KAMA kawaida, mheshimiwa Ismail Aden Rage
alianza uongozi wa Simba na ujanja mwingi, amemaliza hivyohivyo, ujanjaujanja
tu.
Mambo yanaweza kuwa mengi, lakini mawili tu
yanaweza kutosha kudhibitisha namna ambavyo mambo mengi hayakuwa sawasawa ndani
ya Simba, nitayataja.
Haya yametokea wakati wa uongozi uliopita wa
Klabu ya Simba chini ya Rage, ulipokuwa ukikabidhi ofisi kwa ule mpya chini ya
Rais Evans Elieza Aveva ambaye sasa ana jukumu la miaka minne kuiongoza Simba
na kuirudishia heshima yake.
Kazi ya Aveva haitakuwa rahisi na lazima
Wanasimba kama kweli wanaipenda klabu yao, wakubali kumsaidia, naye awe tayari
kupokea misaada hata kama itakuwa ya ushauri. Kipindi cha Rage, Simba imevurugwa
sana.
Tukirudi kwenye suala la makabidhiano, Rage
alikabidhi vitu wazi huku akivitaja, lakini ajabu suala la kwanza alipoanza
kuonyesha kuna walakini ni aliposhindwa kutaja Simba imebaki na kiasi gani cha
fedha benki!
Rage hakusema, aliwaeleza waandishi wa habari
kwamba ilikuwa ni siri kubwa kwa kuwa hata pale alipokuwa anazungumza nao
wengine ni Yanga. Hivyo ni silaha ya klabu hiyo kuficha walichokuwa nacho.
Maneno hayo yanaonyesha kupitwa na wakati,
wale ambao mnakumbuka wakati wa uchaguzi uliomuingiza Rage madarakani,
nilijitokeza mapema na kueleza msimchague Rage kwa kuwa ataifanya Simba kwenda
mwendo wa kizamani, uliojaa migogoro kama ule wa wakati wa Chama cha Soka
Tanzania (Fat) kilichokuwa kinaongoza kwa migogoro kuliko kingine chochote.
Huenda mliamini mimi ni mbaya, nina nia
mbaya, najua mkanivika ubaya, sasa ni wakati wa kupima ukweli. Mara zote
ninahoji, wako wapi waliokuwa wapambe wa Rage waliopinga kila nilichosema?
Kuficha kiasi cha fedha walichonacho Simba ni
kubabaisha mambo kwa kuwa wanachama wanatakiwa kujua klabu yao ina kiasi gani
na hilo litawekwa wazi tu wakati mahesabu yatakapotakiwa kukabidhiwa kwa
wanachama.
Wanachama wa Simba hawawezi kufanya mkutano
wa siri, maana yake taarifa hizo zitamfikia kila mtu. Kuficha una kiasi gani
ndiyo silaha kwa adui? Kichekesho.
Aveva kakubali kupokea zawadi ya mbuzi aliye
kwenye gunia, lazima yeye atakuwa anajua kiasi gani kilichopo kwenye akaunti za
Simba. Vizuri akaweka wazi kwa kuwa taasisi zinazohusu wanachama, kwa kawaida
ni vizuri kuweka hadharani mahesabu yao kila baada ya miezi mitatu. Hii
itasaidia wanachama hao kujua mwenendo wa klabu.
Kuficha maana yake kuna tatizo, Simba ikiwa
na fedha nyingi hakiwezi kuwa chanzo cha kuangushwa na kama ingekuwa na fedha
nyingi, vipi Rage aliondoka bila ya kuwalipa wachezaji lukuki mishahara yao
hadi uongozi wa Aveva ulipofanya hivyo wiki iliyopita? Siri maana yake ni
kuficha madudu!
Mimi siamini kama wanachama hawawezi
kujifunza katika mambo kama haya ambayo hawahitaji nguvu hata kidogo kutafakari
na kung’amua kuwa Rage alitumia nguvu nyingi kuficha suala la mahesabu kwenye
mikutano ya wanachama na sasa amekataa kutaja, maana yake kuna tatizo kubwa.
