MALIMA |
UNAPOTAJA majina ya wachezaji wa zamani wa
Yanga, itakuwa ni suala gumu kama hutamtaja beki kisiki, Bakari Malima ‘Jembe
Ulaya’.
Malima ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji
vikubwa vya kucheza soka na umasikini ndiyo ulichangia ajitume zaidi katika
mchezo huo.
Malima alianza kucheza soka kwenye timu ya
Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) akiwa kibarua kwenye shirika hilo
ingawa lengo lake lilikuwa kumuwezesha kupata ajira.
Anasema haikuwa kazi rahisi kwake kupata ajira
kama alivyokuwa akifikiria, hali iliyomfanya aondoke mwaka 1990 kwenda Pan
African iliyokuwa inafundishwa na Syllersaid Mziray ‘Mwanangu’.
Lakini huko nako alipata wakati mgumu wa kuweza
kucheza baada ya timu hiyo kupanda ligi kuu mwaka 1994 na kusajili nyota wengi
waliokuwa wakicheza ligi kuu kama Makumbi Juma na Isihaka Hassani ‘Chuku’.
Ehh! Kizota amvuta
Yanga
Moja ya mambo yaliyonifanya nisajiliwe na Yanga
ni kutokana na uwezo niliouonyesha katika mchezo wa ligi nilipokuwa na Pan
tulipocheza na Yanga. Nilifanikiwa kumkaba vema mshambuliaji wa timu hiyo, Said
Mwamba ‘Kizota’.
Unajua Said Mwamba ndiye aliyesababisha mimi
kusajiliwa Yanga baada ya kumkaba vya kutosha na hakuweza kutembea kama
ilivyokuwa kawaida yake lakini kocha Mziray alinipa jukumu hilo halafu ndiyo
ilikuwa mechi yangu ya kwanza.
Kilichotokea hakuna aliyeweza kuamini kwani
Yanga walimtuma aliyekuwa katibu wao kipindi hicho, Mpondela ambaye ndiye
alifanikisha usajili wangu Yanga.
Alicholipwa na Yanga
Daah! Wakati ule hakukuwa na mishahara ya
kulipana kwa mwezi zaidi ya timu kutegemea mapato ya mlangoni, hakukuwa na wa
kuwalipa mishahara wachezaji. Sasa ilikuwa inategemea na kinachopatikana.
Hata usajili wenyewe haukuwa katika ‘system’ ya
hivi sasa ambapo unakuta mchezaji anasaini mkataba wa miaka miwili au mitatu,
sisi ilikuwa kila ligi ikimalizika unasajili tena.
MALIMA (WA PILI KUSHOTO) WALIOCHUCHUMAA, NONDA SHABANI 'PAPII' WA TATU KUSHOTO WALIOCHUCHUMAA WAKIWA NA KIKOSI CHA YANGA. |
Alitoroka Yanga na
Nonda
Unajua wakati ule Yanga tulikuwa na timu nzuri,
mwaka 1996 tulikuwa tunashiriki kwenye Kombe la Washindi, tulikutana na Vaal
Professional ya Afrika Kusini.
Katika mechi ya kwanza ugenini tulipata sare ya
mabao 2-2, walipokuja hapa tulitoka 1-1.
Jamaa wakavutiwa na mimi Nonda Shabani ‘Papii’,
wakazungumza na viongozi lakini Katibu wa Yanga, George Mpondela na katibu mwenezi wa wakati huo, John
Ungelle walikataa kwa sababu ya kuhofia kufukuzwa kazi na wanachama kama
wangeturuhusu.
Viongozi walituficha, tulipogundua tukaamua
kutoroka kuelekea Afrika Kusini baada ya kuonana na wale viongozi wa Sauz hapa
Dar.
Kutoroka halikuwa jambo rahisi, kwa sababu
ilitulazimu kuvaa mavazi ambayo ilikuwa ngumu kugundulika kwa kuwa tulisafiri
kwa basi mpaka Zambia halafu kule ndiyo tukapanda ndege hadi Afrika Kusini.
Yanga yamnyima ITC
Viongozi wa Yanga waligoma kutoa Hati za
Uhamisho (ITC) ambazo zingeturuhusu kucheza kule kwa kuwa tulitoroka, Nonda
akaamua kuomba kwao Congo, akapata.
Nikajaribu kuomba Fat (sasa hivi ni TFF),
lakini Mwenyekiti Mhidin Ndolanga naye akaniwekea ngumu kwa kuwa hakuwa na
ruhusa ya klabu.
