YANGA ni klabu kongwe zaidi ya soka hapa
nchini na ndiyo inaaminika kuwa yenye wapenzi wengi zaidi kuliko nyingine zote
hapa nchini.
Mpinzani mkubwa wa Yanga ni Simba, kwa kuwa
ndiyo klabu kongwe zaidi kuliko nyingine zote nchini zinazokubalika zaidi.
Kukubalika kwa Yanga na Simba ni suala la
historia na rekodi, kwa kifupi ni klabu za wananchi ndiyo maana unaona
zinachipuka klabu zenye fedha na zinazojitahidi kwa mengi kama Azam FC, lakini
bado hazifikii ukubwa hata robo ya Yanga na Simba.
Wapo ambao wamekuwa wakikasirika kuona Yanga
na Simba zinakuwa kubwa na huenda wanataka kuupokonya ufalme huo kwa siku moja
au mbili, ni kujidanganya badala yake wanatakiwa kufanya kazi ya ziada.
Maana hata wale wanaopambana na ukubwa wa
Yanga na Simba kwa kuwa wako Azam FC, Mtibwa Sugar au kwingine, hakika
walianzia kupenda mpira kupitia klabu hizo mbili, kwingine wamehamia kwa ajili
ya ajira au kuhamisha tu mapenzi.
Huo ni mfano tu, ninacholenga ni kutaka
kukumbusha ukubwa wa klabu kama Yanga, kwamba haikuanza hivihivi kirahisi tu.
Kuna watu wameumia hadi kufikia ilipo sasa.
Maisha ya Yanga yamekuwa ni kama wale
wanariadha wanaopokezana vijiti, kwamba baada ya fulani atapewa huyu, baada ya
muda tena anachukua yule.
Hii ni kawaida na mafanikio ya klabu
yanaendana na wale waliopo baada ya kupita waliotoka. Sasa tunazungumzia
waliopo ndani ya klabu na hasa wanachama.
Wao ndiyo wenye deni kubwa la kuiendeleza Yanga
kwa kuwa wanatakiwa kuwa na mawazo endelevu au chanya na si yale yasiyozaa
lolote au hasi.
Kuna watu wengi ndani ya Yanga wamekuwa
wakijisifia kuhusiana na mapenzi yao kwa klabu, lakini ukweli wanajali maslahi
yao na wanaangalia wanaweza kupata zaidi nini si Yanga itapata nini kusonga
mbele, hawa ni sumu.
Wako ambao wanafanya kila kitu kuona Yanga
inaendelea na hii ni kutokana na mapenzi yao ya dhati kwa klabu ambayo
wanaamini ni furaha ya mioyo yao, ndiyo maana wako tayari kujitolea.
Wamepita watu wengi walioichangia Yanga, ndiyo
maana waliopo sasa wameikuta vile. Bado wako wenye mioyo ya kutaka kuiona
inaendelea na wanataka kujitolea, basi waungwe mkono.
Wote wanaoigeuza Yanga mtaji, nawaita sumu kwa
kuwa kuiua ni kuchangia kuporomoka kwa mpira nchini kwa kuwa wengi watakatishwa
tamaa.
Kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya kitu hasa
kinachohusisha utaifa ni jambo jema, hivyo wale wanaojali matumbo yao kwa
kisingizio kuwa wanaipenda Yanga au wametoka nayo mbali, ni simu ya maendeleo
ya klabu hiyo na wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutengeneza wimbo wa
majungu kwa kila viongozi wanaotaka kujitolea.
Kuipenda Yanga bila ya kuichangia lolote ni
kuidanganya nafsi, kuiunga mkono bila ya kusaidia lolote pia ni unafiki. Lakini
kuwakubali viongozi au watu ambao wanaimaliza Yanga kwa kuwa utafaidika, wewe
ni sumu, jitambue.
Mafanikio ya Yanga lazima yatapatikana kupitia
Wana Yanga wenyewe na si vinginevyo. Hivyo kila anayeamini kweli anataka
maendeleo ya Yanga, basi ajipigie hesabu na kuangalia kwamba kipi amewahi
kukifanya kwa ajili ya kuisaidia klabu yake.
Ilipofikia Yanga sasa, ni robo ya
inachostahili kwa kuwa ndani ya Wanayanga, wako ambao ni sumu na wanatafuta
maendeleo yao na si ya klabu. Basi vizuri watafutiwe maziwa ili kuinusuru iweze
kwenda na kasi sahihi ya maendeleo, wanaoonekana wanataka kusaidia maendeleo,
waungwe mkono kwa kuwa hapa ilipo kwa hesabu tokea mwaka 1935, inaonekana
imechelewa.
0 COMMENTS:
Post a Comment