August 15, 2014

PHIRI AKIWA NA MSAIDIZI WAKE NA ALIYEKUWA NAHODHA WAKATI AKICHEZA, SELEMANI MATOLA. HAPA ILIKUWA NDIYO WAMEKUTANA KWA MARA YA KWANZA BAADA YA PHIRI KUWASILI TENA NCHINI KUANZA KUINOA SIMBA.


Na Saleh Ally
KOCHA mpya wa Simba, Patrick Phiri amesema ameamua kuja kukinoa kikosi hicho huku akiamini kikubwa kilichomleta hapa nchini ni mapenzi.

Phiri raia wa Zambia kwa mara ya kwanza amefanya mahojiano mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa Simba na kusema urafiki wake na watu wengi waliopo Simba, umemfanya aache ofa kubwa zaidi.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Phiri amesema Shirikisho la Soka la Namibia (NFA) ndiyo lilikuwa la kwanza kufanya naye mawasiliano kwa ajili ya kukinoa kikosi cha timu hiyo.


“Wakati Simba wananipigia simu, tayari Namibia walikuwa wamenitumia tiketi ya ndege kwenda Windhoek kwa ajili ya mazungumzo. Viongozi walisafiri na timu na wakaniambia ndani ya siku chache watakuwa wamerejea, hivyo nisafiri watanikuta huko ili tumalizie na kusaini mkataba.

“Wakati najiandaa, Simba walianza mazungumzo na mimi baada ya kunipigia simu. Kweli lilikuwa ni jambo la kuchanganya kwangu kwa kuwa imekuwa ni vigumu sana kusema hapana kila ninaposikia ni Simba ndiyo wananihitaji.

“Nina mapenzi ya juu sana na Simba kwa kuwa najua watu wa hapa (Simba) wananipenda, wananiheshimu na kunijali. Hivyo nikachanganyikiwa, sikujua hasa sahihi ni kipi ingawa kama ni maslahi, Namibia yatakuwa juu.


“Mwisho mapenzi yangu kwa Simba ndiyo yalinifanya kuchukua uamuzi huu, nikasema nitakuja Dar es Salaam kuwasilikiza,” anasema Phiri ambaye mara zote ni mtaratibu huku akisisitiza amefurahishwa zaidi kukuta watu wengi aliowaacha wakiwepo Simba, kitu kinamfanya aamini hajakosea kuweka mapenzi yake kwa klabu hiyo inayotumia rangi nyekundu na nyeupe.

Kazi:
Nitaanza kazi rasmi nikiwa Zanzibar ingawa hapa (Dar es Salaam) ninaweza kuwaona vijana kwa ajili ya kuwasalimia na kuwaona namna walivyoanza kufanya kazi. Najua mambo yatakuwa yanakwenda vizuri na nitakutana na kushirikiana na watu wengi ninaowafahamu.

Matola & Nyagawa:
Matola na Nyagawa wote walikuwa nahodha katika kikosi changu ingawa ni kwa wakati tofauti. Sasa wao ni kocha msaidizi na meneja. Ninaamini hawa ni wanangu pia ninafurahi kuwakuta bado wakiwa Simba na hii inaonyesha mapenzi yao makubwa kwa klabu hii kama ilivyo kwangu.

Mapenzi ni silaha kubwa kwa unachokifanya. Ninaamini kabisa kuwa na watu wanaoipenda kazi yao na kampuni wanayoitumikia, basi itasaidia kupatikana kwa maendeleo ambayo mnayatarajia.

Kufanikiwa lazima ufanye kazi bila ya kuchoka, ukiamini kuwa mafanikio yanakuja baadaye. Ukiwa unakipenda kitu fulani, huwezi kuchoka hadi mafanikio yapatikane.

Mafanikio:
Kama nilivyosema awali, ninahitaji muda ingawa ninajiamini kabisa mambo yatakuwa mazuri. Kwangu ingawa si mgeni hapa Simba, kikazi itakuwa ni mgeni. Nimeambiwa kuna wachezaji wengi wageni na wachache ambao nilifanya nao kazi.

Utamaduni wa Simba hauwezi kubadilika sana, najua kutakuwa na wachezaji wazuri ambao tukipata muda wa pamoja, tutatengeneza kikosi bora ambacho kitafanya vizuri.

Lakini lazima tukubali katika hili kuwa muda unahitajika, lazima kuwe na uvumilivu kidogo wakati nikiwaona wachezaji, wakati nabadilisha mifumo, halafu mafanikio yataanza kupatikana.

Phiri aliifundisha Simba kwa vipindi viwili tofauti (2003-05) na (2008-11) na vyote amechukua makombe tofauti yakiwemo mawili ya ubingwa Tanzania Bara. Mwaka 2005 alitwaa Kombe la Tusker. Huku akiwa na rekodi ya mmoja wa makocha wa Simba ambao walikuwa wakiitesa Yanga.

Wachezajii aliowahi kuwafundisha mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2011 alipoondoka ni Shabani Kisiga, Nassor Said ‘Chollo’ na Amri Kiemba ambao kwa mara nyingine atafanya nao kazi tena akiwa nao katika kikosi kimoja cha Simba.

Moja ya sifa ya Phiri ni soka la haraka-haraka na pasi fupifupi lakini kikosi ambacho kinacheza soka la nguvu bila kuchoka na wachezaji wengi ambao amekuwa akiwafundisha anawajenga kujiamini zaidi uwanjani.

Phiri aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Nkana pia timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ ambayo pia aliifundisha, ni kati ya makocha wenye heshima ya juu zaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Bara la Afrika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic