendelea kuchelewa. Maana yake huu
ndiyo wakati mwafaka wa kubadili suala hilo.
Kulisahihisha
au kulibadili, basi ni lazima tuwe na vijana wanaopata mafunzo bora, si bora
mafunzo. Hao ndiyo watakaokuja kuwa tegemeo la klabu na Tanzania kwa jumla na
inawezekana pia makocha watakaokuja baadaye, kamwe hawatalalamika.
Leo Pluijm
na Loga kwa kuwa ni Wazungu angalau wameweza kufungua midomo yao na kusema
ukweli. Msiotaka kuambiwa ukweli mtawachukia, lakini jiulizeni kwa nini makocha
hao ingawa kila mmoja kwa wakati wake lakini wamelalamika kuhusiana na kitu
kinachofanana.
Kusikiliza
na kukubali au kukataa ni hatua moja, lakini hatua muhimu zaidi ni kufanyika
kwa utafakari. Soka sasa linaendana na mafunzo kuanzia utotoni na si kuamini
vipaji kama nilivyoeleza hivi karibuni. Msizibe masikio, zitumieni kauli za
Pluijm na Loga kama kinga ya kuepusha kuwa na wachezaji wasio na mafunzo hapo
baadaye, inawezekana.
0 COMMENTS:
Post a Comment