KATI ya vipindi vya michezo redioni ambavyo hunipita kwa
nadra sana ni kile cha Radio One Stereo. Siku chache zilizopita, nilikuwa
nikifuatilia namna Maulid Kitenge alivyokuwa akimhoji Katibu Mkuu wa Chama cha
Riadha Tanzania (RT), Selemani Mujaya Nyambui.
Kitenge alikuwa akitaka kujua sababu ya timu ya Tanzania
iliyoshiriki michuano ya Jumuiya ya Madola kurejea nyumbani bila ya hata
kipande cha medali.
Nyambui ambaye katika sauti yake unaweza kubaini mengi,
alizungumza mambo ya ajabu ambayo hauwezi kutarajia kiongozi au mwanamichezo
mwenye sifa yake anaweza kuzungumzia.
Mwanariadha huyo wa zamani ambaye unaweza kumwita ni kati ya
mashujaa waliowahi kuchukua medali na kuileta nyumbani kupitia michuano ya
Olimpiki, alikuwa akizungumza sawa na mtu aliyekuwa hayuko vizuri, labda kwa
uchovu au ni yule asiyejali tu.
Wakati Kitenge akieleza alitaka kujua kwa nini timu hiyo
haikuleta medali, Nyambui hakufafanua lolote zaidi ya kuhoji vipi Taifa Stars
nayo mbona imefungwa na Msumbiji na kurejea nyumbani mikono mitupu!
Hata aliposisitiziwa kwamba suala la soka halimhusu na
alipaswa kujibu lile linalomhusu, akasema anashangazwa na watu kuhoji medali
wakati hawajui hata muda mzuri waliokimbia wanariadha waliokwenda Glasgow,
Scotland na hicho ndiyo kitu cha kujivunia.
Huyo ni mwanariadha nyota wa zamani wa nchini, kiongozi wa
sasa wa mchezo wa riadha ambaye anadiriki kuzungumza pumba tena akionyesha
hajali na badala ya kufafanua anachoelezwa, yeye anakwenda kuhoji vipi wengine
pia wamefanya vibaya!
Majibu ya Nyambui yanathibitisha kwamba mafanikio katika
mchezo wa riadha sasa ni ndoto, labda hadi mambo mawili yatokee.
Kwanza Nyambui aondoke kwenye uongozi wa mchezo huo au soka
warudi na kombe nyumbani baada ya kushinda nje, basi Nyambui ataongeza juhudi
kuwajibu.
Anachokisema anaonyesha hajali kwa kuwa soka hawajashinda,
wangeshinda huenda angesikia wivu. Lakini kwa anachozungumza, inaonyesha wazi
kiongozi huyo ni sehemu kubwa ya tatizo katika mchezo wa riadha.
Sijui wangapi walimsikiliza Nyambui, lakini kwa waliopata
nafasi ya kumsikiliza ‘live’ sijui walitafakari vipi lakini mimi naweka wazi
hisia zangu kwamba ingawa ni mwanariadha wa zamani, anaonyesha kiasi gani
asivyo na uchungu na Tanzania kutofanya vizuri.
Huu ndiyo wakati mzuri na mwafaka wa wanamichezo au Watanzania
kwa jumla kuanza kuhoji na kuwakemea watu kama akina Nyambui ambao wamejisahau
na kugeuza vyama vya riadha kama mali yao huku wakiamini hakuna mtu anayeweza
kuwahoji kutokana na kinachotokea.
Lazima tujue kwamba kizuri na kibaya, kinahusisha jina la
nchi yetu Tanzania.
Tusiruhusu watu kama kina Nyambui wakaendelea kuzaliwa
wengine ambao watakuwa kila kitu wanakichukulia kwa urahisi huku wakiona vyama
wanavyoviongoza utafikiri ni mangi anayemiliki duka, hivyo wanaweza kuamua muda
wa kufunga na kufungua.
Tunajua mamilioni ya fedha yamekuwa yakitolewa na
mashirikisho ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya michuano mbalimbali ya
kimataifa ambayo mwisho wake hatufanyi vizuri.
Kama hiyo haitoshi, safari hii serikali kupitia Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ilitumia fedha za kodi
ya Watanzania kwa ajili ya maandalizi ya timu hiyo ya Jumuiya ya Madola.
Sasa kuzungumza kama vile unazungumzia familia yako, bila ya
kujua Watanzania wengine wanaumia vipi, si kitu sahihi.
Leo nakutumia salamu hizi Nyambui lakini nakuasa, kuna haja
ya kuonyesha kiasi gani una uchungu na taifa lako na si kufurahia tu kusafiri
na kulala kwenye hoteli nzuri halafu mnarudi mikono mitupu na maneno mengi ya
kujidai yasiyokuwa na ustaarabu au kuonyesha upevu. Inaonyesha huwa mnajua
mtarudi hamna kitu!
0 COMMENTS:
Post a Comment