Na
Saleh Ally
TUMSUBIRI
nani ambaye atakuja kutuokoa na kuitoa timu yetu ya taifa hapa ilipo ili iweze
kusonga mbele hatimaye kupata nafasi ya kucheza michuano hii miwili mikubwa
duniani ambayo sasa karibu kila mmoja amecheza, sisi bado kwa zaidi ya miaka
30!
Nazungumzia
Kombe la Mataifa Afrika, ambalo mara ya kwanza na mwisho ilikuwa ni 1980 nchini
Nigeria na Kombe la Dunia ambalo Taifa Stars, haijawahi hata kuonyesha angalau
inakaribia kuvuka na kuingia huko.
Wakati
Taifa Stars inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza na mwisho, nilikuwa
nina umri wa mwaka mmoja na ushee. Sijui hata ilivyokuwa zaidi ya hadithi
ninazopewa, dalili zinaonyesha hata nikijaaliwa kufikisha miaka 50 au 60 au
zaidi, bado itaendelea kuwa hadithi.
Ninaamini
itakuwa hivyo kwa kuwa mfumo wa mwendo wetu umekuwa ni ule wa kupanda na
kushuka au nafuu inatangulia halafu mbaya zaidi inafuatia, hii ni hatari.
Siamini
kama Watanzania wote wana uchungu na Taifa Stars, kuonekana haina lolote, timu
nyanya inayoweza kufungwa na timu yoyote inayokutana nayo, iwe ni Msumbiji na
hata Burundi ambao wakikutana na sisi, sasa ndiyo wanyonge wao!
Angalau
wakati wa uongozi wa TFF, chini ta Leodegar Tenga kulikuwa na mabadiliko na
mwamko katika kikosi cha Taifa Stars, ambayo aliikomboa kutoka huko nyuma
kutoka Fat iliyokuwa chini ya akina Muhidin Ndolanga, Ismail Aden Rage na
Michael Wambura.
Sasa
tuko palepale, tumerudi kulekule kwa kuwa Taifa Stars yetu sasa ni zaidi ya
kichwa cha mwendawazimu na kila mmoja anaona anaweza kuwa kiongozi TFF na vibaya
zaidi, wengi hawapendi kuambiwa.
TFF
imejaza watu wengi ambao si sahihi, watu ambao wana sauti kubwa ndani ya
shirikisho hilo na wanaamini wanachofanya ni sawasawa.
Wachezaji
walio Stars pia naweza kusema hawajitumi, hawana moyo wa kizalendo na hakuna
anayeweza kuweka mezani sababu za msingi vipi timu yetu iwe inafungwa karibu na
kila timu.
Malawi
wanatupa shida, Msumbiji hatuwawezi, Burundi wanatuonea, nani sisi tunamuweza?
Vipi Tanzania ambayo kikosi chake sasa kina udhamini mkubwa na wachezaji
wanapata kila kitu wakilala kwenye hoteli nzuri lakini hawafanyi lolote.
Rais
wa TFF, Jamal Malinzi amekuta mambo mengi yamenyooka, kwa kuwa karibu wadhamini
wote waliingia wakati wa kipindi cha Tenga, yeye amefanya nini. Ndoto na ahadi
zake wakati anaingia madarakani vipi? Mbona sasa watu wanakuwa wakali hawataki
kuhojiwa.
Mnataka
tukae kimya, mfano mimi ambaye katika uhai wangu, nimeona Taifa Stars ikifungwa
mechi nyingi zaidi kuliko ilizoshinda! Natakiwa kuendelea kuvumilia au natakiwa
kuhoji?
Malinzi
ambaye alikuwa tumaini la wengi wakati alipozuiwa kugombewa na wengi
wakamlilia, nahoji vipi naye anaonekana hana tofauti kwa kuwa kila anachofanya
amefeli?
Wapambe
wengi ambao wanalazimika kila anachofanya kionekane ni kizuri kwa ajili ya
kumlipa fadhila kutokana na ushikaji wake kwao, ‘kawabeba’ wako kwenye nafasi
zisizostahili, hawataki wahojiwe.
Washauri,
wasiojua lolote, ambao hawakuwahi kuucheza mpira, kufundisha au kusomea uongozi
wa soka, ndiyo wanaoipeleka TFF huku inapokwenda. Lakini bado wanaona kuhoji
tunapokwenda ni jambo baya au kumuonea Malinzi! Sasa tunyamaze?
Nchi
ya namna gani hii ambayo ina watu wasiokereka na kufeli, wanaoona poa tu kwamba
kufeli ni mazoea yao na wako tayari kuendelea kufeli. Utaona sasa Taifa Stars
haina uhakika wa kucheza Kombe la Mataifa linalofuatia wala Kombe la Dunia
mwaka 2018.
Maana
yake Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij, sasa atakuwa anaendelea kupokea mshahara
huku akila 'bata' tu, anakwenda na kurudi kwao kwa kuwa Tanzania ni wajinga
waliwao.
Kuna
timu nchi ambazo hakuna aliyezitarajia kucheza Kombe la Mataifa Afrika. Angalia
Guine, Botswana na hata Cape Verde ambayo haifikishi hata watu milioni moja.
Nao wamecheza, sisi tuko hapahapa na huenda njia rahisi ni kuomba kuandaa.
Mimi
ninaumia kwa kuwa ni mshindani, ninaona timu za wenzetu zinaendelea kufanya
vizuri, waliokuwa wakifanya vibaya wanabadilika na kufanya vyema, ambao
hawakuwahi kufuzu sasa wanafuzu, sasa ni wakati wa sisi pia kubadilika.
Malinzi
afanye kitu, ikiwezekana awatupe washauri wake ambao sasa wanauza maneno lakini
ukweli wamefeli kwa kumshauri madudu kibao yakiwemo ya Taifa Stars maboresho
ambayo tayari imepotea.
Halafu
aanze mchakato wa uchunguzi kuzaa jibu la nini hasa cha kufanya ili kubadilika kutoka
katika kichwa cha mwendawazimu sugu kupita kiasi hadi watu wanaoweza
kubadilika.
Inawezekana,
lakini haiwezi kuwa kirahisi hivyo kama wanavyofikiria na hasa hiyo timu ya
washikaji ambayo inazidi kuvurunda. Mimi nachangia kidogo tu, kwamba nguvu
kubwa lazima iwe kwa vijana.
Angalau
wakati wa Tenga, vijana walipewa nguvu na ndiyo hao kina Thomas Ulimwengu na
wenzake ambao sasa ni tegemo. Lakini wakati wake Malinzi, hakuna la maana,
hakuna vijana na soka la wanawake kwishney. Maana yake, tutaendelea kusubiri
milele na miaka ndiyo inazidi kwenda, nimechoka, tumechoka!
Tatizo lako saleh ni chuki kwa aliyekutishia chatu!Wakati wa tenga TFF iliitwa Tafuna Fedha Fasta,sasa unataka kuturudisha kulekule.Walipewa mapesa mengi hadi wakakimbilia kugombea ubunge,angalia mahekaru waliyojenga kutokana na TFF au nawe ulikuwa unapata kiasi chake?
ReplyDeleteTenga hajafanya lolote la maana zaidi ya kuweka mahusiano mabovu na timu pamoja na wachezaji,kama macho uoni basi masikio yako yalisikia pale waandishi wa habari walipozuiliwa kuingia uwanja wa taifa kuripoti mechi.
Saleh unategemewa acha kutumika kupotosha watu,Tenga ni zaidi ya gunia!