KESHO ndiyo ile siku,
imesubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, wengi walianza
kuisubiri mara tu baada ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kutangaza ratiba ya
Ligi Kuu Bara msimu mpya.
Imekuwa ni kawaida, kila
inapotangazwa ratiba mpya ya Ligi Kuu Bara, wengi huangalia mechi mbili kali
zitachezwa lini, hakuna ubishi ni Yanga dhidi ya Simba na Simba dhidi ya Yanga.
Mechi hizo ni kubwa, hakuna
anayeweza kubisha na kwa kuwa pamoja na kasoro luluki ambazo tumekuwa tukipata
kwa klabu hizo kongwe, lakini si rahisi kukataa kwamba zinakubalika na ndiyo
kina baba wa soka nchini.
Mashabiki wengi wa soka
nchini ambao kwa asilimia 95 wanaziunga mkono timu hizo mbili wamekuwa
wakitamani zikutane ili kupata burudani ya watani wa jadi ambayo huanzia siku
kadhaa kabla ya mechi, uwanjani kabla ya mchezo, mchezo wenyewe na baada ya
kwisha.
Kuna mambo mengi sana
ambayo ni nadra kuyaona kwenye mechi nyingine zaidi ya hiyo inayowakutanisha
watani kutoka Manispaa ya Ilala, lakini wanasimamisha shughuli za nchi nzima,
watu wakitaka kuwaona wanapambana.
Kinachofurahisha ni kwamba,
pamoja na mashabiki hao kutaka kuziona zikicheza, hakuna yeyote kutoka upande
wowote ambaye anaweza kuwa tayari kuona timu yake inapoteza mchezo kwa kuwa
anaamini anashabikia kikosi bora zaidi.
Utamu ni kwamba moja ya mechi ngumu kutabirika ni hiyo
ya watani, hivyo mashabiki huenda na uhakika uwanjani wakiamini watashinda
kutokana na namna wanavyoziamini timu zao, lakini mpira hauna matokeo ya asilimia
mia kabla haujachezwa.
Wanaokwenda uwanjani
wakijiamini watashinda, wamekuwa wakichukizwa sana pale wanapopoteza, hali hiyo
imesababisha tafrani ya kila aina katika vikosi vya timu hizo iwe Yanga au
Simba, hali ambayo imekuwa ikizua hadi uadui.
Kawaida katika soka, lakini
kuwe na makosa ili mmoja apoteze. Lazima kuwe na uzembe, ili upande mmoja
ufunge bao. Ndiyo kawaida ya mpira kuwa ni mchezo wa makosa, kawaida hilo
lazima litokee ili timu ifunge.
Kama mabeki, kipa au mmoja
wa wachezaji wa Yanga au Simba hatakosea, basi bao halitapatikana. Hiyo ni
asili ya mchezo wenyewe. Lakini jambo hilo linaonekana kutokukubalika hata
chembe kutokea kila upande na kama itatokea, basi tafsiri inakuwa tofauti.
Tafsiri kuu ya hilo ni
hujuma, anayeshindwa kufunga, au anayezembea au kufanya kosa ndiye anakuwa
mchawi, ndiye anakuwa adui wa mashabiki ikiwezekana kwa msimu mzima.
Wanachofanya ni kumuangushia machungu yao yote kwa muda wote huku akionekana ni
kama adui.
Hakuna ubishi, wachezaji wa
Yanga walifanya makosa katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, wakalala kwa mabao
2-0. Pamoja na kushinda dhidi ya JKT Ruvu na Prisons, bado walifanya makosa
pia, wangeweza kushinda mabao mengi zaidi.
Halikadhalika Simba, pia
nao walifanya makosa katika mechi zao zote tatu, upande wa ulinzi na hata
washambuliaji. Sare tatu hazikuwa saizi yao kwa kuwa walionyesha kuwa na kikosi
bora na kinachofanya vizuri. Lakini hakuna shabiki anayehoji makosa hayo kwa
nguvu hadi kusababisha uadui.
Kupoteza dhidi ya Yanga au
Simba kwa watani hao ni kidonda, kweli inauma na hakuna anayetaka kupoteza.
Lakini hakuna ujanja, kama timu hizo ni za soka, haziwezi kuukimbia mzizi mkuu
wa mchezo huo kuwa kuna kushinda, sare au kupoteza.
Itakapofikia mwisho, kuna
kila sababu ya mashabiki kukubali kuwa wamepoteza, wawape moyo wanajeshi wao
ili wafunge safari upya kwa kuwa ndiyo timu itakuwa imecheza mechi ya nne tu,
ziko nyingine 22 za ligi kuu mbele yao. Kuanza kutafuta mchawi ni kujivuruga
baadaye.
Utamaduni wa kutafuta
mchawi umekuwa kawaida, wakati mwingine umewakumba hadi baadhi ya viongozi.
Wakati umefika wa kuamini hata mechi ya watani ni sawa na nyingi za ligi
linapofikia suala la uwanjani. Tubadilike, kesho si mbali.
0 COMMENTS:
Post a Comment