KIDO (KUSHOTO) AKIWA KATIKA MAZOEZI YA COASTAL NA KOCHA WA TIMU HIYO, YUSUPH CHIPPO |
Ofisa Habari wa Coastal Union ametengaza kuazhia ngazi katika klabu hiyo ya Tanga ambayo imekumbwa na migogoro kutokana na mashabiki na wanachama kuupinga uongozi.
Kido ametuma ujumbe ndani ya SALEHJEMBE, yafuatayo ni maneno kutoka katika mkono wake:
MIMI Hafidh Athumani
Kido, nikiwa na akili timamu natangaza kutojihusisha na shughuli zote za
Coastal Union, hasa usemaji wa klabu.
Miongoni mwa sababu
nyingi zilizonifanya kutangaza uamuzi huo ni sintofahamu iliyozuka ndani ya
klabu yetu, kwa taaluma yangu ya uandishi wa habari lazima niwe na msimamo juu
ya mambo yanayoendelea kwenye jamii.
Ili niendelee kufanya
kazi na klabu hii kwa wakati huu wa misuguano, lazima niwe na upande; kwa maana
upande unaounga mkono uongozi ama upande usiokuwa na Imani na uongozi. Lakini
mimi nimeamua kutounga mkono upande wowote.
Kwa hivyo basi, ili niwe
katika mstari sahihi nimeamua kukaa pembeni nifanye shughuli zangu za
uanahabari kwa furaha na amani.
Kwa kipindi kirefu
nimekuwa nikijaribu kuzima habari za uzushi na kuisimamia klabu isiyumbishwe na
mijadala ya hovyo, lakini kutokana na kuwa mbali na klabu, na ama kutopewa
taarifa sahihi hata ninapoziuliza kwa viongozi; nimeona si wakati salama wa
kukuza uwezo wangu wa kiusemaji hasa ikizingatiwa bado ni kijana na sihitaji
kuharibu hadhi yangu.
Bado ni mwanachama halali
wa Coastal Union Sports Club, namba yangu ya kadi ni 0013. Nitaendelea kutoa
ushauri na kuishabikia klabu yangu ambayo nimekuwa nikimuona marehemu baba
yangu na kaka zangu wakiishabikia tangu nikiwa mdogo.
Kadhia kubwa ni kuhusu
uhalali wa Nassor Ahmed Binslum, kuwa ni mfadhili ama mtu tu aliekuwa
akiinyonya klabu yetu kupitia kampuni yake ya matairi na betrii (Binslum Tyres
Company Limited).
Kwa hilo nasema wazi bila
kupepesa macho, kuwa Nassor Binslum ndie alienishawishi kuwa msemaji wa klabu
baada ya aliekuwa msemaji Edo Kumwembe, kujiengua kutokana na sababu za
kutingwa na majukumu ya kiuandishi.
Binslum, huyohuyo ndie
aliefanikisha kununua kamera inayotumika kuendesha shughuli za klabu, ndie alieninunulia
kompyuta mpakato (Laptop), ninayoitumia kwa shughuli za klabu, mtu mmoja
huyohuyo ndie aliekuwa akinifadhili katika safari za klabu kama pesa za nauli
na chakula.
Binslum huyohuyo, ndie
aliefadhili kuanzishwa kwa blogu ya klabu ambayo amekuwa akiifuatilia kila siku
na hata marekebisho madogomadoo yeye ndie anaeyasimamia kwa kutoa fedha.
Binslum huyohuyo aliekuwa
hafai ndie alieshinikiza niwemo kwenye ziara ya Oman, timu ilipoweka kambi kwa
wiki mbili. Kwani viongozi walio madarakani hawakuona umuhimu wangu wakaamua
kukata jina langu mpaka siku moja kabla ya pasi za kusafiria kupelekwa ubalozini.
Binslum, alinipigia simu
saa kumi alasiri akinitaka kupeleka pasi yangu ya kusafiria kwa meneja wa timu
ambae hakutaka kupokea simu yangu kila nilipompigia, na hata nilipompigia
mwenyekiti wa klabu akaahidi atawasiliana na meneja wa timu lakini mpaka jua
linazama hakukuwa na msaada wowote niliopewa, nikaamua kufanya kitendo cha
hatari kwa kuenda kuiwacha pasi yangu ya kusafiria kwa muhudumu wa hoteli
aliyofikia meneja hapa jijini.
Lakini hata alipoipata
asubuhi yake pia hakuniarifu kuwa ameipata yaani mpaka siku ya safari sikuwa na
uhakika kama nilikuwa miongoni mwa wasafiri ama la. Kwa kifupi nilikuwa
nikichezwa shere.
Kwa hivyo basi ikiwa
Binslum, hatakiwi na klabu nitakuwa mnafiki kuendelea kubaki kwasababu nitakuwa
sawa na mnyama ninaetia ulimi puani.
Mtashangaa nimetangaza
uamuzi huu wa kuachia ngazi bila kusema kuwa nimeandika barua ama la, kifupi
sina mkataba wala taarifa yoyote ya kimaandishi juu ya kuajiriwa kwangu na
klabu. Hivyo nimeamua kujiuzulu kienyeji kama nilivyoitwa kienyeji.
0 COMMENTS:
Post a Comment