Nonda alinishauri kuwa, nimwambie rafiki yake
ambaye ni Mrundi ili aniombee kibali cha ukimbizi anayetokea Congo ili nipate
kibali, jambo hilo lilikuwa gumu kwangu kwa kuwa nilijua kuna suala la kubadili
uraia.
Mwisho wake ilibidi nirudi Bongo, cha
kushangaza walinipokea vizuri na mambo yakaendelea vizuri.
Akamatwa kwa madawa,
Yanga yamuokoa
Mwaka 1997 niliwaomba Yanga wasinisajili ili
nirudi tena Afrika Kusini kwenye ile timu, walinielewa na kuniruhusu,
nilipofika kule nikasaini mkataba wa miaka mitatu lakini sikuwa na kibali cha
kufanyia kazi, nikarudi.
Sasa wakati natoka Uwanja wa Ndege wa Dar es
Salaam, kuna mtu alinisimamisha mwanzoni nilimkatalia lakini baadaye nilikubali
ambapo alinichukua mpaka ofisini kwake ila haikupita muda wakaja wenzake kama
15.
Wakaniambia kuwa wao ni maofisa wa usalama
wanaohusika na kuzuia madawa ya kulevya na wakaomba wanipekue lakini hawakupata
kitu chochote kibaya sasa ikabidi waniambie kuwa jana yake kuna mtu wamemkamata
na mizigo ndiyo akawaambia ni yangu.
Ikabidi wanishikilie huku taratibu za
kunipeleka mahakamani Kisutu pamoja na yule jamaa aliyenitaja zikianza,
tulinyimwa dhamana lakini jamaa zangu na viongozi wa Yanga walishughulikia
wakatuachia kwa dhamana.
Sasa Yanga walichokifanya ni kuniletea fomu za
usajili lakini waliniambia kuwa nichague moja Yanga au Keko (gerezani), kwa
kweli sikutaka kuuliza kitu chochote zaidi ya kusaini.
Nashukuru kesi ilimalizika na nikaachiwa huru
kutokana na kukosekana kwa ushahidi na Yanga walinisaidia sana.
Mafanikio ndani ya
Yanga
Namshukuru Mungu tulifanikiwa kuchukua mara
mbili ubingwa wa ligi na Kombe la Muungano mara moja lakini 1999 tukachukua
ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati nchini Uganda baada ya kuwafunga Sports
Club Villa.
Unajua wakati ule mambo hayakuwa mazuri sana,
kwani ilifika wakati wanachama na mashabiki walikuwa wanachanga fedha kwa ajili
ya kutupatia chakula klabuni na ilikuwa inaongeza mwamko kwa wachezaji.
Mechi ya kukumbukwa ni dhidi ya Simba
mwaka 1996 Mwanza katika Kombe la Hedex, kwanza
kurudi kwa Edibily Lunyamila kutoka Ujerumani alipokwenda kufanya majaribio,
viongozi waliamini bila yeye tutafungwa na walimshawishi mpaka akaja kucheza,
sikuamini jamaa amekuja kuungana nasi.
Pili, kuna muda niliruka juu pamoja na Dua Said
wa Simba ile tulipofika chini Dua akawa amezimia, alichukua zaidi ya saa 12
kuzinduka, mechi hiyo tulishinda na nilifunga pia.
Baada ya mechi wote walienda disko ila mimi
nilishindwa mpaka niliposikia Dua amezinduka, saa nane usiku.
Kugomea mapato ya
mechi
Ilikuwa dhidi ya Simba, Mwanza katika Kombe la
Hedex, viongozi walileta mapato kidogo tofauti na idadi ya mashabiki walioingia
uwanjani.
Kuna kiongozi mmoja Mhindi ndiye alipewa fedha
kuja kutugawia, shilingi 50,000 kila mchezaji lakini tulizikataa na kumwambia
arudi tena kwa viongozi waliomtuma.
Hata aliporudi hakukuwa na mabadiliko, tukaamua
kumfungia chumbani na kutishia kumuua, ilibidi awapigie simu viongozi ambapo
waliongeza ile fedha na kufikia laki tatu kwa kila mchezaji.
Kizota amkunja kocha
ndani ya ndege
Wakati tunatoka Mwanza kurudi Dar, rubani
alilazimika kushusha ndege Arusha baada ya Said Mwamba ‘Kizota’ kumkunja kocha wetu (jina
linahifadhiwa), tukiwa angani.
Sasa tilipotua Arusha ndege ililazimika kuzingirwa
na polisi ila baada ya kugundua kuwa ni wachezaji wa Yanga, wakaanza
kushangilia kutokana na kuwa tumewafunga Simba, rubani alipoona vile aligoma
kurusha ndege tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment