Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu
wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo mmoja inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka
huu katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja.
Timu itakayoongoza katika kila kituo
cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2 mwaka huu ndiyo itakayopata tiketi ya
kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu ujao wa 2014/2015. Vituo hivyo ni
Mbeya, Morogoro na Shinyanga.
Kituo cha Morogoro ambapo mechi
zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu za Abajalo FC ya Dar es Salaam,
African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya
United (Pwani), Mji Mkuu FC (Dodoma) Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC
(Dar es Salaam) na Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja wa Sokoine ndiyo utakaotumika
katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC ya Arusha, Magereza FC (Iringa),
Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji FC (Njombe), Panone FC (Kilimanjaro),
Tanzanite SC (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC
(Morogoro).
Timu za Eleven Stars ya Kagera, Geita
Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC (Mara), Mbao FC (Mwanza), Milambo SC
(Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma), Simiyu United (Simiyu), Singida United
(Singida) na Wenda FC (Mbeya) zitacheza katika kituo cha Shinyanga kwenye
Uwanja wa Kambarage.
Orodha ya usajili wa wachezaji wa
timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na
klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa ajili ya kipindi cha
pingamizi ambacho kinamalizika Mei 4 mwaka huu.
Hata hivyo, katika usajili
uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa kuna wachezaji walioshiriki
VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi msimu wa 2013/2014.
Kiongozi yeyote atakayebainika katika
udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa klabu au chama cha mpira wa miguu cha
mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni ikiwemo kufikishwa katika vyombo
vya kimaadili vya TFF kwa hatua zaidi.
Ligi ya Mabingwa haina mdhamini,
hivyo timu shiriki zitajitegemea kwa kila kitu, na zinakumbushwa kuwahi
vituoni.
0 COMMENTS:
Post a Comment