SOKA la England limekuwa likidaiwa kwamba halina burudani ya
kutosha kwa kuwa kila timu imekuwa ikicheza mpira wa Kiingereza ambao ni pasi ndefundefu
tu.
Pasi ndefu zaidi zinalenga kutafuta bao la haraka, tofauti na urembo
ambao pia unawavutia wengi hasa timu inapopiga pasi nyingi na za uhakika.
Arsenal ni sehemu ya burudani na kocha Arsene Wenger ni kati ya
wanaopaswa kupewa pongezi kutokana na mabadiliko makubwa aliyoyafanya.
Soka la England sasa linavutia, ziko timu zinazopiga pasi nyingi,
kwa kasi na zinavutia kuangalia kwa kuwa ushindani pia ni wa juu.
Lakini hauwezi kupata timu inayopiga pasi nyingi bila ya kuwa na
wataalamu wanaopiga pasi zenye macho, unaweza kusema wenye miguu yenye macho.
Pasi wanazopiga zinafika, wakipoteza ni chache. Mfano mzuri wa
ubora wa suala hilo unaweza kuuchukulia kwa Yaya Toure wa Manchester City.
Mwafrika huyo alikuwa bora zaidi katika msimu uliomalizika jana wa
Ligi Kuu England maarufu kama Premiership.
Kweli alionyesha uwezo wa juu na ndiye mchezaji aliyepiga pasi
nyingi zenye macho bila ya kujali zilizaa bao au zilianzisha mipango ya bao.
Lakini wapo wengine walijitutumua kama mkongwe Steven Gerrard,
David Silva, Wayne Rooney na wengine.
Mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi lazima awe anajiamini, fundi na
anayejua analolifanya. Waliofanya hivyo wanaonyesha ni wachezaji wa madaraja ya
juu.
Toure:
Katika mechi 38 za Premiership, amepiga mechi 35 ikiwemo ya jana ambayo imeipa Man City ubingwa wa pili ndani ya miaka mitatu.
Maana yake alikuwa kiungo muhimu cha Manchester City hadi kufikia mafanikio.
Utaona mechi chache tu alizokosekana, kila kitu kilikuwa wazi
kwamba ‘mtu mzima’ hakuwepo na mambo hayakwenda sahihi zaidi.
Ndiye kiungo aliyefunga mabao mengi zaidi, katupia 20 kabla ya
mechi ya jana ambayo ilikuwa ni fainali.
Wastani wake wa pasi ni 70.1 ambao ndiyo wa juu zaidi kuliko wa
kiungo, beki au mshambuliaji yeyote aliyecheza Premiership katika msimu wa
2013-14 uliomalizika jana.
Toure ni Mwafrika kutokea Ivory Coast, huenda sifa yake anayopata
England isiwe kama anayopata Gerrard au Rooney, kama kwa kasi msimu huu
amewapoteza.
Kwanza ameichezesha timu, ndiyo maana unaona amepiga pasi nyingi
zaidi kuliko mchezaji mwingine kwenye ligi hiyo.
Lakini ndiye kiungo aliyefunga mabao mengi zaidi kuliko mwingine
yeyote England katika msimu huo ulioisha jana na timu imepata mafanikio ya juu.
Pia Toure ameonyesha uwezo mkubwa wa mabao ya ‘mipira iliyokufa’
kama moja alilomfunga Juma Kaseja wakati Ivory Coast ilipoivaa Tanzania kuwania
kwenda Kombe la Dunia. Wengi wakasema Kaseja ni mzembe, lakini walipoa baada ya
kuona mabao yake mengine kama hayo, akiwa England.
Achana na mabao ya faulo, katika mechi dhidi ya Aston Villa, Toure
alifunga moja ya mabao bora ya msimu baada ya kutoka na mpira katikati ya
uwanja na kufunga, ndilo lilikuwa bao la 100 msimu huu kwa Man City.
Hakuna ubishi, Toure ndiye alikuwa bora zaidi msimu huu kwa kuwa
alijumuisha mambo mengi na yote akayafanya kwa ubora wa juu zaidi.
Silva:
Ukifuatilia mechi za Manchester City alikuwa kama hayupo, lakini
ukweli ni kati ya wapishi wakubwa na walioifanya timu hiyo kuwa tishio kwa
msimu mzima.
Anatokea Hispania, hivyo suala la pasi si kitu kigeni sana kwake, ‘makofi
polisi’ ndiyo nyumbani. Silva amemaliza ligi na wastani wa pasi 68.7, unaweza
kusema pasi 69 kwa mechi, anafuatia baada ya Toure.
Ramsey:
Ndiye kiungo aliyeanza msimu vizuri zaidi akiwa na Arsenal lakini
katikati mwa ligi akakumbana na bahati mbaya ya majeraha. Lakini utaona bado
amemaliza na wastani wa juu wa pasi 66.4 kwa mechi.
Wastani huo wa juu ni katika mechi 19, kabla ya mechi ya jana.
Maana yake kama asingeumia, hakika ndiye angekuwa mpinzani namba moja wa Yaya
Toure ambaye ‘ametisha’ zaidi.
Gerrard:
Mechi 32 ameonyesha ndiye mchezaji mkongwe kwenye kiungo
aliyefanya vizuri, kaiongoza Liverpool vema zaidi. Usiangalie ana ubingwa au
la, lakini kadiri alivyokuwa anazeeka, ndivyo kiwango chake kimekuwa juu zaidi.
Katika mechi hizo, Gerrard amepata wastani wa kupiga pasi 64.5 kwa
kila mechi ambao bado ni wa juu.
Lovren:
Dejan Lovren amechangia mabadiliko ya Southampton katika kiungo
ingawa mwishoni mwa ligi ilianza kuonekana kama vile ni nguvu ya soda.
Lakini katika mechi zake 30, amekuwa na wastani wa pasi 51.
Pia alikuwa na uwezo na juhudi ya juu katika ukabaji, tayari soko
lake liko juu, huenda akapata timu kubwa zaidi ndani au nje ya England.
Rooney:
Man United ilikuwa haina nguvu sana msimu huu, kila mechi
ilipambana kujing’oa katika nafasi ya saba.
Lakini Wayne Rooney aliyecheza mechi 27 tu kabla ya jana,
aliendelea kuonyesha ni mmoja wa wachezaji bora kutokea katika Premiership,
alionyesha uwezo wa juu utadhani Man United haikuwa pabaya. Amemaliza msimu
akiwa na wastani wa pasi 46 kwa mechi ambao si mbaya.
Hazard:
Eden Hazard aliuanza msimu vizuri sana, lakini mechi kumi za
mwisho alionekana kutokuwa msaada sana kwa Chelsea ambayo iliteleza karibu kila mechi hadi kujiondoa kwenye
mbio za ubingwa.
Kabla ya jana alicheza mechi 31, amefanikiwa kupata wastani wa
pasi 44 katika mechi moja ambayo inaonyesha pia alistahili kuwa mchezaji bora
wa PFA kwa vijana, tuzo ambayo inathaminiwa sana England na kila mmoja
anatamani kuipata.
Cabaye:
Aliondoka England kwenda kujiunga na PSG ya kwao Ufaransa baada ya
kuwa ameichezea Newcastle mechi 17, mbili akiwa ameingia. Lakini ameacha
wastani wa mechi 49 ambao ni wa juu.
Maana yake mashabiki wana haki ya kusema kuondoka kwake
kulichangia kudorora kwao, ndiyo maana walimtaka kocha Alan Pardew aombe radhi
kwa suala hilo.
0 COMMENTS:
Post a Comment