Na Saleh Ally
WABRAZILI wanne ambao wameajiriwa na Klabu
ya Yanga, ndiyo wamekuwa gumzo hali inayofanya mashabiki wa soka kutamani
kuanza mapema kwa Ligi Kuu Bara ambayo imesogezwa hadi Septemba 20, mwaka huu.
Yanga imeamua kuajiri Wabrazili wanne,
wawili wakiwa ni wachezaji ambao ni Geilson Santos maarufu kama Jaja, Andrey
Coutinho halafu makocha ni Marcio Maximo ambaye ni bosi na msaidizi wake,
Leonardo Neiva.
Uongozi wa Yanga umeamua kuboresha benchi
lake la ufundi kwa kuleta makocha hao Wabrazili, lakini bado ukatoa nafasi kwa
wao kuchagua wachezaji wawili ambao wanaamini watakuwa msaada kwao.
Yanga isingekuwa na uwezo wa kuwapa nafasi
Maximo na Neiva kuchagua wachezaji kiwango cha wale wanaocheza Ligi Kuu Ufaransa
kwa kuwa gharama zao ni juu sana.
Lakini bado inabaki palepale, Coutinho na
Jaja ni wachezaji kutoka nje ya Tanzania, hivyo wanategemewa kuonyesha kitu
tofauti ambacho kitakuwa changamoto.
Kuna mambo kadhaa ya kuangalia kuhusiana na
wachezaji hao, lakini kwanza ni lazima kuutoa nje uongozi wa Yanga kwa kuwa
usajili uliofanyika ni pendekezo la Kocha Maximo.
Suala la ujio wa Coutinho, Jaja na kupokewa
kwao, hizo tayari ni historia na sasa kinachoangaliwa ni kuhusiana na suala la
wataonyesha uwezo kiasi gani, msaada wao kwa Yanga na changamoto kwa soka ya
Tanzania.
Miguu, macho, kichwa ndivyo vinatakiwa
kuzungumza. Wabrazili hao hawatakiwi kuwa na maneno au visingizio vingi, badala
yake waonyeshe kile ambacho kimewaleta hapa nchini.
Wakiisaidia Yanga kufanya vizuri, watakuwa
wameisaidia soka ya Tanzania kwa kuwa matarajio ya wengi ni kwamba mchezo wa
soka uko juu nchini kwao. Hata kama Brazil ilifungwa mabao 7-1 na Ujerumani
katika Kombe la Dunia, si rahisi kuwafananisha na kiwango chetu.
Bado hawawezi kuwa malaika, kwamba kila
watakachokuwa wanafanya kitakuwa ni zaidi ya kile ambacho kimekuwa kikifanyika
hapa nyumbani. Wanayo changamoto.
Pamoja na changamoto ambayo wataipata
kuonyesha walichonacho, mambo kadhaa ya msingi kwao na kwa wazalendo, ndiyo
yapewe nafasi.
Uwezo:
Coutinho na Jaja lazima waonyeshe uwezo,
raha ya mpira hauchezwi kwenye uwanja wenye minazi kwamba kuna mtu anaweza
kujificha. Kila kitu hadharani, kama wanaweza, kila kitu kitaonekana waziwazi.
Kuwapa muda si jambo baya, angalau nusu
msimu, lakini zaidi ya hapo, hakutakuwa na sababu ya kuendelea kubaki nao kama
watakuwa wanacheza samba lisilokuwa na msaada badala yake lile ambalo
linaburudisha watu bila Yanga kupata mafanikio.
Deni lao ni kuonyesha uwezo wao ambao ni
msaada kwa Yanga, zaidi ya hapo mengine yatakuwa ni hadithi tu.
Kuzidisha:
Wao ni binadamu, wanaweza kukosea, wanaweza
kufanya vibaya, hivyo mashabiki wa Yanga wana kila sababu ya kuamini hawawezi
kufanya kizuri kila siku.
Hawatakuwa na vizisingizio watakapoharibu,
lakini kuzidisha imani kwamba wao ni Wabrazili, hivyo watacheza kama alivyo
Neymar au Oscar itakuwa ni makosa.
Kuna wachezaji wengi hapa nyumbani hawana
uwezo kama wa Mrisho Ngassa au Ramadhani Singano ‘Messi’. Hivyo hilo
linawezekana kwa Wabrazili hao pia, ndiyo maana wamekuja kucheza Tanzania.
Wivu:
Suala la wivu ni maumbile ya binadamu,
kulikwepa asilimia mia si rahisi hata kidogo. Hivyo wachezaji wa Yanga wanaweza
kuwa na wivu dhidi ya wachezaji hao.
Ikitokea kuna wale ambao wanawanyima
ushirikiano hata kama kimyakimya kwa hofu kwamba wao watatamba, basi wajue
watakuwa wanajiangusha wao na Yanga.
Ndiyo, inawezekana kujiangusha wao kwa kuwa
wakifeli Wabrazili hao, itakuwa imefeli Yanga na mchezaji aliyewabania naye
atakuwa amefeli. Kila mtu ana nyota yake, kusaidiana kwenye timu ni kuisaidia
timu na kujisaidia mwenyewe, hivyo waamini ushirikiano kwa wageni hao ni jambo
la kwanza kabisa.










0 COMMENTS:
Post a Comment