Mwisho nauliza na ninasisitiza kama ambavyo
nimekuwa nikihoji awali, ziko wapi fedha dola 300,000 (Sh milioni 480) za mauzo
ya Mganda, Emmanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia?
Wale waliosema zitalipwa, wengine wakashiriki
kumuandikia Rage makala dhidi yangu iliyojaa blah-blah kibao, kwamba nilikuwa
ninahisi kitu ambacho si sahihi, lazima zitalipwa kwa wakati, ziko wapi hizo
fedha sasa? Mwisho Simba imeambulia karatasi, barua eti Fifa inatambua kesi.
Upuuzi mtupu!
Aveva amekabidhiwa deni, tena kwa mara
nyingine Rage akizua jambo jipya ambalo halina hoja hata chembe, eti Okwi
alikuwa mchezaji huru, Simba ikawahi kumuongezea mkataba, ndiyo maana nimekuwa
nikisisitiza Mganda huyo aliuzwa bure. Hoja ya msingi hapa, fedha ziko wapi?
Simba ilimuongezea mkataba, ikatoa dola
40,000 (Sh milioni 64), halafu ikaenda kumgawa bure, yenyewe ikaambulia ‘ziro’
na aliyesababisha yote hayo ni Rage kwa kuwa alikuwa ana haraka na kulazimisha
uhamisho hata kabla Waarabu hao hawajatoa fedha.
Wajumbe wa kamati ya utendaji wakati huo
walieleza wazi kuwa Rage alifanya maamuzi kivyake.
Sasa Simba imepoteza fedha ilizompa Okwi,
imepoteza nauli na matumizi ya watu waliosafiri kwenda Tunisia kushughulikia
suala hilo, fedha kwa ajili ya kesi ya Okwi Fifa na kuna dalili zote mzigo
aliopewa Aveva kwa kuwa kakabidhiwa deni utakuwa mkubwa kwake na kupoteza muda
tu.
Nilimsikia Rage akisema eti Etoile du Sahel
wameshindwa kulipa fedha hizo kwa kuwa kuna matatizo katika Serikali ya Tunisia
katika suala la uhamishaji fedha. Jiulize Etoile hawafanyi biashara kwa sasa,
mbona tunasikia wanasajili wachezaji kutoka Afrika Magharibi?
Wakati Rage akiwa Fat alikuwa akisema
anavyojisikia, anaeleza maneno yasiyo sahihi akitumia vipengele vya katiba ya
Fifa na watu wakaamini.
Sasa mambo yamebadilika, watu wanajisomea
mambo, wanaelewa na hakuna tena nafasi ya kudanganya! Ndiyo maana unaona ni
rahisi kujua uozo na blah-blah kwa urahisi.
Rage hakupaswa kumkabidhi Aveva deni
lililotokana na uzembe wake, ilitakiwa fedha. Aliahidi fedha hizo angezipata
kabla ya kuondoka, nikasema haitawezekana, leo amekabidhi maneno matupu na
amethibitisha nilichokieleza, nasisitiza Simba haikustahili kumuuza Okwi bure
halafu ikaendelea kupoteza fedha eti inashughulikia.
Kama Rage angekuwa makini mwanzoni, basi haya
yasingetokea. Kulazimisha kwake mambo, sijui kwa nini ndiyo kumekuwa chanzo cha
haya! Aveva ajifunze, ikiwezekana na Rage awaombe radhi Wanasimba kwamba hakuwa
sahihi na ameharibu mambo.
Nina hoja za msingi kumhoji Rage bila kujali
ninaowaudhi kwa kuwa ni rafiki au wapambe, ukweli ndiyo huo Simba ili ibadilike
lazima isiende mwendo wa aliokuwa nao Rage, la sivyo kufeli kutakuwa ndiyo
njia.
0 COMMENTS:
Post a Comment